Ibadhi.com

49. MASUALI YA MSALAFI

1. Tunakubaliana kuwa Allah mtukufu ni mkalimifu asiyefikiwa na upungufu, na Allah mtukufu amejisifu kuwa ni msemaji, naye ameongea na viumbe vyake hata Iblisi aliongea nae, sasa hii Quraani ambayo ni maneno ya Allah Allah aliiumba wapi ndani ya dhati yake au nje ya thati yake? Ikiwa ndani ya dhati yake italazimika kuwa dhati yake amechukua viumbe ndani yake na hiyo ni kasoro ya kuchanganyika na viumbe, kwa sababu yeye ndiye aliyeisema na kwa vile ameisema itakua yeye imemtoka, na kama hakuiumba ndani ya dhati yake italazimika iwe ni dhati iliyojitosheleza isiyokua dhati ya Allah mtukufu, na ikiwa ni hivo itakua ni nani aliyemwambia Mussa: "Nenda kwa firauna hakika amepinduka mipaka" na "Hakika mimi hasa ndiye Mola wako ninabudu mimi" kwani itakua Quraani ndiyo iliyozungumza sio Allah, tunaomba dalili kua Allah aliiumba Quraani pembeni.

JAWABU:

Allah ni mkamilifu asiyefikiwa na upungufu kwa sababu yeye ndiye wa mwanzo kabla ya kila kisichokua yeye, yeye Allah ndiye mkwasi asiyehitaji chochote, na sisi waja akili zetu haziwezi kufikiri nje ya mipaka ya sehemu (fasi) na wakati, basi hatuwezi kabisa kumpata Allah kwa akili zetu kwa sababu yeye Allah mtukufu ndiye aliyeumba sehemu (nafasi) na wakati na vilivyomo ndani yake, kwa hiyo hatumsifu kwa umbo wala mwili, kutokana na hapo inabatilika kuuliza jee Quraani ilikua ndani ya Allah au nje ya Allah? Kwa sababu hakina ndani na nje isipokua chenye umbile kama mtu, na Allah ametakasika na hilo.

Ama Quraani tukufu Allah mwenyewe ametueleza kuwa imo katika ubao uliohifadhiwa (Lauhin Mahfuudh) pia katika (Kitaabun Maknuun) pia katika (Vifua vya waliopewa elimu) kwa hiyo hizo ndizo sehemu zake ambazo Allah ameiumba humo, na hakiingii ndani ya kiumbe isipokua kiumbe tu.

Ama kuhusu maneno aliyoambiwa Mtume Mussa S.A.W. udhahiri wake ni kuwa Mtume Mussa A.S. alifikiwa na maneno aliyotaka Allah ayasikie kwa njia sauti moja kwa moja naye alisikia alitotaka Allah.

Hakika Allah si kitu cha kutokwa na vitu, Allah hazai wala hatokwi na kitu wala haingiwi na kitu, Allah si mwili, shani yake Allah ni atakapo tu kitu kuwa hapo hapo kitu hicho huwa kama alivotaka (kun fayakuun), na huo ndio uumbaji wake, ama sauti na maneno aliyosikia Mussa kwa hakika vyote ni viumbe vya Allah, na kwa vile ni maneno aliyoyaanzisha Allah mtukufu mwenyewe akwa Allah ndiye msemaji na yakawa maneno ni yake, basi kuanzisha kwake maneno ndio usemaji wake Allah mtukufu, ni sawa kwa sauti au ilhamu au muandiko.

Na kama tutakadiria tu kuwa Quraani ndiyo iliyomwambia Mussa A.S. basi maneno ni ya mwanzilishi wake si ya mfikishaji wake, na sisi tunakubaliana kuwa Quraani ni maneno ya Allah, kwa hiyo alisikia maneno ya Allah wala si maneno ya Quraani wala maneno ya maneno.

Na ikiwa fikra ya muulizaji ni kuwa maneno ya Allah si kiumbe kwa sababu imesemwa na Allah, na kwa vile imesemwa na Allah itakua ni maneno yaliyotoka ndani ya dhati yake na kuja nje (astaghfirullahi), basi pia Allah mtukufu aliipuliza roho kwa Baba yetu Adamu A.S. ambaye ndiye jinsi ya watu wote; kwa hiyo vile vile roho za waja hazitakua viumbe; kwa sababu Roho imepulizwa na Allah; na kwa vile ameipuliza -kwa fikra ya muulizaji- italazimika kuwa ilikua ndani ya dhati yake na kuja nje ya dhati hiyo, na sisi hatujui mada ya roho aslan, ama mada ya Quraani tunaijua bila shaka yoyote kuwa ni lugha ya kiarabu ambayo ni kiumbe bila shaka yoyote.

 

2. Allah amtukufu ametueleza kuwa yeye anapotaka kitu hukiambia ((kun)) na hapo hapo kinakua, na neno hilo ((kun)) ni moja ya maneno ya Quraani, kwa hiyo neno la kusema kuwa Quraani ni kiumbe litalazimisha kuwa hiyo ((kun)) nayo alipata ((kun)) yake na hiyo ((kun)) vile vile na hapo italzimika kupatikana mtiririko usiokua na mwanzo, au ibatilike kuwa Allah kaumba kwa ((kun)) au ibatilike kauli ya kusema Quraani ni kiumbe.

JAWABU: 

Neno ((kun)) ni kiumbe kwa dalili huwezi kutamka ((n)) kabla ya kutamka ((ku)) na umri wa kila herufi unaanza kwa kuanza kutamkwa na kumalizika kutamkwa, kwa hiyo hakuna shaka kuwa neno ((kun)) ni kiumbe, nalo ni neno la lugha ya kiarabu ambayo ni kiumbe, hili halina shaka yoyote.

Kwa hiyo maelezo ya Aya tukufu yana kusudio yale, nalo ni amri ya Allah ya kupatisha viumbe, amri hiyo si neno ya kutamkwa kwa sauti na herufi, bali ni kutaka tu Allah kufanyika alichotaka kifanyike huko ndiko kulikoelezwa kwa (kun) na kufanyika kile alichotaka kifanyike kama alivotaka kifanyike ndio (yakuunu) hiyo ni lugha ya kinaaya kwa kuelezea hali si zaidi ya hapo.

Na amri hiyo huitwa amri tanjizii (amripatisha) ukitaka kupata taswira yake tazama ukichomwa sindano kwa ghafla unafanya nini? Ikiwa utashituka au utapiga kelele au utaguna au utafumba macho au utatokwa na machozi, hizo amri za kufanya hivo hata ukafanya zimetoka wapi? Ubongo ndio uliotoa amri hizo lakini si kwa herufi wala sauti, na utekelezaji unatimia kwa kasi kubwa ya ajabu, huo ndio ukaribisho tu wa kuweza kujua amri tanjizii (amripatisha). 

 Wallahu aalamu wa ahkamu.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment