Ibadhi.com

KURUDIA SALA NA KUILIPA : 1

Je inasihi kurudiwa sala iliyotenguka kwa jamaa au irudiwe na kila mtu peke yake?Sioni kinachozuia kurudiwa sala kwa jamaa ikibatilika, ingawa idadi kadha ya maulama wanaona kinyume na hivo. Kwani katika baadhi ya mapokezi kutoka kwa 'Umar –Allah amridhie- kwamba alirudia sala kwa jamaa katika wakati usio wa sala hiyo, kama alivofanya hivo Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- katika vita vya handaki aliposali adhuhuri na alasiri na magharibi katika wakati wa isha kwa jamaa. Wala siwaoni wale waonao rai tafauti na hii isipokuwa wamo katika kuiga pasina kuzingatia msingi waliojengea rai yao. Kwani wao wameona katika yaliyopokewa kwa baadhi ya wenye ilmu uchukivu wa kukariri jamaa katika msikiti mmoja, wala hawakukusudia kwa hilo isipokuwa kuukata mzizi wa mfarakano baina ya jamaa mbali mbali kwa kukhofia kwamba wanaotafuta mfarakano watapata njia ya kuufikia kwa kupitia jamaa zaidi ya moja, ambapo baadhi yao watajichelewesha makusudi wasisali katika jamaa ya mwanzo kwa ajili ya kuanzisha jamaa ya pili, na kwa namna hii umoja huvunjika, mfarakano huibuka na hikma ya kuwekwa sharia ya sala ya jamaa hutoweka, nayo ni umoja, kuondosha tafauti na kuunganisha nyoyo. Hapana shaka kuwa rai yao hii imetegemea msingi maarufu katika fiqhi, ambao ni kufunga milango ya uharibifu. Hilo ni jambo linalozingatiwa katika malengo ya Sharia Tukufu, na kwa hiyo si ajabu wakiutumia msingi huo watu wetu na wengi kati ya watu wa madhehebu nyengine. Lakini sababu hii haipatikani lau kama jamaa ile ile itarudia sala yake kwa ajili ya kuharibika kwa jamaa, kwani jamaa ya mwanzo ndiyo ile ile ya pili na hakuna baya linaloogopewa katika jambo hili. Watasalije pamoja na hayo kila mmoja peke yake wakati hadithi za Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- zinahimiza kusali jamaa, na zinaonesha tafauti kubwa baina ya sala ya jamaa na sala ya mtu mmoja katika fadhila. Isitoshe, kauli sahihi ni kwamba sala ya jamaa ni wajibu 'aini' (juu ya kila mmoja) kwa dalili zisizopingika na nimezifafanua pahala pengine, itafaaje pamoja na hayo kusali kila mmoja peke yake? Kisha nionavyo mimi ni kwamba haikatazwi kusaliwa zaidi ya jamaa moja katika msikiti mmoja, japo haikuwa kwa ajili ya kurudia sala iliyotangulia pakiwa hapakhofiwi kukusudiwa kuleta mfarakano wa jamaa, kutokana na yaliyothibiti kutoka kwa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- kuwa alimuona mtu mmoja hakuiwahi jamaa akasema: "Je kuna ye yote atakayempa sadaka huyu kwa kusali naye". Hayo yanatosha kuwa hoja, na ikija hukumu ya Allah inabatilika hukumu ya watu. Na Allah anajua zaidi.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment