Ibadhi.com

YANAYO HARIBU SAUMU.

Yafuatayo hapa chini ni miongoni mwa mambo ambayo yamekatazwa kufanywa kwa aliefunga, wakati wa saumu yake, na ikiwa mtu atayafanya nae amefunga basi yanasababisha kufunguza saumu yake. Kama ifuatavyo:

 

1.Kuingiza kitu chochote kile mpaka ndani kooni.

Hairuhisiwi kuingiza chochote kile ndani kooni wakati mtu amefunga. Mfano wa: chakula, kinywaji, dawa, au kutia dawa kupitia puani, au machoni, kwani matundu hayo yanakwenda mpaka kooni. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 187, “

﴿وَ كُلُواْ وَاشْرَبُواْ حَتَّى يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الخَيْطُ الأَبْيَضُ مِنِ الخَيطِ الأسْوَدِ مِنَ الفَجْرِ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِيَامَ إلى الَّيْلِ.

Maana yake, “Na kuleni na kunyweni mpaka ukubainikieni weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku, kisha timizeni saumu mpaka usiku.”

 

2. Kujitoa manii.

Ikiwa mtu atajitoa manii kwa kukusudia kama vile kwa kujichezea, au kwa kufikiria, au kwa njia nyingine yoyote ile, basi saumu yake itaharibika. Lakini saumu haiharibiki kwa mtu kutokwa na manii kwa ajili ya kuota kwani hilio hutokea bila ya yeye kukusudia. Mara akiamka aende haraka kukoga josho kubwa ili kujitoharisha na ile janaba iliyompata, akijichelewesha bila ya sababu basi saumu yake itaharibika.

 

3.Kujitapisha kwa makusudi.

Ikiwa mtu atajitapisha kwa kukusudia, na yakamtoka matapishi basi saumu yake itakuwa imeharibika.  Hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.,[1]

مَنْ ذَرَعَهُ الْقَيْءُ فَلا قَضَاءَ عَلَيْهِ وَمَنْ اسْتَقَاءَ فَعَلَيْهِ الْقَضَاءُ.

Maana yake, “Ikiwa mtu atatapika bila kukusudia (nae amefunga) basi hailipi siku ile, na yule atakaejitapisha kwa makusudi inamuwajibikia ailipe siku ile.”

 

4. Kuingiliana mke na mume:

Kuingiliana mke na mume wakiwa wamefunga wakati wa mchana kuna haribu saumu, wakitokwa na manii, au wasitokwe na manii. Hadithi ya Abu Huraira, R.A.A. kasema[2], “Kasema Abu Huraira R.A.A., “Tulikuwa tumekaa pamoja na Mtume S.A.W. akaja mtu mmoja akasema, “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nimeangamia.” Mtume S.A.W. akamuuliza ni jambo gani lilokutokea?. Akajibu akasema, “Nimeingiliana na mke wangu wakati nimefunga.” Mtume S.A.W. akamuuliza,, “Jee unaweza kuachia mtumwa huru?” Akajibu, “Hawezi”. Mtume S.A.W. akamuuliza, “Jee unaweza kufunga miezi miwili mfululizo?” Akajibu, “Hawezi”. Mtume S.A.W. akamuuliza, “Jee unaweza kulisha masikini sitini?” Akajibu akasema, “Hawezi”. Mtume S.A.W. Akakaa kimya kwa muda na wakati ule tuliokuwa tukisubiri likaletwa kapu kubwa la tende kwa Mtume S.A.W. Mtume S.A.W. akauliza, “Yuko wapi aliekuwa akiuliza?” Akajibu, “Niko hapa”. Mtume S.A.W. akasema, “Chukua kikapu hiki cha tende na utoe sadaka.” Yule mtu akasema, “Jee nimpe mtu masikini kuliko mimi? Haki ya Mungu (Naapa kwa Mungu) hakuna familia iliyo masikini kuliko mimi katikati ya milima hii miwili.” Mtume S.A.W. akatabasamu mpaka mwanya wa meno yake ukaonekana halafu akasema, “Ilishe familia yako kwayo.” Iko ruhusa mtu kuingiliana na mkewe baada ya kwisha wakati wa saumu, yaani baada ya  kuingia kwa magharibi mpaka kabla ya kuingia alfajiri. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya 187, “

﴿أُحِلَّ لَكُمْ لَيْلَةَ الصِّيَامِ الرَّفَثُ إلى نِسآئِكُمْ، هُنَّ لباسّ لَكُمْ وَ أَنْتُمْ لِبَاس لَهُنَّ عَلِمَ الله أَنَّكُمْ كُنْتُمْ تَخْتانُون أَنْفُسَكُمْ فَتَابَ عَلَيْكُمْ وَعَفا عَنْكُمْ ، فَالئنَ بَاشِرُوهُنَّ وابْتَغُوا مَا كَتَبَ الله لَكُمْ.

Maana yake, “Mmehalalishiwa usiku wa saumu kuingiliana na wake zenu. Wao (hao wake zenu) ni (kama) nguo kwenu, na nyinyi ni (kama) nguo kwao. Mwenyezi Mungu anajua kwamba mlikuwa mkizihinisha nafsi zenu. Basi amekukubalieni toba yenu na amekusameheni. Basi sasa ingilianeni nao (wake zenu) na takeni aliyokuandikieni Mwenyezi Mungu.”

 

5.Kufanya madhambi:

Kufanya madhambi yote yamekatazwa wakati wote na kufanya madhambi makubwa wakati wa mchana kwa aliefunga ni katika madhambi makubwa na yana haribu saumu ya siku ile. Kasema Abu Huraira R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W., [3]

رُبَّ صَائِمٍ حَظُّهُ مِنْ صِيَامِهِ الْجُوعُ وَالْعَطَشُ.

Maana yake, “Inawezekana mtu aliefunga hakupata katika saumu yake isipokuwa njaa na kiu.” Pia hadithi iliyohadithiwa na Ibn Abbas R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W.[4],“

وَلاَ صَوْمَ إِلاَّ بِالْكَفِّ عَنْ مَحَارِمِ اللَّهِ.

 Maana yake, “Wala hakuna saumu isipokuwa kwa kujizuia na yaliyo haramishwa na Mwenyezi Mungu.” Pia hadithi ya Abu Huraira R.A.A. kasema, “Kasema Mtume S.A.W,[5]

مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ.

Maana yake, “Mtu asieacha kusema uongo na kuutumilia (huo uongo), basi Mwenyezi Mungu hana haja kwake yeye ya kuacha chakula chake, na kinywaji chake (yaani funga yake).” Na makusudio hapa ya yaliyo haramishwa na Mwenyezi Mungu ni kujizuia na kufanya madhambi. Na madhambi mengi makubwa ni maarufu na yanafahamika ikiwa ni pamoja na kula riba, kuiba, kudharau wazazi, kusema uongo na mengineyo mengi kama hayo.

Yako baadhi ya madhambi ambayo yameenea sana katika jamii, hata imefikia jamii kuyaona kama vile ni mwenendo wa maisha wa kawaida, kwa jinsi vile yalivyoingiliana na vitendo vya mwanaadamu vya kila siku katika, mazungumzo, kusikiliza na kutizama. Mtu akiyafanya basi yanamuharibia saumu yake, kama ifuatavyo:

 

KUZUNGUMZA.

*Kusengenya[6] ni katika madhambi makubwa na kunaharibu saumu. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu  katika Surat Al-H`ujuraat aya ya 12, “

﴿وَلاَ يَغْتَب  بعْضُكُمْ بَعْضًا أَيُحبُّ اَحَدُكُمْ أَ ن يَأكُلَ لَحْمَ أَخِيهِ مَيْتًا فَكَرِهْتُمُوُهُ.

Maana yake, “Wala baadhi yenu wasiwasengenye wengine. Jee mmoja wenu anapenda kula nyama ya nduguye aliekufa? La, hampendi.” Pia kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Qalam aya ya 10 na aya ya 11, “

﴿وَلاَ تُطِعْ كُلَّ حَلاَّفٍ مَّهِينٍ ﴿هَمَّازٍ مَّشَآءِ بِنَمِيمٍ.

Maana yake, “Wala usimtii kila muapaji sana, aliye dhalili. Msengenyaji (msemaji watu), aendaye akitia fitina.”  Pia Hadithi iliotolewa na Ibn Abbas R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W,[7]

الْغِيبَةُ تُفْطِرُ الصَّائِمَ وَتَنْقُضُ الْوُضُوءَ.

Maana yake, “Kusengenya (kusema watu kwa ubaya) kuna haribu saumu (yaani kuna futurisha) na kunaharibu udhu.” Pia kutoka kwa Hudhaifa R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[8]

لا يَدْخُلُ الْجَنَّةَ نَمَّامٌ.

Maana yake, “Haingii peponi msengenyaji.” Na hii ni ithibati yenye nguvu kuwa kusengenya ni katika jambo lililo katazwa na kukemewa kukubwa, na ni katika madhambi makubwa.

Na kama vile kusengenya kuna haribu saumu, basi pia maneno machafu, na maneno ya upuuzi, yanaharibu saumu, na mtu anayetaka kuihifadhi Saumu yake ajiepushe nayo. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat Al-Muuminun aya ya 3, “

﴿وَاْلَّذِينَ هُمْ عَنِ اْللَغْوِ مُعْرِضُونَ.

Maana yake, “Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi.”

 

*Kusema uongo. Kusema maneno ya uongo kunaharibu saumu na ni katika maasia makubwa. Hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W[9]., “

مَنْ لَمْ يَدَعْ قَوْلَ الزُّورِ وَالْعَمَلَ بِهِ فَلَيْسَ لِلَّهِ حَاجَةٌ فِي أَنْ يَدَعَ طَعَامَهُ وَشَرَابَهُ.

Maana yake, “Mtu asieacha kusema uongo na kuutumilia (huo uongo), basi Mwenyezi Mungu hana haja kwake yeye ya kuacha chakula chake na kinywaji chake (yaani funga yake).” Pia hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[10]

مَنْ غَشَّنَا فَلَيْسَ مِنَّا.

Maana yake, “Mwenye kutuhadaa sio katika sisi.” Na hii haijuzu kwa Mwisilamu wakati wowote ule.

 

KUANGALIA.

*Kuangalia mambo yaliyoharamishwa kwa kukusudia:

Kila jambo lililokatazwa na Mwenyezi Mungu kuliangalia, ikiwa mtu ataliangalia kwa kukusudia nae amefunga linaharibu saumu. Na kitu kilicho haramishwa kukiangalia dhati yake, basi hata picha ya kile kitu hukumu yake ni sawa na kama kitu chenyewe. Kasema Mwenyezi Mungu Mtukufu katika Surat An-Nnur aya ya 30 na 31,"

﴿قُلْ لِلْمُؤْمِنِينَ يَغُضُّوا مِنْ أَبْصَارِهِمْ} {وَقُلْ لِلْمُؤْمِنَاتِ يَغْضُضْنَ مِنْ أَبْصَارِهِنَّ.

Maana yake, “Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa). “Na waambie Waumini wanawake wainamishe macho yao.” Wasitazame yaliyo katazwa. Na baadhi ya mambo ambayo tumeharamishiwa kuangalia kwa kukusudia ni mfano:

 

*Kuangalia uchi wa mwenzako kwa kukusudia.

Kuangalia uchi wa mwenzio kwa kukusudia ni katika madhambi makubwa na kunaharibu saumu.  Kasema Mtume S.A.W.,[11]

لعن الله الناظر والمنظور اليه.

Maana yake, “Amelaaniwa anaeungalia uchi wa mwenziwe na anayeangaliwa (yaani anae uonyesha kwa kusudi)” Pia kutoka kwa Ibn Abbas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[12]

«مَلْعُونٌ مَنْ نَظَرَ إِلَى فَرْجِ أَخِيهِ»

Maana yake, “Amelaaniwa mwenye kuangalia uchi wa nduguye.” Na mtu haimstahikii laana ya Mwenyezi Mungu isipokuwa kwa kufanya madhambi makubwa. Jambo hili limeenea sana siku hizi kwani imekuwa ni jambo la kawaida watu kuangalia picha katika magazeti na television ambazo hazikukamilisha sitara, haya ni maasia na yanafunguza Saumu. Ikiwa mtu anataka kuihifadhi saumu yake basi ajiepushe na kuangalia kwa kukusudia picha hizo kwani hukumu yake ni kama kuangalia vitu vyenyewe. Sitara kwa ujumla na yale yanayokhusu mavazi na yanayokusudiwa katika uchi tumeyataja kata kitabu cha Fiqh juzuu ya kwanza na ya pili.

 

KUSIKILIZA.

Kusikiliza: Mambo yaliyo haramishwa kuyasikiliza kwa kukusudia kuyasikiliza ni maasia na yanaharibu saumu. Na jambo lililo haramishwa kulitamka ni haramu kulisikiliza kwa kukusudia. Mifano ya haya ni kama ifuatavyo:

*Kusikiliza muziki: Kusikiliza miziki na vinanda na zumari kwa kukusudia kumekatazwa na kunaharibu saumu. Kutoka kwa Ibn Abbas R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W,[13]

صَوْتَانِ مَلْعُونَانِ فِي الدُّنْيَا وَالآخِرَةِ: صَوْتُ مِزْمَارٍ عِنْدَ نَغْمَةٍ، وَصَوْتُ مُرِنَّةٍ عِنْدَ مُصِيبَةٍ.

 Maana yake, “Sauti mbili zimelaaniwa duniani na akhera sauti za zumari[14] wakati wa neema, na sauti ya yule anaelia huku anaomboleza wakati wa musiba”. Pia kasema Mtume S.A.W., [15]

لَيَكُونَنَّ مِن أُمَّتِي أَقْوَامٌ يَسْتَحِلُّونَ الْحِرَ وَالْحَرِيرَ وَالْخَمْرَ وَالْمَعَازِفَ.

Maana yake, “Watakuwepo katika umma wangu watu wenye kuchukulia: Zinaa[16], na (kuvaa) hariri na (kunywa) pombe na (kutumia/kusikiliza) ala za muziki (kama vile zumari, vinanda, filimbi) kuwa ni yenye kukubalika (yaani watayahalalisha kwa kubadilisha majina yake)”.

*Kusikiliza maneno yoyote ya uongo yaliyo katazwa kisheria au maneno ya kusengenya (kwa ubaya) kwa kukusudia ni maasia na yanaharibu saumu.

 

6. Kutokwa na damu ya hedhi.

Ikiwa mwanamke itamjia ada yake ya mwezi wakati wa mchana nae amefunga basi saumu yake ya siku hiyo itakuwa imeharibika. Hadithi ya Abi Said R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W. [17], “

أَلَيْسَ إِذَا حَاضَتْ لَمْ تُصَلِّ وَلَمْ تَصُمْ.

Maana yake, “Jee sio kweli kuwa mwanamke wakati akiwa na hedhi hasali na wala hafungi?.”

 

YAFUATAYO NI BAADHI YA MAMBO YA WAKATI HUU YALIOENEA AMBAYO YANAHARIBU  SAUMU.

7.Dawa ya pumu ya kuvuta (kibomba cha pumu), kikitumiwa wakati wa saumu.

8.Kusafisha mafigo.

9.Kuongezewa damu.

10.Kuongezwa maji kwa njia ya sindano kupitia mshipa wa damu (sakaya/drip).

11.Kutiwa dawa kupitia tundu la nyuma.

12.Sindano ya kuongeza chakula. Ama sindano ambayo inayotumika kwa ajili ya tiba isiyokuwa na virutubisho wanavyuoni wametofatiana katika jambo hilo, baadhi yao wanasema haiharibu saumu ili mradi dawa ile haikufika katika koo nah ii ndio kauli yenye nguvu zaidi. Na wengine wanasema zote zinaharibu saumu ya mtu zikitumika. Na Mwenyezi Mungu ndie mjuzi zaidi katika jambo hili.[1] Ibn Maajah 5/186 (1666), At-Tirmidhiy 3/162 (653).

[2] Muslim 1870.

[3] Ahmad 18/43 (8501)

[4] Al-Imamu Al Rabi`u 1/134 (329).

[5] Abu Daawud 6/316 (2015), Bukhaari 6/473 (1770).

[6] Kumsema mtu kwa jambo ambalo yeye hatopendezewa kulisikia wakati yeye akiwa hayupo, kumteta.

[7] Al-Imamu Al Rabi`u 1/130 (317).

[8] Muslim1/273 (151), Ahmad Hambal 5/391(23373).

[9] Bukhaari 6/472 (1770), Abu Daawud 6/316 (2015), Baihaqy 3/356 (1138).

[10] Muslim 1/366 (146), Al-Imamu Al Rabi`u 1/231 (582), Ibn Maajah 6/477 (2216).

[11] Baihaqy 7/99 (13344).

[12] Al-Imamu Al Rabi`u 1/250 (638).

[13] Al-Imamu Al Rabi`u 1/249 (636).

[14] Filimbi, kitu kinachotumiwa kutolewa sauti kikipulizwa na aghalabu huwa chembamba sehemu ya mdomoni na mwishoni huwa chenye kupanuka.

[15] Bukhaari 17/298 Mlango wa kuihalalisha pombe lakini namba ya Hadithi haikutajwa.

[16] Tendo la uasherati.

[17] Bukhaari 2/3 (293).

SH. Abdullah Al Shueli

Website: https://ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment