Ibadhi.com

11. YANAYOMPASA KUFANYA MWENYE HEDHI KATIKA HAJI.


438. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid, kutoka kwa (Bibi) Aisha mama wa Waislamu (R.A.A.H.) kasema, "Tulitoka sisi pamoja na Mtume (S.A.W.) katika Hijja ya widaa, tukahirimia kwa ajili ya Umra. Kisha Mtume (S.A.W.) akasema, "

«مَنْ كَانَ مَعَهُ هَدْيٌ فَلْيُهِلَّ بِالْحَجِّ مَعَ الْعُمْرَةِ، ثُمَّ لاَ يُحِلُّ حَتَّى يُتِمَّهُمَا جَمِيعًا».

Maana yake, “Atakaekuwa na mnyama (wa kuchinja) ahirimie kwa ajili ya Hijja na Umra, kisha asitoke katika ihram yake (asitahallal) mpaka atimize zote mbili kwa pamoja”.

(Bibi) Aisha (R.A.A.H.) akasema, "Nikafika Makka nami nimo katika hali ya hedhi, hivyo sikutufu L-Ka`aba, na wala sikuenda baina ya Safaa na Marwaa, nikashtakia haya kwa Mtume (S.A.W.) akajibu akasema, "  

«انْقُضِي رَأْسَكِ وَامْتَشِطِي وَأَهِلِّي بِالْحَجِّ وَدَعِي الْعُمْرَةَ»

Maana yake, “Zichambue nywele za kichwani mwako, na uzichane, na hirimia kwa ajili ya Hijja na iwache Umra”. (Bibi) Aisha ((R.A.A.H.) akasema, "Nikafanya niliyoambiwa (na Mtume (S.A.W.), na baada ya kumaliza Hijja akanituma Mtume (S.A.W.) pamoja na Abdu Rrahmaan bin Abi Bakar mpaka tukafika pahala panapoitwa Tan`iym nikahirimia kwa Umra”. Akasema Mtume (S.A.W.), “Hapa ndipo pahala pa kuhirimia Umra yako”. (Bibi) Aisha (R.A.A.H.) akasema, "Wakafanya tawafu wale waliojistarehesha (tamattu’u) kwa ajili ya `Umrah, na kuizunguka L-Ka`aba, na kwenda baina ya Safaa na Marwaa, halafu wakatoka katika Ihraam zao. Halafu wakafanya tawafu nyingine baada ya kurejea kwao kutoka Mina kwa ajili ya Hijja yao, ama wale waliohirimia kwa ajili ya Hajji, au Hajji pamoja na Umrah walitufu (walizunguka) tawafu moja tu”. 

 

439. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid, kutoka kwa (Bibi) Aisha mama wa Waislamu (R.A.A.H.) kasema, "Nilimwambia Mtume (S.A.W.) kwamba Safia bint Huyayyi amepata hedhi”. Mtume (S.A.W.) akamwambia, "

«لَعَلَّهَا حَابِسَتُنَا، أَلَمْ تَكُنْ قَدْ طَافَتْ مَعَكُنَّ بِالْبَيْتِ»

Maana yake, “Anaweza akatuzuia (kwa ajili ya kumsubiria mpaka afanye tawaf ifadha), (akauliza) jee yeye hakutufu pamoja na nyinyi (tawaf ifadha)?” Nikasema, "Ndiyo (yaani katufu na sisi tawaf ifadha),” Akasema, "

«فَاخْرُجْنَ».

Maana yake, “Ondokeni mwende zenu (kutoka Mina muelekee Madina, yaani siyo kwake wajibu kutufu tawaf widaa kufuatatna na hali yake)”.

 

440. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid, kutoka kwa (Bibi) Aisha mama wa Waislamu (R.A.A.H.) kasema, "Nilikwenda Makka nami nina hedhi, sikuizunguka L-Ka`aba, wala sikuenda baina ya Safaa na Marwaa. Nikashtakia haya matatizo kwa Mtume (S.A.W.) akasema, "

«اِفْعَلِي مَا يَفْعَلُ الْحَاجُّ غَيْرَ أَنَّكِ لاَ تَطُوفِي بِالْبَيْتِ حَتَّى تَطْهُرِي».

Maana yake, “Fanya kama afanyavyo anayehiji isipokuwa usitufu (usizunguke) L-Ka`aba mpaka utoharike”.

 

441. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid, kutoka kwa (Bibi) Aisha (R.A.A.H.) kasema, "Safia bint Huyayyi mke wa Mtume (S.A.W.) alipatwa na hedhi akamtajia hayo Mtume (S.A.W.), akamjibu akasema, "

«أَحَابِسَتُنَا هِيَ»؟

Maana yake, “Atatuziwia yeye” Akaambiwa amefanya “Tawafu Ifadha”. Akajibu akasema, "

«فَلاَ إِذَنْ».

Maana yake, “Kwa hivyo hakuna cha kutuzuia”.

 

442. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid, kutoka kwa (Bibi) Aisha mama wa Waislamu (R.A.A.H.) kasema, "Asmaa bint Umaysi alimzaa Muhammad bin Abi Bakar pahala panaitwa Albaydaa[1], Abu Bakar (R.A.A.) akamtajia hayo Mtume (S.A.W.) akamjibu akasema, "

«مُرْهَا فَلْتَغْتَسِلْ ثُمَّ لِتُهَلِّلْ».

Maana yake, “Mwamrishe akoge halafu ahirimie”.[1] Ni sehemu iliyo karibu na Dhulhulayfa.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment