Ibadhi.com

14. SIMULIZI ZA HADITHI KUTOKA KWA ALI BIN ABI TAALIB (K.W).

 

14.1 KATIKA KUMUADHIMISHA MOLA MTUKUFU NA KUONDOSHA MSHABAHA NA VITU.

835. A-Rrabi`i kasema, "Nimearifiwa kutoka kwa Ibn Mas`uud bin `Uthmaan bin `Abdul-Rrahmaan Al-Madaniy, kutoka kwa Abi Is-haaq na Sha`abiy kasema, "Ali Ibn Abi Taalib alikuwa akisema katika kumtukuza Allah Mtukufu, "

الْحَيُّ الْقَائِمُ الْوَاحِدُ الدَّائِمُ، فَكَّاكُ الْمَقَادِمِ، وَرَزَّاقُ الْبَهَائِمِ، الْقَائِمُ بِغَيْرِ مَنْصَبَةٍ، الدَّائِمُ بِغَيْرِ غَايَةٍ، الْخَالِقُ بِغَيْرِ كُلْفَةٍ. فَأَعْرَفُ الْعِبَادِ بِهِ الذِي بِالْحُدُودِ لاَ يَصِفُهُ، وَلاَ بِمَا يُوجَدُ فِي الْخَلْقِ يَتَوَهَّمُهُ، {لاَّ تُدْرِكُهُ الاَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الاَبْصَارَ}.[1]

Maana yake, “Hai wa Milele, Msimamizi wa mambo yote, Mpweke wa daima, Mfunguzi wa mambo Yake, na Mwenye kuruzuku wanyama, Mwenye kusimama bila ya jukwaa. Wa Milele bila mwisho, Muumbaji bila kulazimishwa, amjuae zaidi katika waja ni yule asiyemsifia Allah katika mipaka, wala hayamdanganyi yaliomo katika (sifa) viumbe (ili amsifie Allah kwa sifa hizo). [Macho hayamfikilii bali Yeye anayafikilia macho]”.

 

 

14.2 . HOTUBA YA ALI (R.A.A)

836. A-Rrabi`i kasema, "Na Abaan ametuambia, “Katuhadithia Yahya bin Ismail, kutoka kwa Al-Haarithi L-Hamdaani kasema, "Aliarifiwa Ali kwamba kundi moja la watu kutoka kambini mwake lilimshabihisha Mola, na kupindukia mpaka, akasema, "Akawahutubia watu, akamshukuru na kumsifu Allah kisha akasema, "Enyi watu! Jihadharini na upotofu huu”. Wakajibu wakasema, "Ewe Kiongozi wa Waislamu,! Ni nani yule aliyeropoka?” Akasema, "Wale ambao wanamshabihisha Mola kwa nafsi zao”. Wakasema, "Na vipi wanavyomshabihisha Allah kwa nafsi zao?” Akasema, "Wanayaiga maneno ya waliokufuru katika watu waliopewa Kitabu (Wayahudi na Manasara) waliposema: “Allah kamwumba (Nabii) Adam kwa sura Yake. Mola Ametakasika na hayo wanayoyasema, na hayo wanayomshirikisha nayo. Bali Yeye ni Allah Mmoja, Ambaye hapana kitu chenye mfano Wake. Amejihukumia pekee upweke nguvu zote. Amepitisha kutaka, na uwezo, na ujuzi katika yaliopo, hana mpinzani kwa kitu chochote, wala hakuna aliyefanana Nae, na wala anayeweza kuwa sawa Naye, wala aliyekinyume Naye, na wala anayeweza kupingana Naye, wala jina lilofanana Naye, au kupitiwa na matokeo mapya ya mambo asiyajue, wala hapitikiwi na mabadiliko ya hali, wala hayamteremki mambo mapya (asiyoyajua), bali Yeye huyapitisha, na kuyateremsha matokeo kwa viumbe, hawajafikia wamsifiao uhakika wa sifa Zake, wala nyoyo (za watu) hazijavifikiria nguvu Zake, kwa sababu hashabihiani na viumbe wala vitu. Hawamfikilii Wataalamu, wala watu wenye kufikiri, kuyazingatia au kuyawaza, isipokuwa kuhakiki kwa kuamini kwa yasiyo kuweko, kwa kuwa Allah hasifiwi kwa sifa wanazosifiwa nazo viumbe. Naye ni Mmoja hapana aliye sawa Naye”.

}وَأَنَّ مَا يَدْعُونَ مِن دُونِهِ هُوَ ٱلْبَاطِلُ وَأَنَّ ٱللَّهَ هُوَ ٱلْعَلِيُّ ٱلْكَبِيرُ {[2]

Maana yake, "{Na kwamba wale wanaowaomba badala Yake, ni baatili, na hakika Allah Ndiye Aliye juu, na Ndiye Mkubwa}.

 

14.3 KISA CHA YAHUDI NA ALI BIN TAALIB.

 Kasema, "Alituelezea Ismaili bin Yahya kasema, "Alituhadithia Sufyaan, kutoka kwa Adh-dhahaak (kwamba), "Alikwenda Yahudi mmoja kwa Ali bin Abi Talib akasema, "Ewe Ali, Mola wenu alikuwa toka lini?” Akasema Ali, “Inasemwa lini kwa kitu ambacho hakikuwepo (kabla) baadae kikawepo,  Yeye yupo bila ya kuwa wapi, wala vipi, Yeye hana kabla, na wala mwanzo, Yeye ni wa kabla bila kikomo, na wa mwisho bila kuwepo mwisho, Kwake ndio umeishia mwisho. (Hana mwanzo wala mwisho).

 

14.4  KISA CHA MUUZA NYAMA NA ALI BIN ABI TAALIB ((R.A.A)).

838. Ametupa khabari Abu Qubaysa, katuambia kutoka kwa Abdul-Ghaffaar L-Waasitiyyi, kutoka kwa `Atwaa kwamba, "Ali bin Abi Taalib alipita kwa muuza nyama akamsikia akisema, “Naapa kwa Yule Ambaye kaziziba mbingu saba sikuzidishii kitu”. Akasema, "Ali akampiga kwa mkono wake kwenye bega lake akasema, "Ewe muuza nyama! Allah hajifichi asionekane na viumbe Vyake, bali watu ndio walioziziba wasionekane Naye. (Muuza nyama) akasema, "Jee, nilipe kafara kwa kiapo changu?” Akamjibu: “La, kwani wewe umeapa kwa asiyekuwa Allah?”.[1] Surat Al An-A`am aya ya 103.

[2] Surat Al-Hajj aya ya 62.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment