Ibadhi.com

Nini hukumu ya wale wanaoacha kuhudhuria sala ya Ijumaa ?

Nini hukumu ya wale wanaoacha kuhudhuria sala ya Ijumaa ? Ni kiasi gani cha masafa ambayo mtu husameheka kuhudhuria Ijumaa ? Je imamu anaweza kuwahoji wasiohudhuria Ijumaa ? Na je wachukiwe kwa ajili ya Allah wanaoacha kuhudhuria Ijumaa bila udhuru ? Tupe fatwa Mstahiwa Sheikh na Allah akulipe malipo bora na mema kabisa.

Allah Taala amesema :{Enyi mlio amini! Ikiadhiniwa Sala siku ya Ijumaa, nendeni upesi kwenye dhikri ya Mwenyezi Mungu, na wacheni biashara. Hayo ni bora kwenu, lau kama mnajua}Na imesihi katika hadithi kutoka kwa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- kuwa kasema : « Lazima watu waache kuziepuka sala za Ijumaa au Allah atazipiga muhuri nyoyo zao kisha watakuwa miongoni mwa walioghafilika ». Pia kasema : « Atakaewacha Ijumaa tatu mfululizo Allah ataupiga chapa moyo wake ». Na imekuja kutoka kwake –rehma za Allah na amani zimshukie- katika riwaya aliyoitoa Ibnu Maajah kupitia kwa Jabir bin Abdallah –Allah amridhie- kwamba yeye –rehma za Allah na amani zimshukie- kasema : « Na jueni kuwa Allah amekufaradhishieni Ijumaa katika kisimamo changu hiki katika siku yangu hii katika mwezi wangu huu wa mwaka wangu huu hadi siku ya kiyama. Atakaeiwacha katika uhai wangu au baada yangu naye ana imamu muadilifu au si muadilifu kwa kuidharau au kuikanusha basi Allah asimkusanyie yake yaliyotawanyika, wala asimbarikie mambo yake, tena huyo hana sala, wala hana zakaa, wala hana hija, wala hana saumu, wala hana wema, mpaka atubu; kwani mwenye kutubu Allah humkubalia toba".Imamu Abu Sufyan Mahboub bin A'Ruhail –Allah amrehemu- ametaja kwamba watu wa Oman walimwandikia Imamu Abu A'Sha'thaa –Allah amridhie- wakimuomba fatwa kukhusu Ijumaa, je inamlazimu aiendee yule ambaye haisikii adhana yake? Akawajibu: Kama hawaiendei ila wanaosikia adhana yake wangalikuwa wachache wanaoiendea; bali inaendewa kutoka masafa ya farsakhi mbili na tatu. Kisha imethibiti kutoka kwa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- kuwa aliazimia kuzichoma moto nyumba za wanaowacha kuhudhuria sala ya Ijumaa kama alivyoazimia kuzichoma moto nyumba za wanaowacha kuhudhuria sala ya jamaa. Na hakuazimia –rehma za Allah na amani zimshukie- kuzichoma moto nyumba zao isipokuwa kwa kuwacha kwao lililo wajibu juu yao. Na katika haya kuna dalili ya kwamba imamu ana haki kuwahoji watu kukhusu sababu za kuto kuhudhuria kwao sala ya Ijumaa na ya jamaa, bali ana haki kuwapa adabu kwa hayo. Na mwenye kuendelea kuwacha Ijumaa bila udhuru itawajibika achukiwe kwa ajili ya Allah kwa kuacha kwake kilicho wajibu juu yake. Na Allah anajua zaidi.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment