Ibadhi.com

6. YANAYOHUSU AL-KA`ABA, NA MASJID AL-HARAAM, NA SAFWA NA MARWA.

 

409. Abu Ubayda kasema, "Nimepata khabari kutoka kwa Ibn Umar (R.A.A.) kasema, "Nilimwuliza Bilal (R.A.A.) siku aliyoingia Mtume (S.A.W.) L-Ka`aba alitenda nini na alifanya nini?” Kasema, "Aliiweka nguzo kushotoni kwake, na nguzo mbili kuliani kwake, na nguzo tatu nyuma yake, na L-Ka`aba siku hiyo ilikuwa na nguzo sita.

 

410. Abu Ubayda kasema, "Nimepata khabari kutoka kwa Aisha mama wa Waislamu (R.A.A.H.) kasema, "Mtume (S.A.W.) kasema, "

«أَلَمْ تَرَيْ قَوْمَكِ حِينَ بَنَوُا الْبَيْتَ اقْتَصَرُوا عَلَى قَوَاعِدِ إِبْرَاهِيمَ»؟

Maana yake, “Hukuona kwamba watu wako (Ma-Quraishi) walipokuwa wanaijenga L-Ka`aba walipunguza misingi ya (Nabii) Ibrahim?” Akasema, "Ewe Mjumbe wa Mola! Jee, huzirejeshi kwenye misingi ya Ibrahim?” Akajibu akasema, "

«لَوْلاَ حِدْثَانُ قَوْمِكِ بِالْكُفْرِ».

Maana yake, “Lau kama si watu wako kutoka katika ukafiri karibuni (na kuingia uislamu basi ningalirudisha katika asili yake)”

 

411. Abu Ubayda kasema, "Nimepata khabari kwamba Mtume (S.A.W.) aliingia L-Ka`aba mwaka wa ufunguzi, akasali rakaa mbili ndani yake”.

 

412. Abu Ubayda kasema, "Aliulizwa Ali bin Abi Taalib (R.A.A.) kuhusu kitu gani alichomtuma Mtume wa Mola (S.A.W.) kwa Abu Bakar (R.A.A.) wakati wa Hija ya mwaka wa tisa?” Akajibu akasema, "(Alinituma) Kwa mambo manne: Asitufu (asiizunguke) L-Ka`aba (mtu) alie uchi, wala haiingii Peponi ila nafsi yenye kuamini, baada ya mwaka huu wala wasichanganyike mwislamu, na mshirikina katika L-Haram (kufanya ibada pamoja), na aliyekuwa na ahadi kwa Mtume (S.A.W.) basi aitelekeze ahadi yake, na asiyekuwa na ahadi basi aambatane na miezi minne”.

 

413. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid, kutoka kwa Jaabir bin Abdullah (R.A.A.) kasema, "Nilimwona Mtume wa Mola (S.A.W.) akiliendea haraka jiwe jeusi hadi kufikia ukomo katika mizunguko mitatu. Na anaposimama kwenye Safaa[1] hupiga takbira tatu na husema, “

«لاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ لَهُ الْمُلْكُ وَلَهُ الْحَمْدُ يُحْيِي وَيُمِيتُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْء قَدِيرٌ».

[La ilaaha illa Llaahu wahdahu la shariyka lahu lahu L-Mulku walahu L-Hamdu wahuwa `ala kulli shay-in qadiyr]

Maana yake, “Hapana anaepaswa kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allah peke yake hana Mshirika. Ufalme ni Wake, na Yeye ndie anaepaswa Kushukuriwa, Anaehuisha (kutoa uhai) na Anaefisha. Naye (ni) Muweza wa kila kitu”. Na hufanya kama hivyo kwa Marwah[2] mara tatu tatu. Na anapoteremka kutoka Safaa anatembea hadi kwenye tumbo la bonde (halafu) anakazana mwendo[3] mpaka atoke nje yake, na atachinja baadhi ya wanyama kwa mikono yake, na baadhi watachinjwa na wengineo". 

 

414. Abu Ubayda kasema, "Niliarifiwa kutoka kwa Urwa bin Zubeir kasema, "Ameniambia Ummu Ssalama (R.A.A.H.) mke wa Mtume (S.A.W.) kuwa, "Nilimtajia Mjumbe wa Allah (S.A.W.) ya kwamba mimi ninaumwa akasema, "

«طُوفِي بِالْبَيْتِ وَرَاءَ النَّاسِ وَأَنْتِ رَاكِبَةٌ»

Maana yake, “Tufu (izunguke) L-Ka`aba nyuma ya watu nawe umepanda kipando”. Kasema, "Nikatufu na Mtume (S.A.W.) wakati huo anasali upande mmojawapo wa L-Ka`aba na huku akisoma, " 

{وَالطُّورِ وَكِتَابٍ مَّسْطُورٍ}.

Maana yake, “Naapa kwa mlima wa T'ur. Na Kitabu kilichoandikwa[4] 

 

415. Abu Ubayda kasema, "Niliarifiwa kutoka kwa Jaabir bin Abdillah (R.A.A.) kasema, "Nilimsikia Mtume (S.A.W.) akisema wakati alipokuwa akitoka Msikitini akienda Safaa, "

«نَبْدَأُ بِمَا بَدَأَ اللَّهُ بِهِ».

Maana yake, “Tunaanza kama alivyoanza Allah”.

 

416. Abu Ubayda kasema, "Niliarifiwa kutoka kwa Urwa bin Zubeir kasema, "Nilimwambia Aisha (R.A.A.H). wakati ule mimi nilikuwa bado kijana mdogo, uliiona kauli ya Allah inayosema,  "

{إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللَّهِ فَمَنْ حَجَّ الْبَيْتَ أَوِ اعْتَمَرَ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ يَّطَّوَّفَ بِهِمَا}[5]

Maana yake, “{Hakika vilima vya Safaa na Marwa ni katika alama za kuadhimisha dini ya Allah. Basi anayehiji kwenye Nyumba hiyo, au kufanya Umra, si kosa kwake kuvizunguka (vilima) hivyo viwili}, Sioni kama pana ubaya wowote ikiwa mtu hakuvizunguka (vilima) hivyo viwili". Aisha (R.A.A.H.) akasema, "

 لَوْ كَانَ اْلأَمْرُ كَمَا تَقُوْلُ كَانَ فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ لاَ يَطَّوَّفَ بِهِمَا .

Maana yake, “Ingalikuwa hivyo unavyosema ni sawa basi aya ingalisomeka, "

 فَلاَ جُنَاحَ عَلَيْهِ أَنْ لاَ يَطَّوَّفَ بِهِمَا.

Maana yake, "{Basi hakuna makosa kama hataizunguka vilima hivyo}, lakini aya hii wameteremshiwa Ma-Ansari, walikuwa wakiharamisha, na kuzuia (kuzunguka vilima hivyo) kutokana na kuwepo jiwe (la ibada zao kabla ya kuja Uislamu) Manata. Na jiwe hilo Manat lilikuwa nyuma ya Qudayd, walikuwa wakikhofia kuzunguka baina ya Safaa na Marwaa. Lakini ulipokuja Uislamu walimwuliza Mtume (S.A.W.) juu ya hayo, Allah Mtukufu akateremsha  {إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ...} aya iliyo tajwa hapo juu”.

Arrabi`i kasema, "(مناة)" ni jiwe lililoko Qudayd lililo kuwa likiabudiwa kabla ya kuja Uislamu (zama za Ujahilia).

 

417. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid kasema, "Mtu mmoja alikuja kwa Abdullah bin Umar (R.A.A.) akasema, "Ewe Abu Abdu-Rrahmani nimekuona unafanya vitu vinne”. (Hadithi hii imeelezewa kwa kirefu punde hivi)[6].

 

418. Abu Ubayda, kutoka kwa Jaabir bin Zaid kasema, "Ilipoungua Baitil Llaahi L-Haraam kwa ajili ya kurukiwa na cheche za moto zilizopeperushwa na upepo, baadhi ya watu walitamka hayo yamekadiriwa na Allah Mtukufu, wengineo wakasema, "Si kudra ya Mola Mtukufu iungue Nyumba Yake. Hapa ndipo ilipoanza hitilafu mwanzo ya juu ya kudra".

 

419. Abu Ubayda kasema, "Niliarifiwa kwamba Mtume (S.A.W.) aliingia L-Ka`aba mnamo mwaka wa ufunguzi, na akasali humo rakaa mbili, kisha akatoka na walikuwako watu wengi wanaizunguka L-Ka`aba akazishika papi za mlango akasema, "

«الْحَمْدُ لِلَّهِ الذِي صَدَقَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ، وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ، مَاذَا تَقُولُونَ وَمَاذَا تَظُنُّونَ»[7]

ALHAMDULLILAH AL`LADHII SADAKA WA`ADAHU, WA HAZAMA AL`AH`ZABA WAH`DAHU.

Maana yake, “Ninamshukuru Allah Ambaye ametimiza ahadi Yake, na akamnusuru mja Wake, na akayashinda makundi ya watu peke Yake. Jee nyinyi mnasema nini na mnadhani nini?”. Wakasema, "Tunasema yaliyo ya kheri, na tunadhani yaliyo ya kheri, wewe ndugu karimu una uwezo tufanyie yaliyo mepesi, na utupe msamaha mkunjufu, akasema, "

«وَأَنَا أَقُولُ كَمَا قَالَ أَخِي يُوسُفُ: {لاَ تَثْرِيبَ عَلَيْكُمُ الْيَوْمَ يَغْفِرُ اللَّهُ لَكُمْ وَهُوَ أَرْحَمُ الرَّاحِمِينَ}، أَلاَ إِنَّ كُلَّ رِبًا فِي الْجَاهِلِيَّةِ وَدَمٍ وَمَالٍ أَوْ مَأْثَرَةٍ فَهِيَ تَحْتَ قَدَمَيَّ هَاتَيْنِ، إِلاَّ سِدَانَةَ الْبَيْتِ وَسِقَايَةَ الْحَاجِّ فَإِنِّي قَدْ أَمْضَيْتُهَا لأَهْلِهَا عَلَى مَا كَانَتَا عَلَيْهِ، أَلاَ وَإِنَّ اللَّهَ تَعَالَى قَدْ أَذْهَبَ نَخْوَةَ الْجَاهِلِيَّةِ وَتَكَبُّرَهَا بِالآبَاءِ، كُلُّكُمْ لآدَمَ وَآدَمُ مِنْ تُرَابٍ، لَيْسَ إِلاَّ مُؤْمِنٌ تَقِيٌّ، أَوْ فَاجِرٌ شَقِيٌّ، وَأَكْرَمُكُمْ عِنْدَ اللَّهِ أَتْقَاكُمْ، أَلاَ فِي قَتِيلِ الْعَصَا وَالسَّوْطِ وَالْخَطَأِ شِبْهِ الْعَمْدِ الدِّيَةُ مُغَلَّظَةً: مِائَةٌ مِنَ الإِبِلِ، مِنْهَا أَرْبَعُونَ خَلِفَةً. مَكَّةُ حَرَامٌ حَرَّمَهَا اللَّهُ تَعَالَى إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ، لَمْ تَحِلَّ لأَحَدٍ وَلاَ تَحِلُّ لأَحَدٍ بَعْدِي، وَإِنَّمَا أُحِلَّتْ لِي سَاعَةً مِنْ نَهَارٍ»

Maana yake, “Na mimi nasema kama alivyosema ndugu yangu Yuusuf. {Leo hapana lawama juu yenu. Allah atakusameheni, Naye ni Mwingi wa kurehemu kuliko wote wanaorehemu}[8]. Jueni kwamba kila riba iliyofanyika zama za ujahilia[9], damu, na mali, au utukufu na majivuno, basi nimeyaweka chini ya miguu yangu miwili hii hapa,[10] isipokuwa uangalizi wa L-Ka`aba, na kunywesha maji mahujaji, nimewakabidhi wenyewe wanaostahiki, kama ilivyokuwa mwanzoni. Jueni kwamba Allah Mtukufu ameondosha majivuno ya kijahilia, na kufakharishana kwa mababa. Nyinyi nyote mmetokana na Adam, na Adam (kaumbwa) kutokana na mchanga. Hapana isipokuwa Mwislamu mchaMungu, au muasi muovu. Na aheshimiwaye zaidi miongoni mwenu mbele ya Allah ni yule amchaye mcha Mungu zaidi katika nyinyi. Juweni kwa mwenye kuuwawa kwa fimbo, au kiboko, au kwa kukosea, ni mfano wa kuazimia kimakusudi, inalazimu kutoa dia nzito ya ngamia mia, kati yao arubaini wenye mimba. Makka pamefanywa patakatifu, Allah Mtukufu amepafanya kuwa patakatifu mpaka siku ya Kiyama. Haikuhalalishiwa kwa yeyote kabla yangu, na wala kuhalalishiwa yeyote baada yangu. Lakini nilihalalishiwa saa moja katika mchana mmoja. Akasema, "Mtume (S.A.W.) akaashiria kwa mkono wake na akasema, "

«لاَ يُنَفَّرُ صَيْدُهَا، وَلاَ يُقْطَعُ شَجَرُهَا، وَلاَ تَحِلُّ لُقْطَتُهَا إِلاَّ لِمُنْشِدٍ وَلاَ يُخْتَلَى خَلاَهَا»

Maana yake, “Wanyama wake wasiwindwe, wala miti yake isikatwe, wala si halali kukiokota kitu ila ikiwa kwa kukitangaza, na wala majani yake yasikatwe”.[1] Moja ya jabali lilipo Makka ambapo mahujjaj wanapofanya ibada ya Hijja wanatembea baina yake.

[2] Moja ya jabali lilipo Makka ambapo mahujjaj wanapofanya ibada ya Hijja wanatembea baina yake

[3] Anachapuka kwa kwenda haraka, au anagangira.

[4] Surat Attu`r aya ya 1 na aya ya 2.

[5] Surat Al- Baqarah aya ya 158.

[6] Hadithi namba 401.

[7] Hadithi hii imetajwa katika Hadithi namba 411.

[8] Surat Yusuf aya ya 92.

[9] Zama za giza kabla ya uisilamu.

[10] Yaani yamebatilishwa na kutenguliwa na kuondoshwa.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment