Ibadhi.com

YASIYOPENDEZA WAKATI WA SAUMU.

 

Vifuatavyo hapa chini ni vitendo visivyopendezwa kufanya na yule mwenye saumu wakati wa saumu yake.

 

1.Kubusiana na Kukumbatiana.

Haipendezi kwa mtu na mkewe kubusiana, na kukumbatiana wakati wa mchana wakiwa katika saumu zao, kwani inaweza kuwapelekea kufanya mambo yanayopelekea kufunguza saumu yao. Ingawa imethibiti kutoka kwa Mtume S.A.W. kuwa yeye alikuwa akimbusu Bibi Aisha R.A.A.H. wakati akiwa amefunga. Lakini Mtume S.A.W. alikuwa ni tofauti na watu wengine, yeye alikuwa ana uwezo wa kuimiliki nafsi yake zaidi kuliko mtu mwingine. Kasema Bibi Aisha R.A.A.H.[1]

كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُقَبِّلُ وَيُبَاشِرُ وَهُوَ صَائِمٌ وَكَانَ أَمْلَكَكُمْ لِإِرْبِهِ.

Maana yake, “Alikuwa Mtume S.A.W. akibusu, na akikumbatia nae amefunga, lakini yeye ni mwenye kuimiliki zaidi nafsi yake kuliko nyinyi.”  

 

2.Kufanya Hijama au kuumika.

Haipendezi kwa aliefunga kuumika, kwani kunaweza kumdhoofisha kwa ajili ya upungufu wa damu. Mtume S.A.W. Yeye aliumika hali ya kuwa  amefunga, lakini tusisahau kwamba uwezo wake ni tofauti na watu wengine. Kasema Ibn Abbas R.A.A, [2]

احْتَجَمَ وَهُوَ مُحْرِمٌ وَاحْتَجَمَ وَهُوَ صَائِمٌ.

Maana yake, “Mtume S.A.W. aliumika (alihajimu) wakati yeye alikuwa amehirimia, na aliuumika (alihajimu)  na yeye amefunga.”

 

3. Kutia maji puani na kuyavuta ndani.

Haipendezi kwa aliefunga kutia maji puani na kuyavuta ndani, kwa kukhofia maji yale yasije yakaingia ndani ya koo na yakamfunguza Saumu yake. Kasema Aasim kutoka kwa baba yake, "Kasema Mtume S.A.W.,[3]

إِذَا اسْتَنْشَقْتَ فَبَالِغْ إِلَّا أَنْ تَكُونَ صَائِمًا.

Maana yake, “Unapovuta maji puani (wakati wa kutawadha) basi hakikisha yamefika ndani isipokuwa ikiwa kama umefunga.”

 

4.Kugogomoa.

Kugogomoa ni kusukutua kwa kuyafikisha maji mpaka ndani kooni. Na kama vile haipendezi kutia maji puani na kuyavuta ndani kwa kukhofia yasiingie ndani  kooni, pia haipendezi kugogomoa kwa hofu ya yale maji kuingia ndani kooni yakamfunguza Saumu yake.[1] Bukhaari 7/9 (1792), Muslim 5/409 (1854).

[2] Bukhaari 7/28 (1802).

[3] Ibn Haziima 3/236 (1985), Ahmad 33/121 (15785). Al-Imamu Al Rabi`u 94.

SH. Abdullah Al Shueli

Website: https://ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment