Ibadhi.com

54. NI LIPI KUNDI LILILO ONGOKA?

Asalamu alaykum wa barakatuh

Naam ndugu zangu nauliza, jee! nyinyi IBADHI mnalichukulia kuwa ni lipi lile kundi lililo ongoka kati ya yale 73 au kwenu hamukuipokea HADITHI hii?

JAWABU:

Hadithi ya kugawika umma wa Kiislamu makundi 73 imethibiti kwetu, ameipokea Imam Rabii bin Habib Allah amrehemu, kutoka kwa Sheikh wake Imam Abu Ubaidah Allah amrehemu, naye kaipokea kutoka kwa Sheikh wake Imam Jabir bin Zaid Allah amridhie, naye kaipokea kutoka kwa Sheikh wake Sahaba Abdullahi bin Abbaas Allah amridhie, naye kaieleza katika maneno ya Mtukufu wa Daraja Mtume Muhammad S.A.W. 

"سَتَفْتَرِقُ أُمَّتِي عَلَى ثَلاَثٍ وَسَبْعِينَ فِرْقَةً كُلُّهُمْ إِلَى النَّارِ مَا خَلاَ وَاحِدَةً نَاجِيَةٌ، وَكُلُّهُمْ يَدَّعِي تِلْكَ الْوَاحِدَةَ"

"Utagawika umati wangu katika makundi sabiini na tatu, wote wataingia motoni isipokua moja litaokoka, na kila moja litadai kuwa ndilo hilo moja (litakalo okoka)."

Na ukahika wa kuwa moja tu ndilo litakalo okoka umekuja katika Quraani tukufu, amesema Allah mtukufu:

((وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا)) 

((Na yoyote atakayepingana na Mtume baada ya kubainikiwa na uongofu na akafuata siyokua njia ya Waumini tutamuelekeza atakakoelekea na tutamfikisha jahannamu nayo ni mafikio mabaya sana.)) [Annisaa 115]

Na amesema:

((فَمَاذَا بَعْدَ الْحَقِّ إِلَّا الضَّلَالُ))

((Basi kuna kipi baada ya haki isipokua upotevu tu)) [Yunus 32].

Kwa hiyo njia ya Waumini ni moja tu, nayo ndiyo njia ya uongofu uliosimama kwa mabainisho ya haki kwa dalili, nayo ndiyo haki ambayo kutafautiana nayo baada ya kubainikiwa na uongofu wake kutakua ni upotevu bila shaka yoyote. 

Na sisi tunasema: Kwa mujibu wa ilivyodhihiri kwetu ni kuwa njia hiyo -katika yale ambayo Waislamu wametafautiana ndani yake na ambayo ni lazima haki iwe kwa upande mmoja tu bila mwengine- ni ile waliyopo Waislamu wa Madhehebu ya IBADHI katika mafundisho yao, wala hatuna shaka katika hili, basi imetudhihirikia kuwa kila mwenye kutafuatina na ITIKADI YA IBADHI baada ya kubainikiwa na uhaki wake huyo atakua anafuata njia isiyokua ya waumini na atakua katika batili bila shaka yoyote, na lau ingalidhihirika kwetu kuwepo ITIKADI ya Madhehebu nyengine isiyokua IBADHI kuwa ndiyo haki basi tusingaliridhia nafsi zetu kuwa kuni za Jahannamu.

Na kuhusisha kwetu ITIKADI bila FIQHI hakumaanishi kuwa FIQHI yake ni dhaifu au batili, lakini kunamaanisha kuwa ITIKADI ndio asili ambayo migawiko ya msingi ya kupotezana baina ya Madhehebu tafauti imepatikana ndani yake, ama FIQHI uwanja wake ni mpana, na ndani yake kuna wasaa mkubwa wa kutafautiana.

Na sababu za kuwa IBADHI ndiyo haki na njia ya waumini ni:

1. Kushikamana uwepo wake kizazi kwa kizazi katika kila karne bila kukatika kuanzia karne ya mwanzo mpaka hivi leo.

2. Kujishika kwake vizuri na Kitabu ch Allah (Quraani Tukufu) na Sunna ya Mtume Muhammad S.A.W.

3. Kutokubali kupingana na Quraani tukufu kwa hali zote.

4. Kusalimika kwake na itikadi pofu -au mfano wake- ambazo Allah amezieleza kuwepo kwa umma zilizopita katika Kitabu chake.

5. Kusalimika kwake na wimbi la kupendelea Madhalimu waovu waliojitosa katika bahari ya kumuasi Allah mtukufu, si kwa kuwapa matarijio bila kutubia wala kukubali kushiriki katika dhulma zao ikitokezea wao kuhukumu jamii kiutawala.

6. Kuwepo kwake katika nafasi yenye usalama katika yale yaliyoingiwa na tafuati za Kimadhehebu.

7. Kutoinyima Akili haki yake kwa kuheshimu malazimisho yake katika kukubali yanayolazimika kiakili na kukataa yasiyowezekana kiakili. 

8. Kuheshimu tafauti inapotokezea bila kutumia ubabe na fujo bali dalili ndizo pekee zitakazobainisha haki.

9. Kukubali kwake haki kwa asiyekua Muibadhi iwapo itathibiti kwa dalili kuwa ni haki.

Wabillahi Taufiiqi.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment