Ibadhi.com

15. SIMULIZI ZA HADITHI KUTOKA KWA IBN ABBAS (R.A.A.).

15.1 KATIKA KUMTUKUZA MOLA NA KUMUONDOSHEA UPUNGUFU: IBN ABBAS (R.A.A) NA NAJDATU AL-HARUURIYY.

839. Abu Qubaysa katuambia kutoka kwa Umayri, kutoka kwa Muhammad bin Ya`aly, kutoka kwa Juwaybir, kutoka kwa Dhihaak, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kwamba, "Najdata L-Haruuriyy alimjia akasema, "Ewe Ibn Abbas! Vipi utambuzi[1] wako kwa Mola wako? Kwani waliokuwa kabla yetu wamekhitilafiana na sisi”. Ibn Abbas (R.A.A.) akasema, "Ninamtambua kama Alivyojijulisha Mwenyewe bila kuonekana, na nitamwasifia[2] kama Alivyojiwasifia Mwenyewe bila uthibitisho wa sura. Hafikiliwi kwa hisia, wala halinganishwi kwa kipimo pamoja na watu, Anajulikana kwa watu bila ya kumshabihisha. Yu karibu pamoja na umbali wake, Haangaliwi wala kufikiriwa muda wa kudumu Kwake, wala halinganishwi na viumbe Vyake, wala Hadhulumu katika hukumu zake, viumbe wanaongozwa na yale ayajuayo, na wanafanya yale aliyo yahukumu katika kitabu chake (tokea azal[3]), wala hawatarudi kwa mwenginewe asiyekuwa Yeye, Naye yu karibu hakugandana (na viumbe), yuko mbali hakutengana na (viumbe), anathibitishwa (kuwepo kwake) wala hafananishwi, anawahidishwa[4] wala hafanywi zaidi ya mmoja, anajulikana kwa dalili na huthibitishwa kwa alama. Akasema, "Najdata akasimama kabobea hana la kusema ameshangaa kwa maneno aliyoyasikia kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.)”

 

15.2  KISA CHA NAAFI`I BIN L-ARZAQ PAMOJA NA IBN ABBAS (R.A.A.).

840. A-Rrabi`i kasema, "Na ametuambia Muhammad bin `Ali L-Kuufiy, kutoka kwa Abi Bakar    L-Hudhaliy, kutoka kwa Sa`id bin Jubair (R.A.A.) kasema, "Ibn L-Azraq alipoona kwamba Ibn Abbas (R.A.A.) haulizwi chochote isipokuwa Ibn Abbas (R.A.A) hujibu akasema, "Ni mtu uliye shujaa unajibu bila khofu ewe Ibn Abbas!” Akajibu akasema, "Ni kitu gani hicho ewe Ibn L-Azraq?” Akasema, "Nakuona huulizwi kuhusu chochote ila unajibu”. Akasema, "Ole wako! Hiyo ni elimu niliyonayo. Niambie mtu anayeficha elimu aliyokuwa nayo, na mtu anaesema bila ya kujua”. Akasema, "Jee, yote unayoyasema unayajua?” Akasema, "Naam, sisi watu wa nyumba tumepewa hekima”. Nafi`i akasema, "Nakuuliza kuhusu ambaye unaemuabudu yupo vipi?” Ibn Abbas (R.A.A.) akamnyamazia kimya, kuadhimisha aliyosema. Kisha akamwambia, “Nakuarifu ya kwamba Allah ni Mmoja bila kushabihiwa, na yupo bila ya kufikiri, na Muumbaji bila ya namna, na Mjuzi bila ya kifani, Mwenye sifa njema bila ya kumfananisha, wa Milele hana mwisho, Maarufu bila kiwango, Mwenye kubainisha bila ya kuwa na mwenziwe wa sura moja wa kumsaidia, Mwenye enzi, Muweza, Yungali yupo tangu awali isiyokuwa na mwanzo, na atabakia bila ya kuwa na mwisho, Nyoyo zimejaa khofu kwa utukufu Wake, wamedhalilika wakuu (wafalme) wote kutokana na utukufu Wake, shingo zimejitupa Kwake kwa sababu ya uwezo Wake, nyoyo hazijafikiria kukadiria utukufu Wake, wala nyoyo hazifungi dhamiri kumfikia, Wataalamu hawamfikii kwa akili zao, wala wale wanaofikiri kuzingatia kwa njia ya fikira. Mjuzi zaidi katika viumbe (katika kumjua Allah) ni yule ambaye Hamsifii, wala Hamfananishi kwa mfano ambao utawapeleka viumbe wengine wachanganyikiwe juu yake (katika kumjua). Naafi`i akasema, "Umesema kweli ewe Ibn Abbas!”

 

841. Mtume (S.A.W.) kasema, "

«اللَّهُمَّ فَقِّهِ ابْنَ عَبَّاسٍ فِي الدِّينِ وَعَلِّمْهُ التَّأْوِيلَ».

 Maana yake, “Ewe Allah! Muelimishe dini Ibn Abbas na umfundishe tafsiri”.

 

842. Jaabir kasema, "Naafi`i bin L-Azraq alikuja kwa Ibn Abbas (R.A.A.) akasema, "Ewe Ibn Abbas! Nielezee kuhusu Mola wako yupo vipi na yupo wapi?” Ibn Abbas akamjibu akasema, "Unashangaza ewe Ibn L-Azraq! Allah haulizwi kwa kutumia vipi? ila viumbe peke yao[5]. Ameumba viumbe Naye, ni Muumbaji kwa namna zao, Naye yupo kila sehemu”. Kasema, "Akanyamaza kimya Ibn L-Azraq”. Ibn Abbas (R.A.A.) akasema, "Hayatapita masiku na siku hata watu wakaelimika na elimu ya sheria. Nao kwa kumpwekesha Allah wameghafilika. Watu wanaomuwasifia Mola wao kwa umbile la kibinadamu, na kuwaita wale waliokwenda kinyume na hayo kuwa ni makafiri. Nao ndio wanastahiki zaidi kuitwa makafiri, lakini wao ni madhalimu, wanatofautiana baada ya kuwajia ubainisho. Na wanachukulia dalili za mutashabihati, na za kuleta mifano, na simulizi za watu waliopewa Kitabu na kumwita ni wanachuoni, nao si hivyo. Na wakati huo mbingu zinazuia matone ya mvua, na ardhi kutokutoa mimea, na kupungua nchani mwake, na hapo ndipo Allah anaharibu vitendo vyao, na kuwapa nguvu watu ambao wanawaadhibu kwa adhabu mbaya ” 

 

843. Jaabir bin Zayd kasema, "Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Allah anasema, “Mimi ni Mola wenu, msimuabudu mwingine, wala Msinishirikishe na mwingine, wala Msinishabihishe[6] mbinguni na katika ardhi. Kwa hakika nyinyi hamtaniona”.

 

15.3  KAULI INAYOSEMA: MOLA KAMUUMBA ADAM KWA SURA YAKE.

844. Kasema na katwambia Bishru L-Muraisy, kutoka kwa Muhammad bin Ya`ala kasema, "Hasan bin Diynaar alituambia, kutoka kwa Khusaib bin Jahdar, kutoka kwa Is-haaq bin Abdallah kwamba L-Haarith bin Naufal kasema, "Nilimwambia Ibn Abbas (R.A.A.), "Nimemsikia Abu Hurayrah (R.A.A.) akisema, “Allah amemuumba (Nabii) Adam kwa sura Yake, naye ni dhiraa 60. Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Kasema kweli Abu Hurayrah (R.A.A). Mola amemuumba (Nabii) Adam kwa sura Yake ambayo anaijua Mwenyewe kwamba atamuumbia kutokana nayo, hataibadili kwa nyingine. Bishru kasema, "Na maana nyingine. Mola amemuumba (Nabii) Adam kwa sura Yake aliyokuwa akiifahamu Yeye atamuumbia kutokana nayo. Nakuarifu kwamba haikunukuliwa tone la uzazi kuwa damu iliyoganda, wala damu kuwa pande la nyama, na wala pande la nyama kuwa mifupa. Na maana nyingine, “Alikuwepo wala hakuna kitu kilichokuwa nae pamoja, Mola alikuwa akijua sura Anayoiumba, na ardhi, na roho na Mitume. Na Allah akamchagua (Nabii) Adam kwa sura Yake yaani sura aliyoichagua inajulikana, na akachukua ardhi takatifu akaifanya ni pahala pa ibada kwa kwaja Wake, Akaifanya ndani yake nyumba Yake wanayoiabudia waja Wake, kwa kuizunguka na kuhijia. Na inasemekana, “Nyumba ya Allah aliyoichagua, na kuichagua roho moja katika roho nyingi. Na ikasemwa, “Roho ya Mola kwa ajili ya yule aliyemchagua”. 

 

845.A-Rrabi`i kasema, "Abu Ubayda kasema, "Nimearifiwa na Sa`id bin Jubair (R.A.A.) kasema, "Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Hakika itakuja zama kabla ya kiama, (itakuwa) wanavyuoni wao ni wale wajinga. Viongozi wao wanajivuna. Na wasomaji wao ni wenye kujitia ujuzi wa kupunguza na kuzidisha. Na wakati huo Shetani ataweka mitego yake, watakapomfikiri Muumbaji watamshabihisha na waumbwaji. Wanaleta Hadithi wanazitaja kwamba zinatokana na Mtume (S.A.W.) na kumwekea Mola mipaka. Na wanamsifia kwa sifa za viumbe. Mtakapoona fitina hii wala hakuna fitina nyingine yenye madhara kuliko hii, basi jilindeni kwa Qur-ani. Kwani ina mwangaza kutokana na giza, na mabainisho kutokana na shubuha, na wokovu kutokana na kila angamizo. Na ina uongozi kutokana na upotofu”.

 

846. Kasema, "Nimepata khabari kutoka kwa Kulabiyyu, kutoka kwa Abiy Saleh, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.) kasema, "Mtume (S.A.W.) kasema, "

«تَفَكَّرُوا فِي الْخَلْقِ وَلاَ تَتَفَكَّرُوا فِي الْخَالِقِ، فَإِنَّ فِتْنَةَ كُلِّ أُمَّةٍ بَعْدَ نَبيِّهَا تَفْكِيرُهَا فِي الْخَلْقِ، وَكَذَلِكَ فِتْنَةُ أُمَّتِي بَعْدِي».

Maana yake, “Fikirieni viumbe wala msimfikirie Muumbaji. Kwa hakika fitina ya kila umma baada ya Mtume wao ni kumfikiria Muumbaji. Na ndivyo hivyo fitina kwa umma wangu baada yangu”.[1] Yaani unamfahamu vipi?.

[2] Kumuelezea, kumfananisha.

[3] Toka milele.

[4] Yuko Pekee hana mshirika.

[5] Yaani masuala kama hayo wanauliziwa viumbe wake tu.

[6] Msinifananishe.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment