Ibadhi.com

Zifuatazo ni shuruti ambazo ni lazima kwanza kukamilika ili saumu iweze kuwa sahihi. Na iwapo moja ya shuruti yoyote ile katika hizi itakosekana basi saumu hiyo itakuwa batili (yaani saumu hiyo itakuwa haikukamilika). Na shuruti zenyewe ni kama zifuatazo:

 

1.Kuwa Muislamu:

Ibada yoyote ile katika Uisilamu haikamiliki mpaka kwanza anaeifanya ibada hiyo awe ni Muislamu, na hii ni hali kadhalika kwa saumu. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Surat Al I`mran aya ya 85, “

﴿وَ مَن يَبْتَغِ غَيْرَ اْلإِسْلامِ دِيناً فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَ هُوَ فيِ اْلأَخِرَةِ مِنَ اْلْخَاسِرِينَ.

Maana yake, “Na anaetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake. Naye akhera atakuwa katika wenye khasara.” Sharti nyingine ya kukubaliwa vitendo ni uchamungu. Kasema Mola Mtukufu katika Surat Al-Maida aya 27, “

﴿إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ.     

Maana yake, “Mwenyezi Mungu huwapokelea wachamungu”.

 

2. Kuwa na akili timamu:

Kuwa na akili timamu ni sharti ya lazima kwa kila Muislamu anaetaka kufunga. Watu wasiokuwa na akili kwa maradhi au kwa uzee wamesamehewa kufunga na kufanya ibada nyingine. Hadithi iliohadithiwa na Al`Amash. Kasema Mtume S.A.W.,[1]

رُفِعَ الْقَلَمُ عَنْ ثَلاثَةٍ: عَنِ الْمَجْنُونِ حَتَّى يُفِيقَ، وَعَنِ النَّائِمِ حَتَّى يَسْتَيْقِظَ.

Maana yake, “Wamesamehewa katika uma wangu watu aina tatu: alie mwehu mpaka akili zirudi na alie lala mpaka aamke.”

 

3.Kubaleghe:

Kubaleghe ni sharti ya kukamilika kwa kuwajibika kwa ibada ya Saumu. Kasema Ibn Abbas R.A.A., "Kasema Mtume S.A.W[2], “

وَعَنِ الصَّبِيِّ حَتَّى يَحْتَلِمَ.

Maana yake, “Na  mtoto mdogo mpaka abaleghe Na alama ya kukua kwa mtoto mwanamume ni kuota nywele  sehemu zake za siri na kwapani, au kubadilika sauti, au kuota (kuhtalim), au kufika umri wa kiasi miaka kumi na tano. Na kwa mtoto wa kike ni kuanza kutoka damu ya hedhi. Kwa wale watoto ambao hawajabaleghe wao hawalazimiki kufunga, lakini ni bora kwa wazazi kuwaanzisha kufunga mapema ili kuwazowesha na  kuwapa moyo kabla ya kufikia umri wao wa kuanza kufunga. Hadithi ya Rabi`a bint Muawiyyah kasema[3], "

أَرْسَلَ النَّبِيّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ُ غَدَاةَ عَاشُورَاءَ إِلَى قُرَى الأَنْصَارِ مَنْ أَصْبَحَ مُفْطِرًا فَلْيُتِمَّ بَقِيَّةَ يَوْمِهِ، وَمَنْ أَصْبَحَ صَائِمًا فَليَصُمْ، قَالَتْ: فَكُنَّا نَصُومُهُ بَعْدُ وَنُصَوِّمُ صِبْيَانَنَا وَنَجْعَلُ لَهُمْ اللُّعْبَةَ مِنَ الْعِهْنِ فَإِذَا بَكَى أَحَدُهُمْ عَلَى الطَّعَامِ أَعْطَيْنَاهُ ذَاكَ حَتَّى يَكُونَ عِنْدَ الإِفْطَارِ.

Maana yake, “Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. alimtuma mjumbe wakati wa asubuhi ya siku ya Ashurah, katika makaazi ya Ansar, akatangaza akasema, “Yeyote yule aliemka hali ya kuwa hakufunga, basi na afunge muda wa siku uliobakia. Na yeyote yule alieamka hali ya kuwa amefunga toka asubuhi, basi aikamilishe saumu yake.” Akasema, “Kutoka tulipotangaziwa tulikuwa tunafunga pamoja na watoto wetu. Na tulikuwa tukiwafanyia watoto michezo ya kuchezea kwa pamba. Na kama mtoto mmoja akililia chakula, tulikuwa tukimpa mchezo wa kuchezea mpaka wakati wa kula.”

 

4.Kutoharika na hedhi na damu ya ujusi.

Haijuzu kwa mwanamke mwenye hedhi au damu ya ujusi (yaani damu ya uzazi) kufunga saumu. Na akifunga atakuwa amemuasi Mola Mtukufu na saumu yake haikubaliwi. Hadithi ya Abu Said R.A.A kasema, "Kasema Mtume S.A.W.,[4]

أَلَيْسَ إِذَا حَاضَتْ لَمْ تُصَلِّ وَلَمْ تَصُمْ قُلْنَ بَلَى قَالَ فَذَلِكِ مِنْ نُقْصَانِ دِينِهَا.

Maana yake, “Jee si hivyo akiwa katika hedhi hasali wala hafungi, kadhalika huo ni upungufu wa dini yake.” Pia Hadithi ya Bibi Aisha R.A.A.H kasema,[5]

كُنَّا نَحِيضُ عَلَى عَهْدِ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ ثُمَّ نَطْهُرُ فَيَأْمُرُنَا بِقَضَاءِ الصِّيَامِ وَلا يَأْمُرُنَا بِقَضَاءِ الصَّلاةِ.

Maana yake, “Tulikuwa tunapata hedhi wakati wa Mtume S.A.W. halafu tunatoharika, alikuwa akituamrisha kulipa saumu na wala hakutuamrisha kulipa Sala”.

Inapendeza kwa mwanamke mwenye hedhi, asile hadharani, ili watu wasiofahamu hali yake ya wakati ule wasimtuhumu kuhusu dini yake. Ama kwa mwanamke aliejifungua, na mwenye damu ya ujusi, yeye haina neon, hata akila hadharani kwani hali yake inaeleweka na kila mtu.

 

5.Kutoharika na janaba kabla ya kuingia alfajiri.

Mwenye janaba, aliyoipata kwa kuingiliana, au kwa kuota, au kwa njia nyingine yeyote ile, anatakiwa aoge janaba kabla ya kuingia alfajiri. Na ikiwa ataamka alfajiri na janaba kwa kukusudia, au kwa uvivu basi saumu yake ya siku ile itakuwa imeharibika. Na itamlazimu ajizuie asile chochote mchana ule. Baada ya Ramadhani itamuwajibika kuilipa siku ile. Hadithi iliyohadithiwa na Abu Huraira R.A.A. kasema, "Kasema Mtume S.A.W., [6]

مَنْ أَصْبَحَ جُنُبًا أَصْبَحَ مُفْطِرًا.

Maana yake, “Atakaeamka (asubuhi) hali ya kuwa ana janaba basi kaamka amefungua.” Yaani hana saumu. Kuna baadhi ya wanavyuoni wengine wanasema kuwa hata mtu akiamka na janaba haidhuru saumu yake (yaani haiharibiki) kwa kutegemea Hadithi ya Bibi Aisha R.A.A.H. kasema[7], "

كَانَ النَّبِيُّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ يُصْبِحُ جُنُبًا مِنْ غَيْرِ حُلُمٍ ثُمَّ يَصُومُ

Maana yake, "Alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akiamka nae mwenye janaba bila ya kuota halafu anafunga" Hadithi hii ni sahihi inayoelezea sunna ya kitendo cha Mtume S.A.W. Lakini  zinapokutana Hadithi mbili na ikitokezea kuna migongano baina yake basi hukumu yake kwenye elimu ni kuwa, ile Hadithi yenye kuamrisha au kukataza ya kauli inakuwa yenye nguvu zaidi na ndio yenye kufuatwa kwetu sisi, kuliko ile ilioelezea Sunna ya kitendo. Kwani inawezekana Sunna ya kitendo inaweza kuwa ni mahsusi kwake Mtume S.A.W. peke yake bila kuwahusisha waisilamu wengine. Kama vile alivyoruhusiwa yeye kuowa wake zaidi ya wanne, na waisilamu wengine wasipate kuruhusiwa, au kufunga saumu ya wisali ambayo kwa waisilamu wengine wameharamishiwa na kadhalika. Na masuala haya ni marefu sana kwa hali hiyo nimeona bora kuyaachia hapa. Na Mwenyezi Mungu ndio mjuzi zaidi, namuomba atuongoze wote katika haki. Na khitilafu hii isiwafanye waisilamu kubughudhiana.

6. Uwezo wa kufunga Saumu:

Wale ilio wanawajibika saumu, lakini kufuatana na hali zao za afya kwa ajili ya uzee, au maradhi yasiyopona, ambayo yanaweza kuwasababishia kupata madhara ikiwa watafunga, basi wao wanaruhusiwa kutokufunga, na badala yake walishe masikini. Kasema Mwenyezi Mungu katika Suratil Baqara aya ya 184, “

﴿وَعَلَى الَّذِينَ يُطِيقُونَهُ فِدْيَةٌ طَعَامُ مِسْكِينٍ

Maana yake, “Na wale wasio weza, watoe fidiya kwa kumlisha masikini”. Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yeyote ile isipokuwa kwa uwezo wake. Kasema katika Suratil Baqara aya ya 286, “

﴿لاَ يُكَلِّفُ اللّهُ نَفْساً إِلاَّ وُسْعَهَا.

Maana yake, “Mwenyezi Mungu haikalifishi nafsi yoyote ila kwa kadiri ya iwezavyo”.

 

7. Kuwa mkaazi.

Msafiri anaruhusiwa kutokufunga, na mara akisha maliza safari yake, baada ya Ramadhani alipe siku ambazo alizofungua. Nia ya kutokufunga siku ya safari iwekwe kutokea usiku wa kuamkia safari iliyokusudiwa. Kasema Mwenyezi Mungu S.W.T. katika Suratil Baqara aya ya184, “

﴿فَمَن كَانَ مِنكُم مَّريضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَرَ.

Maana yake, “Basi atakaekuwa mgonjwa miongoni mwenu au katika safari (akafungua) basi (atimize) hisabu katika siku nyingine.” Na pia kasema katika Suratil Baqara aya ya 185.

﴿وَ مَن كَانَ  مَّريضًا أَوْ عَلَى سَفَرٍ فَعِدَّةٌ مِنْ أَيَّامٍ أُخَج.

Maana yake, “Na atakayekuwa mgonjwa au yu safarini, basi atimize hisabu siku nyingine.” Pia Hadithi iliyo hadithiwa na Anas  kasema,[8]

سَافَرْنَا مَعَ رَسُولِ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ فَمِنَّا مَنْ صَامَ وَمِنَّا مَنْ أَفْطَرَ، فَلَمْ يَعِبِ الصَّائِمُ مِنَ الْمُفْطِرِ وَلاَ الْمُفْطِرُ مِنَ الصَّائِمِ.

Maana yake, “Tulisafiri pamoja na Mtume S.A.W., miongoni mwetu wapo waliofunga, na wengine hawakufunga. Wale waliofunga, hawakuwalaumu wasiofunga, na wala wale wasiofunga hawakuwalaumu waliofunga.” Yaani ni ruhusa iliyowazi kwa wote, kwa hivyo mtu anaetaka kufunga katika safari na afunge, na anaetaka kula katika safari na ale.”[1] Abu Daawud 11/479 (3823)

[2] Abu Daawud 11/479 (3823

[3] Nukhary 1824

[4] Bukhaari 3/2 (293).

[5] At-Tirmidhiy 3/269 (717).

[6] Al-Imamu Al Rabi`u 1/129 (315)

[7] Muslim 5/420 (1864) Pia mfano wa hadithi hii imetolewa na Bibi Umm Salama R.A.A.H. yeye kaongezea, "Kwa tendo la ndoa na bila kuilipa"

[8] Al-Imamu Al Rabi`u 1/126 (307)

Add comment