Ibadhi.com

53. KUTOMUONA ALLAH MTUKUFU NA VIZITO VIWILI

Asalamu alaykum

Suali La Kwanza:

Ningependa kufahamu nyinyi IBADHI mnaitakidi kwamba ALLAH MTUKUFU hayuko mbinguni.

Je! NABII MTUKUFU (s.a.w.w) alipoenda israa na miiraj kukabidhiwa SWALAA si dalili ya kua ALLAH yuko huko au vipi ?

Suali la pili:

Kuna hii Hadithi ambayo imepokelewa SUNI na SHIA ya VIZITO VIWILI. Kwamba Nabii (s.a.w w) katika HIJA ya kuaga aliusia kwamba viwili hivyo watu washikana navyo kuwa hawatapotea milele.

Suni wanasema Quran na suna, Shia wanasema Quran na Ahlulbayt.

Je nyinyi IBADHI mmeipokea vipi ? ! Nakama Ahlilbayt wapo Maifafanua vipi ndugu ?

JAWABU:

Waalaykum salam wa rahmatullahi wa batakatuh.

Maibadhi hatumdhibiti Allah kwa sehemu, si mbinguni wala ardhini wala popote, kwa sababu yeye si kiumbe wala hasifiki kwa lenye lazimisho la kuhitajia, neno letu kuhusu uwepo wa Allah ni kuwa uwepo wake umejitegemea kidhati, kwa hiyo uwepo wa viumbe na ukosekanaji wa viumbe hauathiri chochote kwa Allah mtukufu; kwa sababu yeye ndiye wa Mwanzo kabla ya viumbe vyote ambavyo ni sehemu na wakati na viathiriwa vya sehemu na wakati.

Allah si dhatimwili; kwa hiyo sisi tumtakasa na malazimisho ya mwili, hatumuulizii kwa wapi, wala nje, wala ndani, wala kuunganyika, wala kutengana, neno letu tunasema: Uwepo wa sehemu na ukosekanaji wa sehemu ni sawa mbele ya Allah.

Ama suala la Israa na Miiraji halikua kwa ajili ya kuonana na dhati ya Allah mtukufu, bali ni kama ilivyoelezwa wazi wazi katika Quraani kuwa ni kuona ishara kuu za Allah mtukufu, kwa hiyo haina maana ya kuwa Mtume s.a.w. alikwenda pahala ambapo Mungu yupo -haasha lillaahi- ametakasika Allah na uwepo wa ndani ya sehemu.

Ama suala la vizito viwili.

Imekuja katika Musnad Imaam Rabii bin Habiib Allah amrehemu:

Abu ‘Ubaydah kasema, “Imenifikia kutoka kwa Mjumbe wa Allah (S.A.W.) ya kwamba, kasema:

«خَلَّفْتُ فِيكُمْ مَا إِنْ تَمَسَّكْتُمْ بِهِ لَنْ تَضِلُّوا أَبَدًا كِتَابَ اللَّه عَزَّ وَجَلَّ فَمَا لَمْ تَجِدُوهُ فِي كِتَابِ اللَّهِ فَفِي سُنَّتِي، فَمَا لَمْ تَجِدُوهُ فِي سُنَّتِي، فَإِلَى أُوْلِي الأَمْرِ مِنْكُمْ».

"Nimewaachieni ambacho ikiwa mtashikamana nacho hamtapotea kamwe, Kitabu cha Allah Mtukufu, na msichokiona katika Kitabu cha Allah, basi katika Sunna yangu (na ikiwa pia) hamkuona kwenye Sunna yangu, (basi angalieni) kwa wasimamizi wa mambo yenu (Maulamaa na Viongozi waadilifu)”.

Pia imekuja Riwaya ya pili:

Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Ibn Abbas (R.A.A.), kutoka kwa Mtume wa Allah (S.A.W.) kasema:

«إِنَّكُمْ سَتَخْتَلِفُونَ مِنْ بَعْدِي فَمَا جَاءَكُمْ عَنِّي فَاعْرِضُوهُ عَلَى كِتَابِ اللَّهِ فَمَا وَافَقَهُ فَعَنِّي وَمَا خَالَفَهُ فَلَيْسَ عَنِّي».

“Hakika nyinyi mtatofautiana (mtakhitilafiana) baada yangu, (basi) kitakachokujieni kutoka kwangu (Hadithi  na Athari zilizoegemezwa kwa Mtume wa Allah (S.A.W.) ) kilinganisheni na kitabu cha Allah, kile kitakachowafikiana nacho, basi kimetoka kwangu, na kile kitakachokwenda kinyume nacho, basi hakitokani na mimi”.

Hizi ndizo riwaya zetu katika maudhui hii.

Zinduka kuwa Kuna kile ambacho hakipingani wala hakikubaliani, hicho tunahakilisha kwa kuchunguza sanadi yake na matni yake.

Na haya tuliyojishika nayo ndiyo yanayokubaliana na Kitabu cha Allah mtukufu katika neno lake:

﴿يا أَيُّهَا الَّذينَ آمَنوا أَطيعُوا اللَّهَ وَأَطيعُوا الرَّسولَ وَأُولِي الأَمرِ مِنكُم فَإِن تَنازَعتُم في شَيءٍ فَرُدّوهُ إِلَى اللَّهِ وَالرَّسولِ إِن كُنتُم تُؤمِنونَ بِاللَّهِ وَاليَومِ الآخِرِ ذلِكَ خَيرٌ وَأَحسَنُ تَأويلًا﴾ [An-Nisâ': 59] 

Enyi mlio amini! mt'iini Allah, na mt'iini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi. Na mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Mwenyezi Mungu na Mtume, ikiwa mnamuamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho. Hayo ndiyo bora zaidi na ndiyo yenye mwisho mwema.

Wabillaahi taufiiqi.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment