Ibadhi.com

MAMBO YALIYO RUHUSIWA KWA ALIEFUNGA.

Mambo yaliyo ruhusiwa kwa aliefunga kuyafanya.

1.Kutia dawa masikioni. Haikatazwi kutia dawa masikioni kwani tundu la sikio halifiki kooni.”

2.Kutapika bila kukusudia. Kutapika bila kukusudia hakuharibu saumu ili mradi yale matapishi hayakurudi ndani.

3.Kuoga. Hadithi ya Abu Bakr bin AbduraRahman, kutokana kwa miongoni mwa masahaba, kasema, [1]"

رَأَيْتُ رَسُولَ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِالْعَرْجِ يَصُبُّ عَلَى رَأْسِهِ الْمَاءَ مِنْ الْعَطَشِ أَوْ مِنْ الْحَرِّ

Maana yake, "Nimemuona Mtume S.A.W. akimwagia kichwa chake maji wakati akiwa amefunga kwa ajili ya kiu au joto kali". Lakini kwa anayeoga anahitajia achukue hadhari maji yasimuingie ndani ya koo.

 

4.Kuonja chakula ili kujua ladha yake, bila ya kukimeza hii ikiwa ni dharura kwa mpishi, inaruhusiwa hata kumtafunia chakula kwa ajili ya mtoto bila kukimeza.

 

5.Kujitia mafuta mazuri na au kuyanusa.

 

6.Kutoa jino. Inaruhusiwa mradi damu isiingie kooni.

 

7.Kunusa manukato makali kama ubani na udi inaruhusiwa ikiwa ni harufu, bila ya moshi wake kuingia katika koo, ama ikiwa moshi wake utaingia katika koo basi inafunguza saumu kwa kauli ya baadhi ya wanavyuoni. Na Mwenyezi Mungu ndie mjuzi zaidi kwa hili.

 

8.Kumeza mate inaruhusiwa lakini yasiwe yawe kwanza yamekusanyika mdomoni, au yakachanganyika na kitu kingine, au akayotoa halafu akayameza, ikiwa itakuwa hivyo basi yanafunguza saumu. Ama makohozi na makamasi mtu akiyameza na ana uwezo wa kuyatoa yanafunguza saumu.

 

9. Kutoa damu inaruhusiwa, ikiwa kwa kumsaidia mtu au kwa kuipima. Kipimo kimechukuliwa na kama vile kufanya hijama.

 

10.Kupaka mafuta nje ya mwili

 

11.Kukata kucha, kukata nywele, na kujisafisha kwapa na sehemu za siri inaruhusiwa.

 

12.Kumbusu mke, au kumkumbatia inaruhusiwa lakini yasiwepo matamanio. Hadithi ya Jabir R.A.A. kasema, "Kasema Umar R.A.A,[2]

هَشَشْتُ فَقَبَّلْتُ وَأَنَا صَائِمٌ، فَقُلْتُ: يَا رَسُولَ اللَّهِ صَنَعْتُ الْيَوْمَ أَمْرًا عَظِيمًا قَبَّلْتُ وَأَنَا صَائِمٌ، قَالَ:  أَرَأَيْتَ لَوْ مَضْمَضْتَ مِنَ الْمَاءِ وَأَنْتَ صَائِمٌ، قُلْتُ: لا بَأْسَ بِهِ، قَالَ: فَمَهْ"

Maana yake, “Nilikuwa nimefurahi, basi nikambusu mke wangu na mimi nimefunga,” (Akamuendea Mtume S.A.W akamuambia) “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimefanya jambo kubwa; nimembusu mke wangu nami nimefunga”. Akajibu, “Jee unafikiri vipi ukisukutua mdomo wako kwa maji na hali ya kuwa umefunga?”  Nikasema, “Haina tatizo” Akasema, “Ni mfano wake”.[1] Ahmad 32/70 (15338).

[2] Abu Daawud 6/346 (2037).

SH. Abdullah Al Shueli

Website: https://ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment