Ibadhi.com

WALIO RUHUSIWA KUTOFUNGA.

Hali za watu zinatofautiana kufuatana na afya zao, na umri wao. Kwa hali hiyo uwezo wao wa kufanya ibada pia unatofautiana. Mwenyezi Mungu Mtukufu haikalifishi nafsi yoyote ile zaidi ya uwezo wake alioipa, Naye ni Mwenye kufahamu, na Mjuzi wa kila jambo, na kaifanya dini hii ni nyepesi kwa kwa waja Wake. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Hajj aya ya 78, “

﴿وَ مَا جَعَلَ عَلَيْكُمْ فىِ الدِّينِ مِنْ حَرَجِ مِّلَّةَ أَبِيكُمْ إِبْرَاهِيمَ.

Maana yake, “Wala hakuweka mambo mazito katika dini (Nayo dini hii) ni mila ya baba yenu Ibrahim.” Pia kasema katika Surat AN-Nisaai aya ya 28, “

﴿يُريِدُ الله أن يُخَفِّفَ عَنكُمْ وَ خُلِقَ الإِنسَانُ ضَعِيفًا.

Maana, “Mwenyezi Mungu anataka kukukhafifishieni maana mwanaadamu ameumbwa dhaifu.”

Watu wenye dharura walioruhusiwa kutofunga wamegawanyika sehemu tatu kama ifuatavyo:

(1) Watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na baadae wanalazimika kuzilipa saumu zao.

(2) Watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na badala yake  kutoa fidia.

(3) Watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao za wakati ule, na baadae kufunga, na kutoa fidia.

 

WANAO TAKIWA KULIPA SAUMU.

Wafuatao ni baadhi ya watu ambao wameruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na baadae kuzilipa saumu zao kwa kufunga baada ya dhurufu zao kuondoka:

 

1.Wanawake wenye hedhi na ujusi:

Wanawake wenye hedhi, na wale wanaotoka damu ya ujusi[1], wao wanaruhusiwa kisheria kutokufunga, na baada ya kutoharika wafunge zile siku ambazo walikuwa hawa kuzifunga. Na ikiwa kama watafunga na hali wako katika hali hiyo basi saumu zao hazikubaliwi, na watakuwa wamefanya maasi. Hadithi ya Bibi Aisha R.A.A.H. kasema,[2]

كُنَّا نَحِيضُ عِنْدَ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَيَأْمُرُنَا بِقَضَاءِ الصَّوْم ولا نؤمر بقضاء الصلاة.

Maana yake, “Tulikuwa tukipata hedhi wakati wa Mtume S.A.W. na alikuwa anatuamrisha kulipa saumu (na wala hatukuamrishwa kulipa Sala)[3].”

 

2.Mtu alie na maradhi.

Mtu aliepatwa  na maradhi, na akahofia maradhi yake kuzidi, au kupata madhara iwapo atafunga, basi anaruhusiwa kutofunga, na baadae Mwenyezi Mungu Mtukufu akimuondolea maradhi yake kulipa siku zile ambazo alizokuwa hakuzifunga. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya aya 184, “

﴿فمن كان منكم مَّريضًا أو على سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Basi atakaekuwa mgonjwa miongoni mwenu au yuko safari (akafungua) basi (atimize) hisabu katika siku nyingine.”

 

4.Kuzidiwa na saumu:

Ikiwa mtu atazidiwa na saumu kwa sababu ya kiu,  au njaa, na akahofia kumsababishia madhara, basi anaruhusiwa kula, au kunywa, kiasi tu cha kumuondolea yale madhara. Ikimuondokea hali ile ya madhara basi, ajizue kula, au kunywa, tena mchana ule uliobakia. Baada ya Ramadhani siku hiyo itabidi ailipe. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Suratil Baqara aya 195, “

﴿ولاَ تُلْقُواْ بِأَيْديكُمْ إلى التَّهْلُكَةِ.

Maana yake, “Wala msijitie kwa mikono yenu katika maangamizo.” Pia kasema katika Suratil Baqara aya ya 185, “

﴿يُريِدُ الله بِكُمُ الْيُسْرَ و لا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito.”

 

WANATOA FIDIA BADALA YA KUFUNGA.

Wafuatao ni baadhi ya watu ambao kufuatana na hali zao hawalazimiki kufunga, na badala yake kutoa fidia katika kila siku ambazo hawakufunga:

 

1.Wazee wasioweza kufunga.

Wale wote ambao kwa sababu ya umri wao kuwa mkubwa, na kuwafanya wawe dhaifu kiasi cha kutoweza kufunga au kutoweza kuvumilia njaa,  basi wao wanaruhusiwa kutokufunga na badala yake kutoa fidia kwa kulisha masikini. Kila siku moja ambayo hakuifunga atalisha masikini mmoja mlo mmoja. Kasema  Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 184, “ 

﴿وَ عَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ, فِديَةٌ طَعَامُ مِسكِينٍ.

Maana yake, “Na wale wasioweza (kufunga), watoe fidia kwa kumlisha masikini.” Na akasema Ibn Abbas aya hii imeshuka kwa ajili ya watu wazee sana, na ambao hawawezi kufunga. Pia Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat At-Taghaabun aya ya 16, “

﴿فَاْتَّقُواْ الله مَااْستَطَعتُمْ.

Maana yake, “Mucheni Mwenyezi Mungu muwezavyo.” Yaani mtu afanye ibada kufuatana na uwezo wake. Na pia Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 286, “

﴿لاَ يُكَلِّفُ الله نَفْسًا إلاَّ وُسْعَهَا.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yeyote ila yaliyo sawa na uweza wake.” Pia kasema katika Surat AN-Nnisaai aya ya 29, “

﴿وَلاَ تَقْتُلُوا أَنفُسَكُمْ إِنَّ الله كَانَ بِكُمْ رَحِيمًا.

Maana yake, “Wala msijiue nafsi zenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kukuhurumieni.”

 

2.Mtu alie na maradhi yasiyopona.

Mtu yoyote alie na maradhi yasiyopona ambayo yatamsababisha asiweze kufunga anaruhusiwa kutokufunga na baadae kulipa fidia kwa kila siku aliyoacha kufunga kulisha masikini mmoja siku moja mlo mmoja.

 

KULIPA SAUMU KWA KUFUNGA.

Wafuatao ni watu ambao wanaruhusiwa kutokufunga kufuatana na hali zao, na badala yake kufunga baada ya dharura zao kuondoka:

 

1.Mama mja mzito, au mama anaenyonyesha.

Inaruhusiwa kwa mama mja mzito, na mama anaenyonyesha, ikiwa atahofia yeye, au mtoto wake, kupata madhara ya aina yoyote yale ikiwa atafunga wakati wa mimba yake, au wakati wa kunyonyesha, kutokufunga, na badala yake kulipa siku alizokula. Hadithi ya Anas bin Malik R.A.A kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[4]

إِنَّ اللَّهَ عَزَّ وَجَلَّ وَضَعَ لِلْمُسَافِرِ الصَّوْمَ وَشَطْرَ الصَّلَاةِ وَعَنْ الْحُبْلَى وَالْمُرْضِعِ.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu Mtukufu amemuondolea saumu msafiri na nusu ya sala, na (mwanamke) mwenye mimba na (mama) anaenyonyesha (saumu).”

 

2.Mtu alie na maradhi yenye kupona.

Mtu alie na maradhi ambayo yanapona anaruhusiwa kutokufunga wakati wa maradhi yake, na baadae kuilipa siku aliyokula wakati wa maradhi yake. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Baqarah aya ya 184, “

﴿فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine”.

 

3.Msafiri.

Msafiri anaruhusiwa kutokufunga wakati wa safari yake, na akisha rejea kutoka  safarini kwake, alipe siku alizofungua. Na kiwango cha masafa ya safari  ni sawa sawa na kiwango kile kile cha masafa ya safari cha kupunguza sala, yaani masafa ya umbali wa kilometa kumi na mbili. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 184, “

﴿فَمَن كَانَ مِنكُم مَّرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Na atakaye kuwa miongoni mwenu mgonjwa, au yumo safarini basi atimize hisabu katika siku nyengine”.

Na pia kasema katika Surat Al-Baqara aya ya 185, ambayo tumekwisha itaja hapo mwanzo. Na kama vile inaruhusiwa kutokufunga, pia inaruhusiwa kufunga kwa mwenye uwezo. Hadithi ya Bibi Aisha R.A.A.H. kasema, “Kasema Mtume S.A.W. kumuambia Hamza Bin Umar R.A.A.,[5]

صُمْ إِنْ شِئْتَ وَأَفْطِرْ إِنْ شِئْتَ.

Maana yake, “Ukipenda unaweza kufunga na ukipenda unaweza kula.” Kasema Mola Mtukufu katika Surat al-Baqara aya ya 185, “

﴿وَمَن كَانَ مَرِيضاً أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِّنْ أَيَّامٍ أُخَرَ يُرِيدُ اللَّهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلاَ يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ وَلِتُكْمِلُواْ الْعِدَّةَ وَلِتُكَبِّرُواْ اللَّهَ عَلَى مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ.

Maana yake, “Na mwenye kuwa mgonjwa au safarini, basi atimize hisabu katika siku nyengine. Mwenyezi Mungu anakutakieni yaliyo mepesi, wala hakutakieni yaliyo mazito, na mtimize hiyo hisabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushukuru”. Kwa yule msafirir mwenye uwezo wa kufunga ni bora zaidi kwake kufunga kuliko kuacha kufunga.[1] Hali ya kutokuwa msafi mwenye tohara kwa kutokwa damu au yale yanayotoka baada ya damu anayopata mwanamke aliyejifungua. Hali hii inatofautiana baina ya mwanamke na mwanamke aghalabu kwa wengi wao huwa ni siku arubaini lakini inaweza kuwa chini ya hapo au zaidi hata kufikia siku sitini.

[2] Abu Daawud 1/334 (229), Ibn Maajah 5/177 (1660), Muslim 2/232 (508).

[3] Sehemu hii imeongezwa na Abu Daawud na Muslim.

[4] Abu Daawud 6/375 (2056), An-Nasaai`y 8/10 (2276).

[5] Abu Daawud 1/328 (2050), At-Tirmidhiy 3/148 (645), Bukhaari 7/34 (1807).

SH. Abdullah Al Shueli

Website: https://ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Comments   
# Rashid Suleiman 2018-05-17 01:30
Assalaam alaikum.
Sheikh Al-Shuel, uniwie radhi
Nashkuru kwa uchambuzi wako kuhusu walioruhusiwa kutokufunga.
Baada kusoma kwa kina nimegundua kasoro ifuatayo;,
1. Kwamba umeeleza migawanyiko mitatu. Lkn mgawanyiko kwa kundi LA kulipa saum na fidia halipo.
Hivyo nakuomba ufafanuzi kipengele hicho
Reply
Add comment