Ibadhi.com

SAUMU NYINGINE ZILIZO ZA WAJIBU.

Zaidi ya saumu ya mwezi wa Ramadhani ambayo ni faridha kwa kila Mwislamu alietimiza shuruti zake, zipo saumu nyingine ambazo ni wajibu kwa yule ziliyomuwajibikia kufuatana na hali na sababu zenyewe, kama ifuatavyo.

 

1. Kafara ya kuapa.

Ikiwa mtu ataapa kwa jambo, na akataka kubadilisha kiapo chake alichoapa, mfano mtu kaapa: kutoingia katika nyumba ya ndugu yake, na akataka kukibadilisha kiapo chake, basi kafara yake ni kulisha, au kuvisha masikini kumi, au kumpa mtumwa uhuru, kwa asie kuwa na uwezo ni kufunga siku tatu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 89,"

﴿........فمَنْ لم يجدْ فصيامُ ثلاثة أيامٍ، ذلك كفارة أيْمانِكُم إذا حَلَفْتُمْ.

Maana yake, "[Mwenyezi Mungu hatakuteseni kwa viapo vyenu vya upuuzi, lakini atakukamateni kwa viapo mlivyoapa kwa nia mliofunga barabara. Basi kafara yake ni kuwalisha masikini kumi kwa chakula cha katikati mnachowalisha watu wa majumbani mwenu, au kuwavisha, au kumpa uungwana mtumwa]. Lakini asiyeweza kupata hayo, basi afunge siku tatu." Maneno niliyo yatia katika kifungo (bracket) ni tafsiri ya mwanzo ya aya ambayo siku ileta kiarabu.

 

2.Kafara ya kumuua Mwislamu bila ya kukusudia.

Ikiwa mtu atamuua Mwislamu bila ya kukusudia, na hana mtumwa wa kuachia uhuru, basi itabidi afunge miezi miwili mfululizo. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat An-Nnisaai aya ya 92,"

﴿وَ مَنْ قتلَ مُؤْمناً خَطأ فتحرير رقبةٍ مؤمنة........فمن لم يجدْ فصيامُ شهْرينِ مُتتابِعَيْن.

Maana yake, "Na haiwi Muumini kumuuwa Muumini ila kwa kukosea. Na mwenye kumuuwa Muumini kwa kukosea basi amkomboe mtumwa aliye Muumini, na atoe diya kuwapa jamaa za maiti, isipo kuwa waache wenyewe kuwa ni sadaka. Na akiwa ni jamaa wa maadui zenu, hali yeye ni Muumini, basi ni kumkomboa mtumwa aliye Muumini. Na akiwa ni miongoni wa watu ambao pana ahadi baina yenu na wao basi wapewe diya watu wake na akombolewe mtumwa Muumini. Na asiye pata, basi afunge miezi miwili mfululizo, kuwa ni toba kwa Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi na Mwenye hikima”.

 

3.Kumtenga mke kwa kumfananisha na mama.

Ikiwa mtu atamtenga mkewe bila ya kumuacha kwa  kumfananisha kama vile mama yake, na baada ya muda akarudisha nafsi yake, na akataka kurudiana na mkewe, basi itambidi  atoe kafara ya kufunga miezi miwili mfululizo, kwa yule asieweza kuachia mtumwa uhuru. Na desturi hii ya mtu kumtenga mkewe bila kumuacha walikuwa nayo Waarabu wakati wa kabla ya Uislamu. Ilikuwa mtu akimchoka mkewe anamtenga bila ya kumuacha, akimuambia kuwa anamuona kama mama yake. Inakuwa mwanamke huyu hakuachika, na huyo mume, na haishi nae, lakini pia hawezi kuolewa na mtu mwingine, na wakati huo anakuwa hana haki na mumewe. Hali hii iliendelea mpaka mwanamke mmoja alipokwenda kumshtakia Mtume S.A.W. Mwenyezi Mungu Mtukufu akashusha hukumu Yake katika Surat Al-Mujaadalah aya ya 3 na ya 4,  ''

﴿والذين يُظاهرُون مِنْ نِسائهم ثمَّ يَعُودون لِمَا قالوا فتحرير رقبةٍ مِنْ قبل يتماسَّا.....فمنْ لم يجد فصيامُ شهْرينِ متتابِعَيْنِ.

Maana yake, "Na wale wawaitao wake zao mama zao, kisha wakawarudia katika yale waliyoyasema, (wakataka kuwarejea wake zao wakae nao kama kidasturi ya mke na mume), [basi wampe mtumwa uhuru kabla ya kugusana. Mnapewa maonyo kwa haya. Na Mwenyezi Mungu anajua (yote) mnayoyatenda]. Na asiyepata (mtumwa) basi afunge saumu ya miezi miwili mfululizo kabla ya kugusana. Maneno niliyo yatia katika kifungo (bracket) ni tafsiri ya mwanzo ya aya ambayo siku ileta.

 

4.Kafara kwa kuingiliana mchana Ramadhani.

Ikiwa mtu ataingiliana na mkewe mchana wa mwezi wa Ramadhani au atajitoa manii mchana kwa makusudi, saumu yake itaharibika na itaibidi ailipe siku ile na kafara yake ni kufunga miezi miwili mfululizo kwa yule asieweza kuachia mtumwa uhuru. Hadithi iliyotolewa na Abu Huraira kasema, "Mtu mmoja alimjia Mtume S.A.W. akasema, "Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu mimi nimeangamia!" Mtume S.A.W akamuuliza kipi kilicho kuangamiza?" Akasema, "Nimemuingilia mke wangu mchana wakati wa Mwezi wa Ramadhani." Mtume S.A.W. akamuuliza, "Jee unaweza kuachia mtumwa huru?" Akajibu, "La sina." Mtume S.A.W. akasema, "Jee unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?" Akasema, "La" Mtume S.A.W. akasema, "Jee unaweza kulisha masikini sitini?" Akasema, "La" Mtume S.A.W. akasema, "Kaa" Kikapu cha tende kikaletwa kwa Mtume S.A.W. na akasema, " Toa hizi kama sadaka."  Yule mtu akasema, "Kwa mtu alie masikini kuliko sisi? Hakuna mtu katika mji huu ambae ni alie masikini kuliko sisi!" Mtume S.A.W. akacheka mpaka mwanya wa meno yake ukaonekana akasema, "Nenda kailishe familia yako."        

 

5.Saumu ya Nadhiri.

Hii ni saumu ambayo mtu amejilazimishia mwenyewe nafsi yake. Mtu yoyote alieweka nadhiri ya kufunga kwa ajili ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kufanikiwa na jambo fulani, na ikiwa litatokea jinsi alivyotarajia, basi itakuwa kwake ni lazima atimize nadhiri yake kwa kama jinsi alivyonuia.

 

6.Saumu ya asie na kichinjo katika Hijja ya Tamatu`u.

Ikiwa mtu atafanya Hijja ya Tamat`uu, inamuajibikia  kuchinja ikiwa ana uwezo, na ikiwa hana uwezo basi inamuajibikia kufunga siku kumi. Siku tatu akiwa bado yupo katika Hajj na siku Saba akirejea nyumbani kwake. Kasema Mola Mtukufu katika Suratil Baqara aya 196, “

﴿فَمَن تَمَتَّعَ بِالْعُمْرَةِ إِلَى الْحَجِّ فَمَا اسْتَيْسَرَ مِنَ الْهَدْيِ فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ.

Maana yake, “Basi mwenye kujistarehesha kwa kufanya Umra kisha ndio akahiji, basi achinje mnyama aliye mwepesi kumpata. Na asiye pata, afunge siku tatu katika Hija na siku saba mtakapo rudi; hizi ni kumi kaamili”.

 

7. Kafara ya kuwinda wanyama pori kwa aliye Hirimia.

Ikiwa mtu amehirimia kwa ajili ya Haji, halafu akawinda na kumuua mnyama wa pori, basi itabidi atoe kafara ya kuchinja mnyama sawa na yule aliemuua. Mnyama huyo wa kafara achinjwe katika maeneo matukufu ya Al-Kaaba ya Makka. Nyama ya  mnyama yule walishwe masikini; au ikiwa hawezi kuchinja basi afunge. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 95, “

﴿وَمَن قَتَلَهُ مِنكُم مُّتَعَمِّداً فَجَزَاء مِّثْلُ مَا قَتَلَ مِنَ النَّعَمِ يَحْكُمُ بِهِ ذَوَا عَدْلٍ مِّنكُمْ هَدْياً بَالِغَ الْكَعْبَةِ أَوْ كَفَّارَةٌ طَعَامُ مَسَاكِينَ أَو عَدْلُ ذَلِكَ صِيَاماً.

Maana yake, "Enyi mlio amini! Msiue wanyama wa kuwinda nanyi mmeharimia katika Hija. Na miongoni mwenu atakaye muuwa makusudi, basi malipo yake yatakuwa kwa kuchinja kilicho sawa na alicho kiuwa, katika mifugo, kama wanavyo hukumu waadilifu wawili miongoni mwenu. Mnyama huyo apelekwe kwenye Al Kaaba, au kutoa kafara kwa kuwalisha masikini; au badala ya hayo ni kufunga”. Na hii imekusudiwa wanyama wa pori tu na wala siyo wanyama wa baharini. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Maida aya ya 96, “

أُحِلَّ لَكُمْ صَيْدُ الْبَحْرِ وَطَعَامُهُ مَتَاعاً لَّكُمْ وَلِلسَّيَّارَةِ وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُماً.

Maana yake, “Nyinyi mmehalalishiwa kuvua vinyama vya baharini na kuvila, kwa faida yenu na kwa wasafiri. Na mmeharamishiwa mawindo ya wanyama wa bara (nchi kavu) madamu mmeharimia Hija”.

SH. Abdullah Al Shueli

Website: https://ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment