Ibadhi.com

56.USIKU WA NUSU YA SHAABANI

Suali:

Tumesikia kuwa Allah mtukufu anaangalia waja wake katika usiku wa nusu ya shaabani kisha anawasamehe makosa yao yote isipokua mshirikina na mgomvi tu.

Jee! hili ni kweli?

JAWABU: 

Imekuja hadithi inayoeleza hayo, na siyo nusu ya Shaabani tu, bali na kila wiki Jumatatu na Alkhamisi, na uhakika wa mapokezi hayo ni uzushi alozuliwa Mtume S.A.W., kwa sababu madhambi yanasamehewa kwa kutubia na kujiepusha kumuasi Allah mtukufu, wala hayasamehewi kwa matarajiohewa ambayo Allah katuhadharisha nayo pale aliposema:

((لَّيْسَ بِأَمَانِيِّكُمْ وَلَا أَمَانِيِّ أَهْلِ الْكِتَابِ ۗ مَن يَعْمَلْ سُوءًا يُجْزَ بِهِ وَلَا يَجِدْ لَهُ مِن دُونِ اللَّهِ وَلِيًّا وَلَا نَصِيرًا ))

((Si kwa matarijiohewa yenu wala matarajiohewa ya wahusika wa Kitabu (Mayahudi na Manasara), yoyote atakayefanya uovu wowote atalipwa kwa uovu huo, na hatapata asiyekua Allah kipenzi wala mwenye kunusuru))

Kwa hiyo usamehevu wa makosa ni kwa kurejea kwa Allah mtukufu kwa kutubia na kuepuka kuasi, na sio kwa kujidanganya kwa riwaya za kupwangwa kisha akasemewa Mtume S.A.W.

Na wahusika wa Riwaya hizo ni wale wale aliotueleza Allah mtukufu kwenye Kitabu chake

((ذَٰلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَن تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَّعْدُودَاتٍ ۖ وَغَرَّهُمْ فِي دِينِهِم مَّا كَانُوا يَفْتَرُونَ))

((Hayo ni kwa sababu wao wamesema: "Sisi hautatugusa Moto isipokua siku chache." Na yakawadanganya katika dini yao yale waliokua wakiyazua))

Kwa hiyo tusikae na kudanganyika kwa maneno yao na riwaya zao.

Allah amesema:

((بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ ۚ وَمَن لَّمْ يَتُبْ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ ))

((Ubaya ulioje wa jina ya Ufasiki baaya ya Imani. Na asiyetubia hao hasa ndio Madhalimu)) 

Wala hakusema asubirie nusu ya Shaabani wala Jumatatu wala Alkhamisi atasamehewa tu,

Na amesema:

((إِن تَجْتَنِبُوا كَبَائِرَ مَا تُنْهَوْنَ عَنْهُ نُكَفِّرْ عَنكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَنُدْخِلْكُم مُّدْخَلًا كَرِيمًا ))

((Mukijiepusha makubwa muliokatazwa tutakusitirieni maovu yenu na tutakuingizeni maingizo ya kukirimiwa))

Wala hajasema: Mukijiepusha shirki na uhasama tutakusameheni maovu yenu na tutakuingizeni maingizo ya kukirimiwa.

Na likibainika hili itafahamika kuwa Usiku wa nusu ya Shaabani ni sawa na Misiku mengine isipokua Usiku wa Lailatu Alqadri ambao Allah ameueleza cheo chake katika Kitabu chake kwa wazi kabisa.

Wabillahi taufiqi.

 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment