Ibadhi.com

8. ALLAH MTUKUFU HAONEKANI.

Inalazimika kuitakidi kuwa Allah mtukufu ametakasika na uwezekano wa kuzungukwa na kiumbe chochote, au kumpata yeye kwa macho na kumuona.

Kwa hakika hakuna uwezekano wa kuonekana Allah mtukufu kwa sababu ya dalili zifuatazo:

KIAKILI

Katika malazimisho ya kuonekana kitu kiakili ni:

 1. Kupatikana rangi ya kupambanuka na vyengine.
 2. Kuhusika na sehemu fulani na wakati fulani.
 3. Kupatikana upande wa muelekeo na umbali na ukaribu usiopindukia mipaka.
 4. Kukizunguka kinachoonekana au kuipata kwa macho baadhi ya sehemu yake.

Na malazimisho hayo yote ni sifa za viumbe, basi haiwezekani hayo yawe ni katika sifa za Allah mtukufu, kwani Allah mtukufu si mwili wala umbo, wala hafanani yeye na chochote miongoni mwa viumbe vyake.

Basi vipi sifa hizo ziwe kwake Allah mtukufu:

﴿لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَىْء﴾

 Hakuna mfano wake kitu chochote﴿

 [Shuura 11].

 KUNAKILI

Dalili za kunakili ni zile za maandiko ya kisheria, nayo ni Qur-ani tukufu na Sunna ya Mtume wetu (s.a.w) nazo ni kama zifuatazo:

 • Amesema Allah mtukufu akiisifu dhati yake:

 ﴿لاَّ تُدْرِكُهُ ٱلاْبْصَـٰرُ وَهُوَ يُدْرِكُ ٱلاْبْصَـٰرَ وَهُوَ ٱللَّطِيفُ ٱلْخَبِيرُ﴾

 Havimdiriki yeye venye kuona, na yeye anavidiriki vyenye kuona; na yeye ni Mjuzi Mwenye khabari﴿

 [An-aam 103].

Kwa mujibu wa neno hili hakuna uwezekano wa Allah mtukufu kudirikiwa na vyenye kuona, na huo ndio ukamilifu  wake wa kidhati, na kudiriki chenye kuona hakumaanishi isipokuwa kuona kwake; kwani kudiriki kila kitu ni kwa mujibu wa kile kitu, basi kudiriki kwa akili ni kufahamu kwake, kudiriki kwa mkono ni kugusa kwake, kudiriki kwa sikio ni kusikia kwake, na kudiriki kwa jicho ni kuona kwake, basi maana ya neno hili la Allah mtukufu ni kuwa vyenye kuona yeye havimuoni, na Aya hii tukufu imezingatia wasifu wa kuona, basi ni sawa wasifu huo utakuwa katika jicho au moyo au akili au chochote kile kiwacho.

 • Amesema Allah mtukufu:

 ﴿وَلَمَّا جَاءَ مُوسَىٰ لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنْظُرْ إِلَيْكَ ۚ قَالَ لَنْ تَرَانِي وَلَٰكِنِ انْظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنِ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي ۚ فَلَمَّا تَجَلَّىٰ رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَىٰ صَعِقًا ۚ  فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِين﴾

Na alipokuja Mussa katika mikati (sehemu teuliwa kwa wakati teuliwa) yetu, na akasemezwa na Mola wake.

Akasema: "Mola wangu nioneshe mimi nikuone wewe"

Akasema: "Hutoniona, lakini litizame jabali, ikiwa litatulizana sehemu yake basi utainona"

Basi alipojitokezea Mola wake jabali akalijaalia kupasuka na akaanguka Mussa kwa mshituko na kuzimia.

Basi alipozinduka akasema: "Umetakasika, ninatubia kwako, na mimi ni wa mwanzo wa waumini"﴿

[Al-Aaraaf 143]

Aya hii ni andiko safi la hukumu ya Allah mtukufu kwa Mtume Mussa (a.s.w), ya kuwa Mtume Mussa (a.s.w) hatamuona Mola wake ambaye ni Allah mtukufu.

Basi ikiwa haiwezekani kwa Mtume Mussa (a.s.w) kumuona Allah mtukufu vipi itawezekana kwa mwengine?!!

Huenda mtu akasema: "Lau kuwa haiwezekani kuonekana Allah mtukufu asingelilitaka Mtume Mussa (a.s.w) kupatikana kwake"

Jawabu:
 1. Mazingatio ni katika aliyotueleza Allah mtukufu katika hukumu yake, na nani aliye mkweli zaidi kuliko Allah mtukufu.
 2. Lau kuwa Mtume Mussa (a.s.w) alitaka kumuona Allah mtukufu ni haki basi ungelithibiti uwezekano wa kuonekana Allah mtukufu hapa duniani, na kusingelikuwa na lawama kwa kaumu yake waliotaka kumuona Allah mtukufu; wala asingapatwa na yaliyompata, wala asingalitubia; kwani wangalikuwa wametaka jambo lenye uwezekano, na likibainika kuwa hayo hayawezekani itakuwa imethibiti kuwa Mtume Mussa (a.s.w) alilipeleka hilo kwa Allah mtukufu ili iwe hoja baina yake na kaumu yake ya kuwa hakuna uwezekano wa kuonekana Allah mtukufu; kwani ikiwa halikuwezekana kwake aliye mbora wao ambaye ni Mtume wao basi vipi litawezekana kwao walio chini kidaraja?!.

Huenda mtu akasema: "Hukumu ya kutoonekana Allah mtukufu ni ya hapa duniani tu, ama Akhera hukumu yake ni nyengine kwani tabia za Akhera na Duaniani ni tofauti"

Jawabu:
 1. Bila shaka kubadilika ni sifa ya viumbe nako ni kwa mujibu wa matakwa ya Allah mtukufu, kwa hiyo ni haki kusema kuwa tabia ya akhera ni tofauti na tabia ya hapa duniani, hili halina shaka ndani yake wala kutofautiana. Lakini jee! Allah mtukufu anasifika kwa uwezekano wa kubadilika?!! Bila shaka Allah mtukufu hasifiki kwa uwezekano huo; kwa sababu badiliko ni hali mpya iliyotokeza ambayo haikuwepo kabla, kwa hiyo badiliko lenyewe ni kiumbe, basi ukamilifu wa Allah mtukufu kabla ya kuumba na baada ya kuumba ni huo huo hauathiriki na mabadiliko ya viumbe wala haufikiwi na mabadiliko, hakika yeye si mwenye kufanana na viumbe vyake hapa duaniani, na huko akhera pia si mwenye kufanana na viumbe vyake, yeye ndiye Allah Mkwasi asiyehitaji hapa duniani na huko akhera pia; kwa hiyo mabadiliko ya kiakhera ni yenye kuathiri baina ya viumbe, na haiwezekani mabadiliko hayo kumuathiri Allah mtukufu, na kutoonekana Allah mtukufu ni wasifu wake wa kidhati kama alivyojisifu mwenyewe, na wasifu wake hauathiriki kwa mabadiliko ya wakati na sehemu.
 2. Aya tukufu imebainisha wazi wazi sababu ya kutowezekana kuonekana Allah mtukufu, na sababu hiyo ipo duniani na akhera, na sababu yenyewe ni kuhitajia sehemu; kwani Allah mtukufu ametoa hukumu mbili:
  1. Hukumu ya kwanza imo katika neno lake "Hutaniona" tuichukuwe kuwa hukumu hii ni ya wakati ule tu kimakadirio. Jee! Ni hukumu gani ya wakati unaofuatia wa baada ya wakati ule? Ni sawa wakati huo ni wa maisha haya ya duaniani au maisha ya Akhera. Jawabu yake ni kuwa iwapo jabali litatulizana katika sehemu yake basi ataonekana. Jee! Jabali lilitulizana? Bila ya shaka jabali halikutulizana; kwani lilipasuka pasuka na kutoweka. Kwa maana hiyo kama ilivyokua jabali halikutulizana sehemu yake vile vile haiwezekana kuonekana Allah mtukufu kwa wakati ujao.
  2. Bila shaka Jabali ni kiumbe kizito sana na kigumu sana, nacho ni kiumbe kilichokita zaidi katika sehemu yake husika, na kiumbe hichi kinashirikina na binadamu katika sifa ya kuhitajia sehemu ili kipatikane; kwa hiyo kuwepo sehemu ni sharti ya kuwepo binadamu kama ilivyokua ni sharti ya kuwepo jabali, hivo ndivo alivojaalia Allah mtukufuTukirudia katika Aya tukufu kunakutia kutajwa sehemu ya jabali ((Ikiwa (Jabali) litatulizana katika sehemu yake)), na tukija kwa upande wa pili Allah mtukufu ni Mkwasi (Asiyehitaji chochote) ametakasika na uwezekano wa kusifika kwa sifa yenye lazimisho la kuhitaji; kwa hiyo kuwepo kwake Allah mtukufu ni kuwepo kulikotakasika na kudhibitiwa na sehemu yoyote, na kwa maana hiyo inabainika wazi wazi kuwa ili uwepo uwezekano wa kuonekana Allah mtukufu ni lazima sehemu ikosekane au Allah aihitajie, na kwa sababu yote haya ni muhali katika haki ya Allah ndipo alipolitokezea jabali lililazimikiwa kukosa sehemu yake, na kwa hiyo likamalizika na kupasukapasuka na kutoweka; kwani lilikosa uwezekano wa kubakia kwa kukosa sharti ya kupatikana kwake ambayo ni sehemu ya kuwepo ndani yake.

Basi kama ilivyokua Allah mtukufu ametakasika na uwezekano wa kuhitajia sehemu na kudhibitiwa na sehemu na kufanana na kiumbe vile vile ametakasika na uwezekano wa kuonekana.

Ama kuhusu Aya za Suuratu Al-qiyaaham nazo ni

 ﴿وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ نَاضِرَةٌ * إِلَىٰ رَبِّهَا نَاظِرَةٌ﴾

 Nyuso siku hiyo ni zenye kumetameta (kun`gara) * kwa Mola wake ni zenye kuangalia﴿

  [Surat Al-Qiyama 22 – 23]

Kwanza: Hakuna katika Aya hizi dalili ya kuonekana Allah mtukufu siku ya kiama; kwani kuangalia hakulazimishi kuona, nako kunakubali maana nyingi ikwemo maana ya kusubiria na kutarajia, basi muangalio uliotajwa katika Aya hizo ni muangalio wa kusubiria na kutarajia, na sio muangalio wa kuona; kwa hiyo maana yake ni:

((Nyuso siku hiyo ni zenye kumetameta (kun`gara) * kwa Mola wake tu ni zenye kusubiria))

Maana hii ndiyo iliyo sahihi na inayokubaliana na utukufu wa Allah mtukufu, na ndiyo maana inayokubaliana na maelezo ya Aya hizo na nyenginezo katika Qur-ani tukufu; kwani maelezo yake yako wazi kabisa katika kuelezewa hala ya Waumini kabla ya kuingia watu wema katika Pepo na watu waovu katika Moto; kwa hiyo nyuso za watu wema siku ya kiama ni zenye fuaraha na kunawiri na bashasha huku zinasubiria aliyoyatayarisha Allah mtukufu kwa ajili yao, nayo ni Thawabu yake ya Pepo na yaliyomo ndani yake, na hali ya nyuso hizi imetajwa katika Aya nyengine za Qur-ani tukufu, kama ilivyyo mwisho wa Suratu Abasa (80/38-39)

﴿وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُّسْفِرَةٌ * ضَاحِكَةٌ مُّسْتَبْشِرَةٌ﴾

((Nyuso siku hiyo ni zenye bashasha. Nizafurahi zinajibashiria)).

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment