Ibadhi.com

48. NI IPI KHIYANA YA MKE WA MTUME NUHU A.S.?

Asalamu alaykum.

Mtume Nuhu A.S. alipomuomba Allah kwa kusema: "Ewe Mola wangu hakika mtoto wangu ni katika Ahali zangu, na hakika ahadi yako ni haki, na wewe ndiye mwenye hukumu bora kuliko wahukumuji wote" alijibiwa: "Ewe Nuhu hakika huyo si katika Ahali zako, hakika yeye ni tendo sililo jema, na usiniombe usiyo kua na elimu nayo....." Suuratu Huud 46. wakati huo huo Allah anamueleza Mke wa Mtume Nuhu na Mke wa Mtume Luti kuwa waliwafanyia khiyana waume zao. Suuratu Tahriim.

Tumesikia kuwa mtoto yule alipatikana kwa khiyana yaani hatokani na kizazi cha Mtume Nuhu A.S. bali mama yake alifanya khiyana ya uzinifu hali ya kuwa ni mke wa Mtume wa Allah na ndio maana Allah akamkatalia Mtume Nuhu kuwa mtoto huyo ni katika Ahali zake.

Tunaomba ufafanuzi.

JAWABU:

Ubaya ulioje wa kusema kuwa mtoto wa Mtume Nuhu hakua mwanawe halali bali ni tunda la uzinifu kwa khiyana ya kindoa, wenye kusema hilo wako mbali na haki na uhakika, na haki wameikosea, kwa hakika Allah anaeleza kwenye kitabu chake wazi wazi:

وَنَادَىٰ نُوحٌ ابْنَهُ وَكَانَ فِي مَعْزِلٍ يَا بُنَيَّ ارْكَب مَّعَنَا وَلَا تَكُن مَّعَ الْكَافِرِينَ

((Na Nuhu alimwita mwanawe akiwa yuko mbali naye, ewe kitoto changu panda pamoja nasi na usiwe pamoja na Makafiri)) [Huud 42] 

Allah anatuambia kuwa Mtume Nuhu A.S. alimwita mwanawe, halafu atujie mtu atuambie laa hakua mwanawe tumkubalie? Kallaa kisha Kallaa, alikua ni mwana wa Mtume Nuhu A.S. wala hakua tunda la uzinifu wa nje ya ndoa kama wanavodai wabatilifu, wala hakuna shaka katika hili.

Ama kuelezwa Mke wa Mtume Nuhu kuwa alimkhuni Mtume wa Allah hali ya kuwa ndiye mumewe, hiyo si khiyana ya ndoa bali ni khiyana ya Imani kwa unafiki, anasema Imam Qutbu

"(فخانتاهما) بإضمار الشرك وإعانة أهله." اهــ

Waliwafanyia khiyana kwa kuficha ushirikina na kusaidia wahusika wake. [Taisiiru Tafsiir] 

Allah mtukufu ndiye aliyemwambia Mtume wake Nuhu A.S.:

وَأُوحِيَ إِلَىٰ نُوحٍ أَنَّهُ لَن يُؤْمِنَ مِن قَوْمِكَ إِلَّا مَن قَدْ آمَنَ فَلَا تَبْتَئِسْ بِمَا كَانُوا يَفْعَلُونَ * وَاصْنَعِ الْفُلْكَ بِأَعْيُنِنَا وَوَحْيِنَا وَلَا تُخَاطِبْنِي فِي الَّذِينَ ظَلَمُوا ۚ إِنَّهُم مُّغْرَقُونَ (37)

((Na Nuhu alipewa wahyi: Hakika yalivyo hasa hataamini katika kaumu yako isipokua ambae ameshaamini, basi usihuzunike kwa waliyokua wakiyafanya * na tengeneza jahazi kwa hifadhi yetu na uongozi wetu, wala usinikhutubie kuhusu ambao wamedhulumu, hakika hao ni wenye kuzamishwa)) [Huud 36-37]

Kwa hiyo Allah ametueleza wazi kabisa kuwa walioangamizwa kwa Tufani ni wale waliodhulumu, na mtoto wa uzinifu habebeshwi kosa la mama yake, dhulma ni ya mama yake si ya mtoto, basi vipi isemwe kuwa aliangamizwa kwa sababu hakua mtoto halali wa Mtume Nuhu A.S.?!! Hali ya kuwa Allah mtukufu ameshamuambia Mtume wake A.S.

قُلْنَا احْمِلْ فِيهَا مِن كُلٍّ زَوْجَيْنِ اثْنَيْنِ وَأَهْلَكَ إِلَّا مَن سَبَقَ عَلَيْهِ الْقَوْلُ

((Tukasema: Chukua ndani yake (hiyo jahazi) katika kila (wanyama) pea wawili na ahali zako isipokua ambae neno limeshamtangulia)) [Huud 40].

Kutanguliwa na neno, yaani hukumu ya kuangamizwa na kuwa si katika ahali zake watakaokoa, nalo liko wazi kuwa katika ahali zake wako waliovuliwa katika hukumu ya kuokoka, na hao bila shaka ni Mke wake na Mwanawe huyo Allah awalaani.

Kwa hiyo neno lake Allah mtukufu 

قَالَ يَا نُوحُ إِنَّهُ لَيْسَ مِنْ أَهْلِكَ ۖ إِنَّهُ عَمَلٌ غَيْرُ صَالِحٍ

((Alisema (Allah): Ewe Nuhu hakika huyo si katika Ahali zako, hakika hasa ni tendo lisilo jema)) [Huud 46]

Aya hii imekuja katika kisomo chengine

إِنَّهُ عَمِلَ غَيْرَ صَالِحٍ

((Hakika yeye alitenda lisilo jema.))

Na hiyo iliyotajwa hasa ndiyo sababu ya kuangamizwa kwake na kuvuliwa katika hukumu ya Ahali wa Mtume wa Allah S.A.W. hata kama ni Mtoto wake halali lakini kujitoa kwake nje ya utiifu kumemvua katika hukumu, na hapo tunapata fundisho kubwa sana kuwa asiyekuwemo katika njia ya uchamungu ni mwenye kuangamia tu hata kama atakua ni mtoto wa Mtume.

Imekuja katika hadithi sahihi: ((Na ambae atacheleshwa na matendo yake, hatatangulizwa na nasabu yake)).

Na imesemwa kuwa kosa la Mwana huyo wa Mtume Nuhu lilikua ni kukataa amri ya kupanda Jahazi, kwa hiyo iliposemwa kuwa ni tendo lisilo jema yaani lile alilokaidika ndani yake, na katika kisomo "alitenda lisilo jema" iko wazi kabisa.

Wabillahi Taufiiq

Wallaahu Aalamu.

 

 

 

 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment