Ibadhi.com

24 NYIRADI ZA WAKATI WA KULALA

I. Ayat Kursi. Kutoka kwa Abu Huraira R.A.A. kasema, "Mtume S.A.W. aliniwakilisha kuzichunga Zaka za Ramadhani, akaja mtu akawa anakichota chakula kile[1], nikamkamata nikamwambia, "Nitakupeleka kwa Mtume S.A.W."  (Hadithi hii ni ndefu, kwa ufupi Yule mtu akanieleza sababu yake halafu mwisho akasema), "Unapoenda kitandani kwako kulala soma Ayatul Kursiy, utaendelea kuwa na mlinzi kutoka kwa Allah, na wala hatokukaribia sheitani mpaka upambazukiwe na asubuhi” Mtume S.A.W. akaniambia, [2]"

صَدَقَكَ وَهُوَ كَذُوبٌ ذَاكَ شَيْطَان.

Maana yake, "Amesema kweli ingawa na yeye ni muongo. Huyo ni sheitani"

 

II. Aya mbili za mwisho za Surat al-Baqara[3]. Kutoka kwa Abi Masud R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W., [4]"

مَنْ قَرَأَ بِالْآيَتَيْنِ مِنْ آخِرِ سُورَةِ الْبَقَرَةِ فِي لَيْلَةٍ كَفَتَاهُ.

Maana yake, "Atakaesoma aya mbili za mwisho za Surat al Baqara usiku zitamtosheleza" Wanavyuoni wamekhitalifiana makusudio ya neno "Zitamtosheleza katika ibara hio" Baadhi yao wamesema zitamkinga na shari na yale yasiyopendeza, na wengine wakasema zitamtosheleza kwa kisimamo cha usiku, na wengine wamesema imekusudiwa ni kiwango cha chini cha kusoma katika Sala za usiku.

 

III. Surat al Ikhlas, Surat al Falaq, na Surat N`Naas. Kasema Urwa kutoka kwa Bibi Aisha R.A.A.H.,[5] "Mtume S.A.W. alikuwa kila usiku akitaka kulala, huvikusanya viganja vyake kisha akavisomea Qul huwallahu Ahad, Qul audhu birabbilfalaq, na Qul audhu birabbinnaas, na akavipulizia ndani yake, halafu anajipangusa navyo mwili wake kadiri atakavyoweza, kuanzia kichwani na usoni mwake na sehemu ya mbele ya mwili wake. Akifanya hivyo mara tatu.

 

IV. Kusabih, Kuhimidi, na Kukabir. Kasema Ali R.A.A. kuwa, "Mikono ya Fatima ilikuwa sugu (kuwa na sagamba) kwa ajili ya kusaga kwa kinu cha mkono. Na kulikuwa na mateka wa vita wengi kwa Mtume S.A.W. Fatima alikwenda kwa Mtume S.A.W. lakini hakumkuta, alimkuta Bibi Aisha R.A.A.H. na akamuelezea kuhusu ugumu wa maisha (yake). Alipokuja Mtume S.A.W., Bibi Aisha R.A.A.H alimulezea ujio wa Bibi Fatima R.A.A.H. Mtume S.A.W. alienda kwao. (akawakuta) Wamekwisha kwenda kitandani mwao. Akaendelea Ali R.A.A. kusema, "Tulijaribu kuinuka lakini Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akasema, "Kaeni juu ya vitanda vyenu" na akakaa baina yetu, na nikahisi ubaridi wa miguu yake juu ya kifua changu. Halafu akasema, "Jee nikuonyesheni kitu kilicho bora kuliko ya kile ulicho kiomba? Utakapo kwenda kulala basi usabih mara (SUB`HANALLAH) 33, na uhimidi (ALHAMDULILLAH) mara 33, na ukabiri (ALLAHU AKBAR) mara 34.  Na hiyo ni kheri kwenu kuliko kijakazi (mfanyakazi). 

V. Kutoka kwa Bibi Hafsa R.A.A.H. mama wa waumini kasema, "Mtume S.A.W. akitaka kulala anauweka mkono wake wa kulia chini ya shavu lake halafu anasema, [6]"

اللَّهُمَّ قِنِي عَذَابَكَ يَوْمَ تَبْعَثُ عِبَادَكَ.

Allahumma qini adhabaka yawma tab`athu ibaadaka.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu niepushe na adhabu Yako siku utakayo wafufua waja Wako".  Anasema hivyo mara tatu.

VI. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Alikuwa Mtume S.A.W. anaomba wakati wa kulala,[7] "

اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ السَّبْعِ وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ مُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ وَالْقُرْآنِ فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَيْءٍ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ أَنْتَ الْأَوَّلُ لَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ وَأَنْتَ الْآخِرُ لَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ وَأَنْتَ الظَّاهِرُ لَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ وَأَنْتَ الْبَاطِنُ لَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ وَأَغْنِنَا مِنَ الْفَقْر.

Allahumma Rabba ssamawaati ssabii, wa Rabba l`arshi l`adhiim, Rabbana wa Rabba kulli shain, mun`zila Tauraat, wal`Injiil, wal`Qur`aan, faaliqa l`habbi wa nnawa, Laa ilaha ila Anta, audhubika min sharri kulli shain anta aakhidhun binaasiyatihi, anta l`awwal laysa qablaka shaiun, wa anta l`akhiru laysa baadaka shaiun, wa dhdhaahiru laysa fauqaka shaiun, wa anta baatinu, laysa duunaka shaiun, iqdhi anna ddayn, waagh`ninaa mina l`faqr. 

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wa mbingu saba, na Mola wa Arshi tukufu, Mola wetu na Mola wa kila kitu. Ulieiteremsha Taurati, na Injili, na Quraani, Unaeiotesha (kuichana) mbegu na kokwa. Hakuna mungu anaepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe. Najikinga Kwako dhidi ya shari zote, Wewe ndie uliemiliki utosi wake[8], Wewe ni wa mwanzo hakuna chochote kile kabla Yako, Na Wewe ni wa mwisho, hakuna kitu baada Yako, na Wewe uko wazi hakuna chochote kile juu Yako, na Wewe umefichika hakuna chochote kile kilichojificha chini Yako. Tulipie madeni yetu na utuepushe na ufakiri”.

 

VII. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Alikuwa Mtume S.A.W. anaomba wakati wa kulala[9]."

}اللَّهُمَّ رَبَّ السَّمَوَاتِ السَّبْعِ وَرَبَّ الأرض وَرَبَّ الْعَرْشِ الْعَظِيمِ رَبَّنَا وَرَبَّ كُلِّ شَيْءٍ فَالِقَ الْحَبِّ وَالنَّوَى مُنْزِلَ التَّوْرَاةِ وَالْإِنْجِيلِ وَالْقُرْآنِ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ كُلِّ شَرِّ أَنْتَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهِ أَنْتَ الْأَوَّلُ فلَيْسَ قَبْلَكَ شَيْءٌ وَأَنْتَ الْآخِرُ فلَيْسَ بَعْدَكَ شَيْءٌ وَأَنْتَ الظَّاهِرُ فلَيْسَ فَوْقَكَ شَيْءٌ وَأَنْتَ الْبَاطِنُ فلَيْسَ دُونَكَ شَيْءٌ اقْضِ عَنَّا الدَّيْنَ وَأَغْنِنَا مِنْ الْفَقْرِ{.

Allahumma Rabba ssamawaati ssabii, wa Rabba l`arshi l`adhiim, Rabbana wa Rabba kulli shain, faliqa l`habbi wa nnawa, mun`zila Tauraat, wal`Injiil, wal`Qur`aan, audhubika min sharri kulli shain anta aakhidhun binaasiyatihi, anta l`awwal falaysa qablaka shaiun, wa anta l`akhiru falaysa baadaka shaiun, wa dhdhaahiru falaysa fauqaka shaiun, wa anta baatinu, falaysa duunaka shaiun, iqdhi anna ddayn, waagh`ninaa mina l`faqr. 

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu, Mola wa mbingu saba, na Mola wa ardhi, na Mola wa Arshi tukufu, Mola wetu na Mola wa kila kitu, Unaeitosha (kuichanua) mbegu na kokwa[10], Umeiteremsha Taurati, na Injili, na Quraani, Najikinga Kkwako na shari ya shari zote, Wewe ndie uliemiliki utosi wake, Wewe ni wa mwanzo hakuna chochote kile kabla Yako, na Wewe ni wa mwisho hakuna kitu baada Yako, na Wewe uko wazi hakuna chochote juu Yako, na wewe umefichika hakuna chochote kilichojificha chini Yako. Tulipie madeni yetu na utuepushe na ufakiri.

     

VIII. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Kasema Abu Bakar Sidiq R.A.A. kumuambia Mtume S.A.W., "Niamrishe kitu nikiseme nikipambazukiwa na asubuhi na wakati wa jioni". Akasema (kumjibu), "Sema,[11] "

اللَّهُمَّ عَالِمَ الْغَيْبِ وَالشَّهَادَةِ فَاطِرَ السَّمَوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّ كُلِّ شَيْءٍ وَمَلِيكَهُ أَشْهَدُ أَنْ لَا إِلَهَ إِلَّا أَنْتَ أَعُوذُ بِكَ مِنْ شَرِّ نَفْسِي وَمِنْ شَرِّ الشَّيْطَانِ وَشِرْكِهِ. وَأَنْ أَقْتَرِفَ عَلَى نَفْسِي سُوءًا أَوْ أَجُرَّهُ إِلَى مُسْلِمٍ.

Allahumma a`alima l`ghaybi washaahada, faatira ssamawaati wal`ardh, Rabba kulli shain wa malikahu, ash`hadu an laa ilaha illa anta, audhubika min sharri nafsi, wamin sharri shaitani wa shirikihi. Wa an aqtarifa ala nafsi su`an au ajurrahu ila muslim .[12]"   

Maana yake, "Ewe Mola Mtukufu!, Mjuzi wa yaliyofichikana na yaliyo wazi, muumba wa mbingu na ardhi, Mola wa kila kitu, na Mmiliki wake, nakiri kwamba hapana mungu anaepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Wewe, Najikinga Kwako dhidi ya shari ya nafsi yangu, na shari ya shetani na ushirikina wake, na kuichumia uovu nafsi yangu, au kumsababishia Muisilamu uovu huo” Akasema, "Sema hivyo unapopambazukiwa na asubuhi na jioni na unapolala".

 

IX. Kasema Abdillah bin Umar R.A.A. alimuambia mtu anapolala aseme,[13] "

اللَّهُمّ (أَنْتَ) خَلَقْتَ نَفْسِي وَأَنْتَ تَتَوَفَّاهَا لَكَ مَمَاتُهَا وَمَحْيَاهَا إِنْ أَحْيَيْتَهَا فَاحْفَظْهَا وَإِنْ أَمَتَّهَا فَاغْفِرْ لَهَا اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْأَلُكَ الْعَافِيَةَ.

Allahumma anta khalaqta nafsi, wa anta tatawaffaha, laka mamaatuha wa mahyaaha, in ahyataha fahfadh`ha, wa in amattaha fag h`fir laha. Allahumma inni as`aluka l`afya. 

Maana yake, "Ewe Mwenyezi Mungu Wewe ndie Ulieiumba nafsi yangu, na Wewe ndie utakaeifisha, ni Kwako mauti yake (nafsi yangu) na uhai wake. Ukiiachia kuishi basi ihifadhi, na ikiwa Utaifisha isamehe. Ewe Mwenyezi Mungu nakuomba kukingwa na mabalaa".

Mtu mmoja akasema kumwambia, "Ulisikia hivi kutoka kwa Umar?. Akajibu akasema, "Kutoka kwa Mtume S.A.W."

 

X. Kasema Hudhaifa R.A.A., "Mtume S.A.W. anapokuwa kitandani kwake anasema, [14]"

بِاسْمِكَ اللَّهُمَّ أَمُوتُ وَأَحْيَا.

Bismika allahumma amuutu wa ahya.

Maana yake, "Kwa jina Lako Ewe Mola ninakufa na kuishi[15]".

 

XI. Kutoka kwa Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W., "Mmoja wenu akienda katika kilalio [16] chake (yaani akitaka kulala) basi akikung`ute kwa ncha ya nguo yake mara tatu na aseme,[17] "

بِاسْمِكَ رَبِّ وَضَعْتُ جَنْبِي وَبِكَ أَرْفَعُهُ إِنْ أَمْسَكْتَ نَفْسِي فَاغْفِرْ لَهَا وَإِنْ أَرْسَلْتَهَا فَاحْفَظْهَا بِمَا تَحْفَظُ بِهِ عِبَادَكَ الصَّالِحِينَ.

Bismika Rabbi wadha`atu jambi, wa bika arfa`uhu, in amskata nafsi fagh`fir laha, wa in arsaltaha fah`fadh`ha bima tah`fadhu bihi ibadaka ssalihiin.

Maana yake, "Kwa jina Lako Rabbi nimeuweka ubavu wangu, na kwa ajili Yako nitauinua. Ukiifisha nafsi yangu isamehe, na ukiirudisha (kuipa uhai) basi Ihifadhi kwa kile Unacho wahifadhia waja Wako wema".

 

XII. Kutoka kwa al- Baraa bin Azib R.A.A. kasema, "Kaniambia Mtume S.A.W., "Unapokwenda kulala basi tawadha, ikisha ulale kwa ubavu wako wa kulia na useme,[18] "

اللَّهُمَّ أَسْلَمْتُ نَفْسِي إِلَيْكَ وَفَوَّضْتُ أَمْرِي إِلَيْكَ وَأَلْجَأْتُ ظَهْرِي إِلَيْكَ رَهْبَةً وَرَغْبَةً إِلَيْكَ لَا مَلْجَأَ وَلَا مَنْجَا مِنْكَ إِلَّا إِلَيْكَ آمَنْتُ بِكِتَابِكَ الَّذِي أَنْزَلْتَ وَبِنَبِيِّكَ الَّذِي أَرْسَلْتَ.

Allahumma aslamtu nafsi ilaika, wa fawadhtu amri ilaika, wa alj`atu dhahri ilaika, rahbatan wa raghbatan ilaika, la malja`a wala manjaa minka ila ilaika, amantu bikitabika l`ladhi anzalta, wa bi Nabiyyika ladhi arsalata.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu nimeisalimisha nafsi yangu Kwako, na mambo yangu nimekukabidhi Wewe, na nimeugemeza mgongo wangu Kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila Kwako, nimekiamini kitabu Chako ulicho kiteremsha, na Mtume Wako uliyemtuma”

Akaendelea kusema, "Basi ukifa utakuwa umekufa katika fitra (uisilamu), yafanye maneno hayo yawe ndio maneno yako ya mwisho kuyatamka".

 

XIII. Au aseme,[19] "

اللَّهُمَّ إِنِّي أَسْلَمْتُ نَفْسِي إِلَيْكَ وَفَوَّضْتُ أَمْرِي إِلَيْكَ وَوَجَّهْتُ وَجْهِي إِلَيْكَ وَأَلْجَأْتُ ظَهْرِي إِلَيْكَ رَغْبَةً وَرَهْبَةً إِلَيْكَ لَا مَلْجَا وَلَا مَنْجَا مِنْكَ إِلَّا إِلَيْكَ آمَنْتُ بِكِتَابِكَ الَّذِي أَنْزَلْتَ وَنَبِيِّكَ الَّذِي أَرْسَلْتَ.

Allahumma inni aslamtu nafsi ilaika, wa fawadhtu amri ilaika, wajah`tu wajhi ilaika wa alj`atu dhahri ilaika, raghbatan wa rahbatan ilaika, la malja wala manjaa minka ila ilaika, amantu bikitabika l`ladhi anzalta, wa bi Nabiyyika ladhi arsalata.

Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu nimeisalimisha nafsi yangu Kwako, na nimekukabidhi Wewe mambo yangu, na nimeulekeza uso wangu Kwako, na nimeugemeza mgongo wangu Kwako, kwa matarajio na kwa kukuogopa, hapana sehemu ya kukimbilia wala ya kujiokoa ila Kwako, nimekiamini kitabu Chako ulicho kiteremsha na Mtume Wako uliyemtuma”

 [1] Bila kuwa na idhini.

[2] Bukhary 15/413 (4624)

[3] Suratil Baqara aya ya 285, na aya ya 286.

[4] Bukhary 15/413 (4624).

[5] Ttirmidhiy 11/270 (3324).

[6] Abu Dawud (4388).

[7] Ahmad 22/47 (10503).

[8] Inakusudiwa Wewe ndie unaemuendesha mwanadamu katika yale anayoyafanya. Na imethibiti kuwa sehemu ya mbele ya utosi ni sehemu yenye vituo kadhaa vya akili ambavyo vinatofautiana kwa upande wa eneo na kazi. Kama ifuatavyo: Utandu wa mbele wa utosi (Pre-Frontal Cortex), uko moja kwa moja nyuma ya paji la uso, nao ndio sehemu kubwa ya sehemu ya mbele ya ubongo na kazi yake inashikamana na kujenga haiba ya mtu. Pia ina athari kubwa katika kuainisha hatua (Initiative) na hukumu (Judgment). Halafu kuna sehemu ya kuendeshea maneno ya broka (Motor Speech Area of Broca) yenye kuratibu harakati baina ya viungo vinavyoshiriki katika zoezi la usemaji mfano wa koo, ulimi na uso. Halafu kuna maeneo ya harakati yanayo kusanya sehemu ya mbele ya jicho (Frontal Eye Field) ambayo hutoa msukumo unao ambatana na macho kuelekea kwenye upande unao kabiliana nao na sehemu ya kuendeshea viungo vikuu na visaidizi (Primary & Secondary Motor Areas). Sehemu zote hizo mbili ni zenye kuhusika na matakwa ya viungo. Kujeruhiwa kwake, kunaweza kusababisha mporomoko wa vigezo vya tabia, kiwango cha kumbukumbu na uwezo wa kutatua matatizo ya akili.  

[9] Tuh`fat al`Abrar mlango wa nyiradi zinazosomwa wakati wa kulala. Abu Dawud 13/246 (4392), Ibn Maajah 11/338 (3863).

[10] Ukaisababisha kuota.

[11] Abu Dawud 13/262 (4405).

[12] Ibara hii ya mwisho imeongezwa na Ahmad 1/80 (77).

[13] Muslim 13/238 (4887).

[14] Bukhary 19/394 (5849).

[15] Makusudio nina lala na ni amka.

[16] Inaweza kuwa kitanda, godoro, mkeka na kadhalika.

[17] Bukhary 22/395 (6844).

[18] Bukhary 19/372 (5836).

[19] Tufhat al`Abrar nyiradi zinazosemwa wakati wa kulala.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment