Ibadhi.com

9. TAFSIRI ZA MANENO YA KUFANANISHA

Basi ikalazimika kwa mujibu wa akili na sheria([1]) kuzichukua aya zenye maneno yenye kubeba maana za kufananisha kidhahiri na kuzirejesha  kwenye hukumu za yanayokubaliana na ukamilifu wa Allah mtukufu.

Basi Allah mtukufu ametueleza katika kuwa yeye hafikiwi na uwezekano wa kufanana na chengine chochote pale alipotuambia:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَىْء﴾

Hakuna mfano wake kitu chochote﴿

[Shuura 11].

Basi lau atafanana Allah mtukufu na kitu chochote katika sifa yoyote itakua ni kuvunja maana ya aya hii, na litapelekea hilo kugongana maelezo ya Qur-ani mgongano ambao haukubaliki kabisa, na hali Allah amekisifu kitabu chake kwa neno lake Havi hawazingatii hii Qur-ani? Na lau kuwa inatok1a kwa asiyekua Allah basi hakika wangalikuta ndani yake khitilafu nyingi﴿ [Nisaa 04/82].

 Kutokana na hayo ikawa ni haki kuzichukua Aya kwa mujibu wa ufahamu unaokubaliana na utukufu na ukamilifu wake Allah mtukufu..

Kwa mfano:-

 1. Neno lake Allah mtukufu Na amekuja Mola wako﴿ [Al-fajri 22] kuwa maana yake ni kuja Amri ya Mola wako.
 2. Neno lake Kwa Mola wake (nyuso) zinatazama﴿ [Qiyama 23] kuwa maana yake ni zinatazama malipo mazuri ya Mola wake, au  kusubiria kutoka kwa Allah idhini ya kuingia katika Pepo inayotoka kwake.
 3. Neno lake Na anakuhadharisheni Allah na nafsi yake﴿ [Al-imraan 28] kuwa maana yake ni Adhabu yake.
 4. Neno lake: Ameteremka nayo Roho wa kuaminiwa﴿ [Shuaraa 193] kuwa maana yake ni Jibrilu.
 5. Neno lake: Na ili ufanywe juu ya jicho langu﴿ [Taha 39] kuwa maana yake ni elimu yangu na hifadhi yangu.
 6. Neno lake: Kila kitu kitaangamia isipokua uso wake﴿ [Qasas 88] kuwa maana yake ni isipokua Allah, yaani dhati yake mwenyewe.
 7. Neno lake: Basi huko ndio kwenye uso wa Allah﴿ [Baqara 115] kuwa maana ya uso ni Allah mtukuful dhati yake mwenyewe.
 8. Neno lake: Na utabakia uso wa Mola wako﴿ [Rah-man 27] kuwa maana yake atabakia Mola wako mtukufu dhati yake na sio chengine chochote.
 9. Neno lake: Bali mikono yake iko wazi﴿ [Maida 64] kuwa maana yake ni neema zake za kidunia na kiakhera, au neema zake na uwezo wake vyenye kubaki.
 10. Neno lake: (Mbingu) zitakunjwa kwa wakulia wake﴿ [Zumar 67] kuwa maana yake zitaondoka kwa uwezo wake.
 11. Neno lake: Na Ardhi yote itakua katika fumbato lake﴿ [Zumar 67] kuwa maana yake ni zitakua katika uwezo wake.
 12. Na neno lake: Anafumba na kukunjua﴿ [Baqara 245] kuwa maana yake ni anazuia na anawepesisha.
 13. Na neno lake: Kwa yale niliyofanya katika ubavu wa Allah﴿ [Zumar 56] kuwa maana yake ni katika kuasi amri zake na kuacha kuumtii yeye.
 14. Na neno lake: Siku utakapofunuliwa mguu﴿ [Qalam 42] kuwa maana yake ni mazito ya siku ya Kiama, basi kukunjuliwa mguu ni kinaya cha mazito ya magumu ya siku hiyo.
 15. Na neno lake: Allah ni nuru ya Mbingu na Ardhi﴿ [Nuur 35] kuwa maana yake ni mwenye kuongoza yaliyomo ndani yake.
 16. Na neno lake: Basi alipojitokeza Mola wake katika Jabali﴿ [Al-aaraf 143] kuwa maana yake ni kuitokeza dalili ya Mola wake katika Jabali.
 17. Na neno lake Juu ya kiti cha enzi amekaa﴿ [Taha 5] kuwa maana yake ametawalia kila kitu kwa ufalme na ushindi na uendeshaji, na yeye ametawalia ulimwengu wote, basi akahusisha kiti cha enzi katika utajo ili iwe ni daraja maalumu kwa kiti hicho, na kwa sababu hicho kiti chote kimezungukwa na Malaika, na hakuna jengine isipokua hilo, kwa sababu Allah mtukufu hana sifa ya kuhitaji kitu, amejitosheleza kwa dhati yake.
 18. Na neno lake: Na amemsemeza Mussa msemo﴿ [Nisaa 164] kuwa maana yake ni kumsikilizisha sauti aliyoiumba ambayo alimfahamisha kwa sauti hiyo maneno aliyotaka.
 19. Na kuwa kwake karibu na viumbe﴿ ni kwa maana ya kuyajua yote yaliyoko upande wao, na kusikia kwake maombi yao, na wingi wa rehma zake upande wao, na hifadhi yake iliyoko kwao.
 20. Na kuwa kwake katika kila sehemu na wakati﴿ ni kwa maana ya kuwa yeye anavihifadhi vitu hivyo bila ya kupotea kitu katika elimu yake kwa vilivyomo humo na vinavyofanyika humo, basi vipi vimpotee na ilihali havikua isipokua kwa kuviweka yeye na kuvihifadhi yeye.
 21. Na kuwa kwake pamoja na vitu vyote﴿ ni kwa maana elimu yake imevienea vitu vyote.
 22. Na neno lake (s.a.w) Hakika Allah anaona haya kumuadhibu yule anayemtii﴿ ni kwa maana ametakasika na kulifanya hilo.


[1]. Ama kwa mujibu wa akili ni kwa kuyaondolea maneno maana zisizowezekana, na kulazimika kuyafahamu kwa mujibu wa maana inayokubaliana na walingwa wake; kwa hiyo ikalazimika kuzikataa na kuzikanusha maana zisizokubaliana na utukufu na ukamilifu wa Allah mtukufu, kisha ikalazimika kuyachukua maelezo yake kwa mujibu wa maana inayokubaliana na utukufu na ukamilifu wa Allah mtukufu.

 Ama kwa mujibu wa sheria ni kuwa: Allah mtukufu amezigawa Aya za kitabu chake vigao viwili:-

 1. Aya zilizokua ni muhakamaati (za kuhukumishwa zisizokubali maana zaidi ya moja), basi aya hizi ziko safi katika maelezo yake hazikubali utatanishi na mizozo, nazo ndio asili ya Kitabu.  
 2. Aya zilizokua ni mutashaabihati nazo ni zile zenye kubabaisha kwa kuchukua maelezo yake maana zaidi ya moja, au kufichika makusudio yake kwa kuwa na maana ya udhahiri na nyengine iliyofichika nayo ndiyo maana iliyokusudiwa, au ikawa maana iliyokusudiwa umefichika uhakika wake kabisa.

Basi Allah mtukufu ametubainishia kuwa wale wenye upotevu katika nyoyo zao, wao hufuata aya zenye kubabaisha (mutashaabihati) kwa kuhukumia mapenzi ya nyoyo zao ndani ya aya hizo, na hawa wamegawika makundi mawili:-

 1. Kundi moja katika hayo wanataka kueneza fitina katika jamii kwa kujishika na udhahiri wa aya ambazo makusudio yake yamebainishwa katika (muhkamaati) asili ya kitabu.
 2. Kundi la pili wao wanataka taawili, yaani tafsiri ya aya ambazo uhakika wake haukubainishwa kabisa katika muhakamaati.

Ama wale wenye maarifa mazuri ya kielimu wao mwanaziamini aya zote muhakamaati na mutashaabihaati, na njia yao katika kukifahamu Kitabu cha Allah mtukufu ni:-

 1. Kuzirejesha zile aya zilizobainishwa katika asili ya kitabu.
 2. Ama aya zilizokua hazikubainishwa katika muhkamaati, wao wanasema tumeamini, zote ni kutoka kwa Mola wetu, rejea [Ala imran 3/7].
Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment