Ibadhi.com

47. JEE! QURAANI IMEBADILISHWA?

SUALI:

Asalam alaikum warahmatullah wabarakatuh.

Kwanza natoa shukran za dhati kwa uongozi mzima wa ukumbi huu wa www.ibadhi.com kwa elimu kubwa tunayoipata kwa wakati wake MashaaAllah.

Siku ya jana nilipokea ujumbe uliotoka kwa mshia mmoja aliyeko Iran ambao una anuani UTHIBITISHO KATIKA VITABU VYA KISHIA KUWA QURAAN HII TULIONAYO IMEBADILISHWA NA INA MAPUNGUFU.

Basi tumeona dharura ya kuuliza ni kweli kuwa Quraani imebadilishwa kama inavodaiwa?

JAWABU:

Tunashukuru sana kupata ujumbe wako unaodhamini suali kupitia utata uliofikishwa kwenu kutoka kwa Mashia, Allah atuhifadhi na shari za wabatilifu wote.

Katika mambo ya lazima kuyaamini ni kuwa hakuna mkweli zaidi kuliko Allah mtukufu, na katika hilo zimekuja Aya mbili katika Quraani tukufu katika Suuratu Nisaa ya 87 na 122, na ukianza tu kusoma Quraani Aya ya pili ya sura ya pili inasema:

ذَٰلِكَ الْكِتَابُ لَا رَيْبَ ۛ فِيهِ ۛ هُدًى لِّلْمُتَّقِينَ

((Hicho ni Kitabu hakuna shaka ndani yake ni uongofu kwa Wachamungu)) [Baqarah 2]

na Kitabu maana yake ni kilichoandikwa, kwa hiyo Allah mtukufu alimteremshia Mtume wetu S.A.W. Kitabu kiitwacho Quraani, na muhali kuwa Quraani haikuandikwa katika uhai wa Mtume S.A.W. kwa sababu hakiwi Kitabu bila ya kuandikwa na kusomwa, na katika kusomwa ndio kikaitwa Quraani yaani ni chenye kusomwa sana bila nafsi kushiba kisomo chake.

Kwa hiyo fikra ya kuwa Quraani ilikusanywa na kuandikwa katika zama za Khalifa wa Tatu Othman bin Affaan, kwetu sisi fikra hiyo haipo, bali tunaona alichokifanya Othman ni kukataa misahafu iliyoongozewa tafsiri, na kulazimisha Msahafu kubakia katika andiko lake la asili kama ilivyoteremshwa, si zaidi ya hapo, nalo ni jambo zuri bila shaka yoyote.

Allah mtukufu katika Quraani anatuambia:

إِنَّا نَحْنُ نَزَّلْنَا الذِّكْرَ وَإِنَّا لَهُ لَحَافِظُونَ

((Hakika sisi hasa ndio tulioteremsha ukumbusho na hakika sisi hasa ndio wenye kuuhifadhi)) [Al Hijri 9].

Amepokea Imam Rabii bin Habib -Allah amridhie- katika Musnad kuwa Imam Abu Ubaidah -Allah mridhie- alisema: Imenifikia kuwa Mtume S.A.W. alikua ikimteremkia Aya anasema:

«اِجْعَلُوهَا فِي سُورَةِ كَذَا وَكَذَا وَفِي مَوْضِعِ كَذَا» وَمَا تُوُفِّيَ رَسُوْلُ اللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِلاَّ وَالقُرْآنُ مَجْمُوْعٌ مَتْلُوٌّ.

((Iwekeni katika sura kadha na kadha, au katika sehemu kadha wa kadha)) na hakufa Mtume wa Allah ila baada ya kuwa Quraani yote imeshakusanywa na inasomwa. [Rabii 15].

Na katika nuskha nyengine ya riwaya hii imekuja kuwa Mtume S.A.W. alikua akisema: ((Iwekeni katika sura kadha katika sehemu kadha)).

Kwa hiyo hakuna shaka kuwa Msahafu huu tulionao leo ndio Quraani ile ile iliyoteremshwa kwa Mtume wetu S.A.W. bila kupungua kitu wala kuongezeka kitu, kilichofanyika katika mikono ya Waislamu ni uboreshaji wa kuweka alama za kudhibiti maneno yake na visomo vyake tu, nayo ni sharafu kubwa inayohakikisha kuhifadhiwa Quraani tukufu kama alivoahidi Allah mtukufu, na miongoni mwa waliopata Sharafu hiyo ni Mwanachuoni Muomani Al-Khalil bin Ahmad Al-Farahidi Allah amridhie.

Basi kwa hakika Quraani hii ndiyo yenye makubaliano ya Umma wote kizazi kwa kizazi karne kwa karne tokea zama na Mtume wetu S.A.W. mpaka hivi leo na mpaka Kiama kitasimama.

Amepokea Imam Rabii bin Habiib katika Athari alizotolea Hoja kwa wapinzani wake kuwa Imam Jabir bin Zaid Allah amridhie alisema: Aliulizwa Ibnu Abbaas Allah amridhie, jee! Quraani imeongezwa au umepunguzwa? Naye akajibu kwa kusema: Amesema Mtume wa Allah S.A.W.: ((Allah amlaani mwenye kuongeza katika Kitabu cha Allah)) na akasema: ((Mwenye kuikana herufi moja ameikana Quraani yote)).

Amesema Imam Jabir bin Zaid Allah amridhie: Amesema Uqubah bin Aaamir Al-Juhani: "Alitusalisha Mtume wa Allah S.A.W. sala ya Alfajiri basi akasoma muawwadhataini (suuratu Al-Falaq na suuratu Nnaasi) basi alisema: ((Ewe Uqubah, hakika sura hizi mbili ni bora ya sura katika Quraani na Zaburi na Injili na Taurati)) na kuna watu wanasema kuwa sura hizo mbili si katika Quraani kwa hakika hao wamesema uongo na wameingia katika makosa.

Amesema Ibnu Abbaas Allah amridhie: "Lau kutakua na mtu aongeze ndani yake au apunguze basi mtu huyo atakua ni kafiri mbele ya Umma wote"

Na katika yenye kuhuzunisha sana ni kukutia katika vitabu tegemewa vya hadithi yenye kuonesha kuwa Quraani imechezewa kama ilivyo katika Sahihi Al-Bukhari na Muslim katika riwaya ya Alqamah kuwa alitakiwa na Sahaba Abu Dardaa -Allah amridhie- asome suuratu Allayli kama alivyoisikia kwa mwalimu wake Sahaba Abdullahi bin Massoud -Allah amridhie- basi Alqamah akasoma "Wallayli idhaa yaghshaa * wannahaari idhaa tajallaa * wadhakari wal-unthaa." Hapo Abu Dardaa akasema: Naapa wallwaahi namna hivi ndivyo nilivyoisikia kutoka katika mdomo wa Mtume wa Allah S.A.W. na hawa watu hapa wananitaka niisome: "Wamaa khalaqa dhakara wal-unthaa" wallwaahi siwafuati. Na riwaya hii imekaririwa katika Sahihi Bukhari na Muslim zaidi ya mara moja.

Pia imepokewa kuwa Sahaba Abdullahi bin Massoud -Allah amridhie- alikua akizikwarua Muawadhataini (Suuratu Al-Falaq na Suuratu Nnaasi) na akisema kuwa hizo mbili si katika Quraani.

Kwa hakika sisi tumtakasa Sahaba Abdullahi bin Massoud ambae Mtume S.A.W. alikua akitaka kusikiliza Quraani akimtaka Sahaba huyu amsomee Quraani, hata kufikia Mtume S.A.W. kusema: "Mwenye kutaka kusoma Quraani kama ilivyoteremshwa basi aisome kwa kisomo cha Ibnu Ummi Abdi" sisi tunamtakasa na hayo waliyomnasibisha nayo wabatilifu, kama tunavomtakasa na hayo Abu Dardaa -Allah amridhie-.  

Kwa ufupi, kwetu sisi hakuna fikra wala athari yoyote ya kuonesha kuwa Quraani imepunguzwa au imezidishwa au imechezewa, hata hukumu ya kurujumiwa mzinifu mume au mke kwetu sisi imethibiti kwa njia ya Sunna na si kwa njia ya Aya iliyofutwa kisomo chake na kubakia hukumu yake kama wanavyodai Masunni.

Wabillahi taufiqi.

Wallahu aalamu wa ahkamu.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment