Ibadhi.com

55. PEPO ITAKUA WAPI?

Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

Tumesikia kuwa Pepo itakua chini ya arshi mbinguni siku ya kiama na Jahannamu itakua chini katika ardhi ya saba, tunataka kujua uhakika wa hayo, tunaomba jawabu.

JAWABU:

Lililo muhimu kwa Muislamu katika maisha yake haya ya Duniani ni kuhakikisha sababu ya kuepukana na Jahannamu ili awe mja wa Peponi, na sababu hiyo ni Uchamungu, kwa kufanya aliyoamrisha Allah mtukufu na Mtume wake Muhammad S.A.W. na kuepuka makatazo yao, hili ndilo la muhimu katika maisha haya ya kutahiniwa hapa Duniani.

Ama kuhusu Pepo Allah mtukufu katika Kitabu chake ametwambia kuwa Ardhi na Mbingu zitabadilishwa siku ya Malipo, amesema:

يَوْمَ تُبَدَّلُ الْأَرْضُ غَيْرَ الْأَرْضِ وَالسَّمَاوَاتُ ۖ وَبَرَزُوا لِلَّهِ الْوَاحِدِ الْقَهَّارِ (48)

((Siku itakapobadishwa Ardhi isiyokua Ardhi hii na Mbingu, na watatoka kwa ajili ya Allah aliye mmoja mshindi)) [Ibrahim 48]

Na ametueleza kuhusu waja wa wake wema kuwa ndio watakaoirithi Ardhi

وَلَقَدْ كَتَبْنَا فِي الزَّبُورِ مِن بَعْدِ الذِّكْرِ أَنَّ الْأَرْضَ يَرِثُهَا عِبَادِيَ الصَّالِحُونَ (105)

((Na kwa hakika tuliandika katika Zaburi baada ya ukumbusho: Hakika Ardhi watairithi waja wangu walio wema.)) [Anbiyaa 105]

Na hao hao ndiwo waja wa Peponi:

وَسِيقَ الَّذِينَ اتَّقَوْا رَبَّهُمْ إِلَى الْجَنَّةِ زُمَرًا ۖ حَتَّىٰ إِذَا جَاءُوهَا وَفُتِحَتْ أَبْوَابُهَا وَقَالَ لَهُمْ خَزَنَتُهَا سَلَامٌ عَلَيْكُمْ طِبْتُمْ فَادْخُلُوهَا خَالِدِينَ (73) وَقَالُوا الْحَمْدُ لِلَّهِ الَّذِي صَدَقَنَا وَعْدَهُ وَأَوْرَثَنَا الْأَرْضَ نَتَبَوَّأُ مِنَ الْجَنَّةِ حَيْثُ نَشَاءُ ۖ فَنِعْمَ أَجْرُ الْعَامِلِينَ (74)

((Na watapelekwa wale ambao wamemcha Mola wao mpaka Peponi makundi makundi, mpaka wakishaifikia na ikafunguliwa milango yake na wakaambiwa na wasimamizi wake: Imani iwe kwenu, ubora mkubwa kwenu basi iingieni mubakie milele * na watasema: "Sifa zote njema ni kwa Allah ambaye ametusadikia ahadi yake na ameturithisha Ardhi tunakaa katika Pepo tunapotaka" Na ubora ulioje wa malipo ya wtendao mema)) [Zumar 73-74]

Kupitia Aya hizi tukufu inabainika wazi kuwa Pepo itakua ni Ardhini baada ya kubadilishwa wala si mbinguni kama wanavyoadai wenye kudai, na hakuna mkweli zaidi kuliko Allah mtukufu, wala hajatwambia kuwa waja wema watakau ni wakazi wa mbinguni, bali neno lake liko wazi kabisa:

مِنْهَا خَلَقْنَاكُمْ وَفِيهَا نُعِيدُكُمْ وَمِنْهَا نُخْرِجُكُمْ تَارَةً أُخْرَىٰ (55)

((Kutokana na hiyo (Ardhi) tumekuumbeni, na ndani ya hiyo (Ardhi) tunakurejeshini, na kutoka humu (Ardhini) tutakutoeni mara nyengine)) [Taha 55]

Haya ndiyo yaliyodhihiri kwetu kupitia Kitabu cha Allah mtukufu.

Na Allah ndiye anajua zaidi.

Wabillahi Taufiqi.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment