Ibadhi.com

1. KUMJUA ALLAH MTUKUFU

Bila shaka kila mwenye akili anafahamu ulazima wa kuwa kila kitendo kinahitajia mtendaji wake, na kila mwenye akili anajuwa kuwa huu ulimwengu ni vitu vilivyotendwa na nidhamu iliyopangwa, basi dalili kubwa ya kumjuwa Muumba wa haki ni kumjuwa yeye na kumthibitisha kwa dalili ya vitendo vyake alivyofanya ambavyo ni viumbe vyake na nidhamu aliyoijaalia katika mamlaka ya viumbe vyake.

Mtume Mussa na Mtume Haroun (a.s.w) walipomfikia Firauni Mdaiuungu (l.a), basi Firauni (l.a) alimuuliza Mtume Mussa (a.s.w): ((Hivi ni nani Mola wenu ewe Mussa?)) [Taha 49] hapo Mtume Mussa (a.s) akajibu na ((Akasema: Mola wetu ni yule aliyakipa kila kitu umbile lake kisha akaongoza)) [Taha 50].

Na Mtume Ibrahim (a.s.w) alimwelekea Mola wake kwa kusema ((Hakika mimi naelekeza dhati yangu kwa yule aliyeumba mbingu na ardhi hali ya kuacha mila zote na mimi si katika washirikina)) [Anaam 79]

Basi Allah mtukufu ndiye huyo Mola aliyeumba viumbe vyote, Allah mtukufu ndiye Muuambaji, na vyengine vyote (kila kisichokua Allah) ni viumbe.

Allah anasifika kidhati, basi Allah mtukufu ni mkamilifu asiyefikiwa na namna yoyote ya upungufu.

Allah mtukufu peke yake ndiye muabudiwa wa haki, basi Allah mtukufu ndiye Mungu wa kweli na wa haki, basi vyengine vinavyoabudiwa -pasina Allah mtukufu- vyote hivo ni miungu batili na ibada za wanaoviabudu ni batili.

Allah mtukufu peke yake ndiye Mungu mmoja tu wa haki asiyekuwa na mshirika.

Allah mtukufu ni mmoja tu, hana mshirika katika dhati yake.

Allah mtukufu ni mmoja tu, hana mshirika katika kusifika kwake.

Allah mtukufu ni mmoja tu, hana mshirika katika vitendo vyake.

Allah mtukufu ni mmoja tu, hana mshirika katika ibada za waja wake.

Tunamjua Allah mtukufu kuwa yeye ndie aliyeumba kila kitu, kuwepo kwa Allah mtukufu ni kabla ya kuwepo kila kisichokuwa yeye, basi Allah mtukufu ndiye wa Mwanzo bila ya kuanza, yeye ndiye aliyeumba sehemu na wakati, na kiza na nuru, na uhai na kifo, na mbingu na ardhi, na wanyama na miti, na maji na hewa, na kila tunachokijuwa na tusichokijuwa.

 Allah mtukufu ni Mkwasi (Hafikiwi na hali ya kuhitajia), basi Allaah mtukufu ni Mkamilifu wa Dhati.

Allah mtukufu hawezekani kwake kusifika kwa sifa yoyote ile ya kiumbe chochote; kwani sifa zote za viumbe zinahitajia viumbe, na kusifika viumbe kwa sifa hizo ni kwa njia ya kuzihitaji sifa hizo, na viumbe na sifa zao vyote ni viumbe vya Allah mtukufu vimo katika uhakika wa kumuhitajia Muuumbaji wake ambaye ni Allah mtukufu.

BASI NI WAJIBU KUMSIFU ALLAH MTUKUFU KWA KUUELEZEA UKAMILIFU NA UTUKUFU WAKE WA KIDHATI, NI WAJIBU KUMTAKASA ALLAH MTUKUFU KWA KUPINGA NA KUKATAA YOTE YASIYOKUBALIANA NA UKAMILIFU NA UTUKUFU WAKE WA KIDHATI.

 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment