Ibadhi.com

7. SIFA ZAKE ZA DHATI NDIO DHATI YENYEWE

Allah mtukufu ni mwenye kusifika kidhati pia ni mwenye kusifika kivitendo.

Jee! Inawezekana kuwa sifa zake za kidhati sio dhati yake, kwa kusema kuwa sifa zake za kidhati zimesimama na dhati yake, au kusema kuwa sifa hizo ni ongezeko timilivu katika dhati yake Allah mtukufu?

Haiwezekani, ametakasika Allah na hilo; kwa sababu - kama itakuwa hivo - italazimika ya batili yafuatayo:

 1. Ima sifa ziwe zimemtangulia Allah mtukufu, na hili litalazimisha kuwa Allah hakuwepo kwani ametanguliwa na sifa zake katika uwepo; kwa hiyo atakuwa ni mwenye kuhitajia mtendaji wa kumuweka, na hilo litalazimisha batili ya kuwa yeye ni kiumbe chenye kuhitajia muumba, na hili liatalazimisha batili ya kuwa yeye siye mwenye haki ya kuabudiwa; kwani kilichomuweka kitakuwa ndiye Mungu wa haki.
 2. Ima Allah mtukufu atakuwa ni mwenye kuzitangulia sifa zake, na hili litalazimisha kuwa Allah aliwekuwepo hali ya kuwa sifa hazikuepo, kwa hiyo itakuwa Allah mtukufu alikuwa bila ya kusifika kwa sifa yoyote, na hilo litalazimisha batili zifuatazo:-
  1. Batili ya kuwa Allah mtukufu alikua ni mpungufu; kwani itakua kusifika kwake ni ukamilimu uliopatkana baadae, na ulazima wa kutosifika ni upungufu.
  2. Batili ya kuwa Allah mtukufu atakua ni mwenye kuhitajia sifa, na sifa hazina haja na yeye, kwa maana hiyo sifa zitakua na haki ya uungu zaidi kuliko dhati yake Allah mtukufu.
  3. Batili ya kuwa sifa zake ni viumbe; kwa sababu hazikuepo na zimehitajia wa kuziweka, na katika hili pia kuna batili nyengine, nayo ni nani aliyeziumba hizo sifa? Kwani Allah ikiwa hasifiki vipi ataweza kuumba?
 3. Batili ya kupatikana vitu vingi vyenye sifa ya kutokua na mwanzo([1]). na hili litalazimisha batili zifuatazo:-
  1. Batili ya kushirikiana Allah na Vitu vyengine katika Utangu wake, na hili ni batili kwa sababu litasababisha Itikadi ya kuvunjika upweke wake Allah mtukufu.
  2. Batili ya kuwa Allah atakuwa ni mwenye kuhitajia sifa, na sifa hizo hazina haja na yeye. Batili hii inasababisha Itikadi ya kuwa sifa zina haki zaidi ya uungu kuliko Allah mwenyewe, na kuwa Allah ni mwenye kuhitajia sifa kama viumbe, na hili lina batili ya kumfananisha Allah na viumbe vyake.
 4. Batili ya kuwa Allah ni sehemu ya kukaliwa na vitu vyengine; kwa sababu yeye ndiye mwenye kusifika, na sifa ni vitu vyengine visivyokua yeye, na hili litalazimisha batili ya:-
  1. Kupangika Allah mtukufu.
  2. Kutoka katika hali ya upungufu na kuingia katika hali ya ukamilifu.
  3. Kufanana Allah na viumbe vyake, ametakasika Allah mtukufu na mapungufu hayo. 
 5. Batili ya ulazima wa kuwa Allah mtukufu ni mwenye kuvihitaji vitu hivo, na jambo hilo ni miongoni mwa sifa za viumbe; kwani ndivo vyenye kuhitajia sifa kama tulivo sisi wanadamu, basi haiwezekani kwake yeye Allah mtukufu kuwa hivyo.

Kutokana na hayo ya kubatilika batili hizo tulizozieleza -ambazo sababu yake ni kuitakidi kuwa sifa za Allah mtukufu sio Dhati yake Allah mtukufu- ndio ikalazimika kuitakidi kuwa sifa za dhati ya Muumba (Allah mtukufu) sio vitu vyengine visivyokuwa yeye mwenyewe Allah mtukufu, na kwa maana hiyo sifa zake za dhati ndiyo dhati yenyewe; kwani makusudio hasa ya sifa hizo sio hayo matamko yake, bali ni kusifiwa dhati yake kwa mujibu wa kuulezea ukamilifu wake Allah mtukufu kidhati, basi ukamilifu ndio unaojulishwa kwa maana za sifa hizo.

Kwa hakika:

 1. Allah ni mwenye kuwepo kwa dhati yake.
 2. Allah ni mwenye kujua kwa dhati yake.
 3. Allah ni mwenye kubakia kwa dhati yake.
 4. Allah ni mwenye kuona kwa dhati yake.
 5. Allah ni mwenye kusikia kwa dhati yake.
 6. Allah ni mwenye kutaka kwa dhati yake.
 7. Allah ni mwenye kuweza kwa dhati yake.
 8. Allah ni hai kwa dhati yake.
 9. Allah ni mkwasi (asiyehitaji) kwa dhati yake.

Yote hayo sio kwa kitu chengine kisichokua yeye mwenyewe, wala sio kwa kitu kilichoongezeka katika dhati yake, au kuwa Allah mtukufu yupo kwa kutegemea hizo sifa.

Kwa hakika sifa hizo ni maana za kuzingatia([2]) na kuuelezea ukamilifu wake Allah mtukufu, kwani sifa hizo ni maana za kuielezea dhati yake Allah mtukufu.

Basi imebatilika Itikadi ya wanaoitakidi kuwa sifa hizo ni sifa zilizojitegemea anazozitumilia Allah mtukufu, basi sifa za namna hiyo hazipo katika uhakika wake, wala katika dhati yake Allah aliyetukuka, ametakasika Allah mtukufu na kufanana na viumbe vyake.

Tujue kuwa makusudio ya kusifika Allah mtukufu kwa sifa hizo, ni kuwa sisi waja tuzingatie maana zake kwa kuujua ukamilifu wa Allah mtukufu, basi inalazimika kwetu kukataa na kupinga yale yote yaliyokua ni kinyume na maana za sifa hizo tukufu, basi Allah ametakasika na kila pungufu kwani yeye peke yake ndiye aliye mkamilifu kidhati.

Basi tujue kuwa inakusudiwa:

 1. Kusifiwa Allah kwa sifa ya uhai kukataa sifa ya umauti kwa yeye.
 2. Kusifiwa Allah kwa sifa ya elimu kukataa sifa ya ujinga kwake yeye.
 3. Kusifiwa Allah kwa sifa ya uwezo kukataa sifa ya kushindwa kwake yeye.
 4. Kusifiwa Allah kwa sifa ya kutaka kukataa sifa ya kulazimishwa kwake yeye.
 5. Kusifiwa Allah kwa sifa ya usikivu kukataa sifa ya uziwi kwake yeye.
 6. Kusifiwa Allah kwa sifa ya uoni kukataa sifa ya upofu kwake yeye Allah mtukufu.

Na namna hivi kwa sifa zilizobakia.

Basi Allah mtukufu peke yake ndiye muumba na kila kisichokua yeye hicho ni kiumbe, basi Allah mtukufu ni mwenye kusifika kwani ni mkamilifu kidhati ukamilifu uliojitosholeza, na sio kwa ukamilifu wa kuhitajia sifa.


[1]. Yaani kila sifa miongoni mwa hizo sifa itachukua na sifa ya utangu na kuwa haina mwanzo.

[2]. Yaani kuzingatia ukamilifu wake Allah mtukufu kwa kuzingatia yasiyofichika na yasiyotoka nje ya uwezo wake.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment