2. IMAMU RABII BIN HABIB AL-BASRIY AL-FARAHIDIY (R.A)

Written by

IMAMU RABII BIN HABIB AL-BASRIY AL-FARAHIDIY (R.A)

Imamu Rabiu bin Habib Al-Basri R.A anafahamika katika safu za Kiibadhi kwamba ni Abu Amru Al-Rabiu bin Habib Al-Basriy Al-Farahidiy, naye ni Imamu wa tatu wa Kiibadhi katika marejeo ya Kielimu, Imamu Rabii R.A kazaliwa Oman kati ya mwaka wa 75 mpaka 80 Hijiriya, kisha akahama na kuhamia Iraq katika mji wa Al-Basra na akaishi huko muda mwingi wa maisha yake ya kutafuta elimu na kusoma, kisha akarejea Oman mwishoni mwa maisha yake, na akahitimisha maisha yake katika nchi yake ya asili alipozaliwa ndani ya Oman, alifariki kati ya mwaka 171 na 180 Hijiria na aliongoza sala ya kusalia jeneza lake Imam Mussa bin Abi Jabir Al-Azkawi (r.a) na kaburi lake ni maarufu liko katika wilaya ya Liwa Oman.

Imamu huyu katajwa na Maulamaa wengi wa Kiibadhi na wasiokuwa wa Kiibadhi, pia katajwa na watangulizi katika fani ya Hadithi ambao ni wajuzi wa wapokezi na wasimulizi.

REJEA ZA KIIBADHI ZILIZOMTAJA IMAMU RABII BIN HABIIB (R.A):

Kwa hakika Imamu Rabii (r.a) ni maarufu sana katika safu za Ibadhi, basi hakuna kitabu kilichoandikwa na mwanachuoni wa Kiibadhi na kikazungumzia suala la Hadithi na Athari za Maimamu ila hutajwa Imamu huyu mwenye hadhi kubwa katika safu zao, kuanzia vitabu vya karne ya pili Hijiria hadi zama zetu hizi.

Basi Imamu Rabii bin Habib ametajwa katika vitabu mashuhuri hususan:

 1. KITABU "AL-SIYAR WAL-JAWABAATI" CHA MJUMUIKO WA MAULAMAA KUANZIA KARNE YA PILI HADI YA NNE.
 2. KITABU "AL-MUDAWWANA" CHA ABI GHAANIM AL-KHURASANIY. KILICHOANDIKWA MWANZO WA KARNE YA TATU.
 3. KITABU "AL-JAAMIU" CHA IBNU JAAFAR. KARNE YA TATU.
 4. KITABU "AL-JAAMIU" CHA ABU AL-HAWARIY KARNE YA TATU.
 5. KITABU "AL-MU'UTABAR" CHA IMAMU ABU SAID AL-KUDAMIY KARNE YA NNE.
 6. KITABU "AL-JAAMIU" CHA IBNU BARAKA. KARNE YA NNE.
 7. KITABU "AL-JAAMIU" CHA ABU AL-HASAN AL-BISYAWIY. KARNE YA NNE
 8. KITABU "BAYANU AL-SHAR'IY" CHA SHEIKH MUHAMMAD BIN IBRAHIM AL-KINDIY. KARNE YA TANO
 9. KITABU "AL-MUSANNAF" CHA SHEIKH AHMAD BIN ABDALLAH AL-KINDIY. KARNE YA SITA.
 10. KITABU "TABAQAATU AL-MASHAAYKH. CHA SHEIKH AL-DARJINIY. KARNE YA SABA.
 11. KITABU "AL-JAWAAHIRU AL-MUNTAQAA" CHA AL-BARAADIY. KARNE YA NANE.
 12. KITABU "AL-SIYAR" CHA Al-SHAMMAKHIY ALIEFARIKI MWAKA 928H.

Hivi ni vitabu ambavyo ametajwa ndani yake Al-Imam Al-Rabi'u bin Habib R.A kwa uwazi kabisa na kumzingatia kuwa ni Imamu wa tatu wa Madhehebu ya Kiibadhi, utakuta hapo kwamba Imamu huyu katajwa tangu karne ya pili na ya tatu na zilizofatia.

MASHEKHE WA AL-IMAMU AL-RABIU BIN HABIB (R.A):

Miongoni mwa masheik wa Al-Imamu Al-Rabiu bin Habib ni:

 1. Abu Ubayda Muslim bin Abi Karima Al-Tamimiy (R.A)
 2. Dhimam bin Saaib Al-Umaniy (R.A)
 3. Abu Nuh Saleh Al-Dahhan (R.A)

ATHARI ZA AL-IMAMU AL-RABIU BIN HABIB (R.A):

 1. Al-Musnad Al-Sahihi (المسند الصحيح)
 2. Kitabu "Aatharu Al-Rabii" (كتاب آثار الربيع)

Huu ni mukhtasari mfupi sana kutoka kwa Maibadhi kuhusu Imamu Al-Rabiu bin Habib.

REJEA ZISIZOKUWA ZA KIIBADHI :

Tufahamu kuwa hakuna ulazima wa kutajwa Maimamu wetu katika vitabu vya Maulamaa wa madhehebu nyengine yoyote, na bila shaka kila watu wana haki zaidi na watu watu wao; kwa hiyo shahada ya Maibadhi kutoka vitabuni mwao na kupitia Maulamaa wao ndiyo ya kutegemewa kwa kuwajua Maulamaa wao na Maimamu wa Kiibadhi, basi kuleta kwetu uthibitisho wa Imamu Rabii bin Habib Al-Basriy (r.a) kutoka katika vitabu vya wasiokuwa Ibadhi hususan Masunni ni kwa njia ya kuituliza nafsi ya mwenye shaka kwa wale wanaoona ulazima wa kutajwa Maimamu katika vitabu vyao, basi elewa kwamba miongoni mwa waliomtaja Imamu Rabii bin Habib R.A ni:

MAIMAMU WA KISUNNI:

1. Imamu Al-Bukhari:

Katika kitabu chake "Al-TAARIKHU AL-KABIIR" juzuu ya tatu ukurasa wa mia mbili na sabiini na saba (J.3 UK. 277):

ربيع بن حبيب : سمع الحسن وابن سيرين روى عن موسى البصري

((Rabi'u bin Habib: Kasikia kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, kapokea kutoka kwa Musa Al-Basariy)).

2. Ibnu Hibban:

Katika katika kitabu "AL-THIQAAT" (J. 6 UK. 299) amesema kwamba:

الربيع بن حبيب يروي عن الحسن وابن سيرين ، روى عن موسى بن إسماعيل

((Al-Rabi'u bin Habib kapokea kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, na kapokea kutoka kwa Musa bin Ismail)).

3. Ibnu Shaahiin:

Kasema katika kitabu chake "TAARIKHU ASMAAI AL-THIQAAT"  kwamba: "Na Al-Rabiu bin Habib vile vile ni Al-Bisriy, kapokea kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, naye ni Thiqa.

4. Yahya bin Ma'iin:

Katika kitabu chake "Al-Taarikh" kamtaja katika sehemu kadha wa kadha.

5. Ahmad bin Hambal:

Katika kitabu chake "AL-'ILAL WA MA'ARIFATUL AL-RIJAAL" (chapa ya Al-Maktabatu Al-Islaamiyatu chapa ya mwanzo 1408H-1988)

Anasema Abdallah mtoto wa Imamu Ahmad katika (J. 2 UK. 56 No. 1538) kwamba: Nimemsikia anasema: Ilikuwa anatujia mtu kutoka Basra anaitwa Al-Haytham bin AbdulGhaffar Al-Taaiy anatusimulia rai ya Qatada kutoka kwa Hammam, nakutoka kwa mtu anaeitwa Al-Rabiu bin Habib aliepokea kutoka kwa Dhummam kutoka kwa Jabir bin Zayd na kutoka kwa Rajaa bin Abi Salma….

Zingatia maneno haya:

 1. Alikuwa anatujia mtu kutoka Basra
 2. Anasimulia kutoka kwa mtu anaeitwa Al-Rabiu bin Habib aliepokea kutoka kwa Dhimam kutoka kwa Jabir bin Zayd.

Na andiko hili vile vile limo katika "TAARIKHU BAGHDAD" (J. 14 UK. 55) ila yeye huko kasema Hammam badala ya Dhimam, na bila shaka hili ni kosa (Tas-hiif) la uchanganyaji wa jina ambalo limethibiti usahihi wake katika maneno ya Ahmad bin Hambal, ama Jabir bin Zayd Abu Al-Sha'athaa R.A ni Imamu muasisi wa madhehebu ya Kiibadhi, ama Dhimam yeye ni Dhimam ibn Saaib Al-Umaniy naye ni Ibadhi vile vile.

6. Yahya bin Ma'iin

Kamtaja katika "AL-TAARIKH" chapa ya (DAARUL QALAM BEYRUT KWA RIWAYA YA AL-DUURIY) kamtaja katika sehemu mbili:

 1. Kamtaja katika (J. 2 UK. 157 NO. 3940)
 2. Kamtaja katika (J. 2 UK. 268 NO. 4723)

7. Al-Daulabiy

Kamtaja katika "Al-KUNA WA AL-ASMAA" (J. 2 UK. 74-75).

Na sisi tumetangulia kusema kwamba Dhimam ni katika Masheikh wa Imamu Al-Rabiu bin Habib.

Na kapokea Imamu Al-Rabiu bin Habib katika Musnad wake kutoka kwa Dhimam kutoka kwa Jabir bin Zayd Hadithi (no. 520) na kapokea kutoka kwake Hadithi mbili (no. 112 na 688) kupitia kwa Abu Ubayda Muslim.

Kwa hakika sisi hatujui aslan kuwepo kwa Al-Rabiu bin Habib aliyepokea kutoka kwa Dhammam bin Saaib ambaye ni muibadhi kutoka kwa Jabir bin Zayd ambaye ni muibadhi isipokuwa Imamu Rabii bin Habib ambaye ni Muibadhi.

Tufahamu kuwa katika jerea za Maimamu wa Kisunni wametawa Rabii bin Habib watatu, yaani jina hilo hilo kwa watu watatu tafauti nao ni:

1. Al-Rabiu bin Habib Abu Salma kutoka Al-Yamama:

Huyu kamataja Al-Bukhari katika "Al-Taarikh Al-Kabiir" na akamtaja Ibnu Hibban katika "Al-Thiqaat" na akamtaja Al-Dhahabi katika "Miizan Al-I'itidaal" na akamtaja Al-Maziyu katika "Tahdhiibu Al-Kamaal" na akamtaja Ibnu Hajar katika "Al-Tahdhiib" na katika "Al-Taqriib" naye ni Thiqa.

2. Al-Rabiu bin Habib Al-Kufi:

Huyu ni kaka wa Aaidh bin Habib ambao inasemwa kwamba wao ni katika Banu Al-Malaah.

Huyu kamtaja Al-Bukhari katika "Taarikh Al-Kabiir" na akamtaja Ibnu Hibban katika "Al-Majruuhiin" na akamtaja Al-Dhahabi katika "Al-Miizan" na akamtaja Al-Mazyu katika "Tahdhiibu Al-Kamaal" na akamtaja Ibnu Hajar katika "Al-Tahdhiib" na katika "Al-Taqriib" naye wametafautiana katika kukubalika kwake kihadithi.

3. Al-Rabiu bin Habib Al-Bisriy:

Huyu ndiye Imamu wetu mkusudiwa, na inatosha shahada ya Ibnu Ma'iin  katika kitabu chake "Al-Taarikh" anasema Ibnu Ma'iin katika Taarikh yake kwamba:

1. Al-Rabiu bin Habib vile vile ni Bisriy anapokea kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin naye ni Thiqa. (J. 1 UK. 260 NO. 1711)

2. Al-Rabiu bin Habib ni Bisryi naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 87 NO. 3406)

3. Al-Rabiu bin Habib ni Bisriy anahadithi kutoka kwa Al-Hassan na Ibnu Siirin, naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 113. NO. 3593)

4. Al-Rabiu bin Habib ni Bisriy naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 195 NO. 4206)

5. Al-Rabiu bin Habib ni Bisriy anapokea kutoka kwake Abu Daud na Affan, kama ilivyotangulia kauli ya Ibnu Shaahiin kuhusu yeye, naye ni Thiqa. (J. 2 UK. 263 NO.4697)

Wabillahi Taufiiq.

Asanteni sana.

Read 4280 times
Sh. Nasser Al - Mazrui

www.ibadhi.com | This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.

Latest from Sh. Nasser Al - Mazrui

Add comment


FaLang translation system by Faboba