Ibadhi.com

4. DALILI YA KUSIFIKA ALLAH KWA SIFA ZA LAZIMA

Na dalili ambazo zitaiwezesha akili kujua ulazima wa kusifika Allah mtukufu kwa sifa hizi za lazima kidhati, na kuwa haiwezekani kwa Allah mtukufu kusifika kwa kinyume cha kusifa kwake kwa sifa hizo ni:-

1.       Sifa ya kuwepo:

 Lau kuwa yeye Allah mtukufu hayupo tokea tangu basi usingelikuwepo uwezekano wa kupatikana ulimwengu, kwa sababu ulimwengu ni kitu cha kuwekwa; basi ni lazima upate yule aliyeuweka.

Na dalili ya kutokeza ulimwengu ni kuwa huu ulimwengu ni maumbile na malazimisho yake, na malazimisho yake ni mambo mapya ya kutokeza; kwa dalili ya kubadilika kwake na kupatikana kwake baada ya kukosekana, na kukosekana kwake baada ya kupatikana.

Na maumbile ni yenye kuhitajia; kwani hayawezi kubakia bila ya malazimisho yake ambayo ni kiumbe chenye kuhitaji wa kukikadiria, na kilichokua kinategemea kitu kipya ambacho ni kiumbe bila shaka nacho kitakua ni kiumbe vile vile.

 

 2.       Sifa ya utangu (wa mwanzo kuwepo):

Lau kuwa Allah mtukufu sio wa tangu, na akawa na mwanzo wa kuanza basi angalikua ni kitendo, na kila kitendo kinahitaji mwenye kukitenda, basi italazimika kuunganika kwa watendaji bila ya kupatikana wa mwanzo, au kuzunguka kwa watendaji baina yao wao kwa wao na kuwa kila mmoja atakua ni mwenye kutegemea mwengine ili apatikane, na haya mawili yote hayawezekani, basi ikalazimika kuwa Allah ndiye wa tangu aliyetakasika na kuwa na mwanzo wa kuanza, na kuwa yeye ni mwenye kusifika kuwa ni wa mwanzo wa kuwepo (Watangu).

3.       Sifa ya kubaki:

Lau kuwa Allah mtukufu hailazimiki kuwa ni mwenye kubaki basi ingaliwezekana kuwa yeye ni mwenye kumalizika na akakosekana kabisa, na hiyo ni sifa ya kuathirika na kuzidiwa, kwa sababu italazimika kuwa ni mwenye kuathiriwa na vyengine, na huo -bila ya shaka- utakua ni upungufu, haiwezekani kwa Muumba wa haki kufikiwa na upungufu huo na wowote ule, basi vipi yawezekane hayo na hali yeye ndie aliyeumba vyote?.

Basi kwa hakika Allah mtukufu ametakasika na uwezekano wa kukosekana, basi imelazimika kuwa Allah mtukufu ni mwenye kubakia bila kufikiwa na uwezekano wa kukosekana tangu na milele.

4.       Sifa ya uhai:

Na lau kuwa Allah mtukufu ni maiti basi asingaliweza kuumba viumbe, wala kuvikadiria, na ulimwengu usingelibakia.

Basi imelazimika kuwa Allah mtukufu ni hai; kwani yeye ndiye aliyeumba viumbe, na yeye ndiye aliyevikadiria, na yeye ndiye mwenye kuviendesha.

5.       Sifa ya elimu:

Na lau Allah mtukufu angalikua ni mwenye kupitiwa na hali ya ujinga basi asingaliweza kujua vipi aviweke viumbe; angalikua ni mwenye kuhitaji mwengine.

Basi imelazimika kuwa Allah mtukufu ni mwenye kujua mwenye kutakasika na kiwango chochote cha ujinga.

6.       Sifa ya uwezo:

Na lau Allah mtukufu angalikuwa hana uwezo, na akawa ni mwenye namna ya kushindwa; basi asingaliweza kuviweka viumbe, wala asingeweza kuziendesha, wala asingezewa kupitisha makadirio yake.

Basi imelazimika kuwa Allah mtukufu ni muweza aliyetakasika na uwezekano wa kushindwa.

7.       Sifa ya kutaka:

Na lau Allah mtukufu angalikua si mwenye kutaka basi asingaliweza kuweka viumbe, na ngalikua yeye ni mwenye kulazimishwa kuweka viumbe, tena angalikua ni mwenye kushindwa.

8.       Sifa ya kuona na kusikia:

Na lau Allah mtukufu angalikua ni kipofu au kiziwi basi angalikua na upungufu wa kufichika kwake vya kuonekana na kusikikana, na hilo haliwezekani.

9.       Sifa ya kutofautiana na viumbe:

Na lau angalikua ni mwenye kufanana na viumbe basi angalikua na yeye ni kiumbe, na umeshajua kuwa haliwezekani jambo hilo.

10. Sifa ya kujitosheleza:

Na lau angalihitaji kitu chengine ili awe ni wenye kupatikana kwa sababu ya kitu hicho, au kitu hicho kiwe ni chenye kumuweka yeye, au afanye kwa kutegemea kitu hicho, basi angalikua ni sifa ya kitu chengine, au hicho kitu chengine kingalikua ndio kilichomuweka yeye, au ndicho kilichomsaidia, na hayo yote ni ufungufu hayawezekani kwa Allah.

Wala haikubaliki kuwa yeye ni sifa, kwani yeye amesifika kwa sifa, na sifa hazisifiki kwa sifa, wala haikubaliki kuwa yeye ni mwenye kuwekwa, kwani itakua haiwezekani kupatikana kwake baada ya kukosekana, wala kuwa yeye ni mwenye kujisaidia kwa kitu chengine, kwa sababu jambo hilo litalazimisha kuwa yeye ni mwenye kushindwa, na hilo haliwezekani.

11. Sifa ya upweke:

Lau angalikua sio mmoja katika dhati yake, sifa zake, na vitendo vyake, basi angalikua ni mwenye uwingi, au atakua ni mwenye kufanana na kitu chengine katika dhati au sifa au kitendo, na kwa sababu hiyo isingeliwezekana kupatikana ulimwengu huu:

﴿ لَوْ كَانَ فِيهِمَا الِهَةٌ إِلاَّ ٱللَّهُ لَفَسَدَتَا

Lau kuwa ndani yake (Mbingu na Ardhi) kuna waungu asiyekua Allah kwa hakika zingaliharibika﴿

[Anbiyaa: 22]

Kwa sababu; lau wangalikubaliana hao waungu katika kuuweka ulimwengu, basi ingalilazimika moja katika mawili:-

1.    Walio wengi kati yao kulikubali jambo aliloamua mmoja katika wao, na hilo haliwezekani, na hili ikiwa tutakadiria kuwa uamuzi wao utapita, nalo pia haliwezekani([1]).

2.    Na lau kuwa watatofautiana, itakua kufanyika amuzi la mmoja wao ni kusababisha kushindwa kwa waungu wengine, na kwa sababu wao pia ni mfano wake katika sifa ya uungu, itakua na huyo aliyoweza kupitisha amuzi lake ni mwenye sifa ya kushindwa kama hao wengine, basi itakua haiwezekani kuwepo sifa ya uungu kwake yeye pia, na hilo lingekua ni lazima kwa hao wengine vile vile, na hapo ungalibatilika uungu.

Na kwa sababu hiyo ndio ikalazimika kuwa yeye Allah ndie Mungu mmoja tu, yeye ndie Mungu wa haki asiyekua na Mshirika.

12. Sifa ya kutofanana yeye na kitu chochote:

Kwa sababu haiwezekani kusifika Allah mtukufu kwa hayo tuliyoeleza katika sifa za Muumba wetu; basi ikalazimika kuitakidi kuwa haiwezekani Allah mtukufu awe ni mwenye kusifika kwa chochote katika sifa za viumbe, kama vile: kuwa na rangi, kusimama, kukaa kitako, kupanda juu, kushuka chini, kulala, kuamka, kusahau, kughafilika, na mfano wa sifa hizo.

Na wala haiwezekani kwake yeye Allah mtukufu kusifika kwa chochote miongoni kwa sifa za viungo, kama vile kuwa na uso, jicho, pua, sikio, mkono, mguu, na mfano wake.

Na pia haiwezekani kuwa yeye amejihusisha na sehemu miongoni mwa sehemu, au muelekeo wa upande fulani, au wakati fulani, au ukaribu na umbali wa masafa([2]).[1]. Yote hayawezekani kwa sababu kutalazimisha kutegemea wengine katika kupita amuzi  la yoyote katika wao, na sifa ya kutegemea haiwezekani katika haki ya Mungu kwa sababu inalazimisha kushindwa na kuhitaji, na haya mawili ni upungufu.

[2]. Fahamu kuwa kusikia na kuona kwa waja kunapatikana kwa njia ya kuhitaji na kutegemea vitu vyengine kama mawimbi ya sauti, hewa, rangi, sikio, jicho, n.k, ama tunapomsifu Allah mtukufu kwa sifa hizo na mfano wake inakua kwa njia ya kuzingatia kuwa hakuna kinachofichika kwa Allah mtukufu, basi ikiwa ni sauti -iwe sauti yoyote itakayokua- kwa hakika sauti hiyo iko wazi kwa Allah mtukufu, na hapa tunazingatia sifa ya usikivu, na ikiwa ni vya kuonekana, basi vyote vya kuonekana viko wazi kwa Allah mtukufu, na hapa tutazingatia sifa ya kuona, na namna hivi, kwani Allah mtukufu hana sifa ya kuhitaji na kutegemea yeye ni mkamilifu asiyekua na upungufu, amesema Allah mtukufu:

﴿إِنَّ اللّهَ لاَ يَخْفَىَ عَلَيْهِ شَيْءٌ فِي الأَرْضِ وَلاَ فِي السَّمَاء﴾

Kwa hakika Allah hakifichiki kwake yeye chochote katika Ardhi wala katika mbingu﴿ [Ala imraan 5].

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment