Ibadhi.com

46. JEE! MAANA ZA MANENO YA ALLAH ZIMEUMBWA?

SUALI:

Asalaamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

Tulifuatilia mada ya Quraani ni kiumbe baina ya Sh. Abu Hamed Al Sawafi kwa upande wa Ibadhi na Masheikh kadhaa walioko U.K. Sh. Salim Khatib na Sh. Muhammad Awesi na Sh. Youssuf Anaufali kwa upande wa Sunni.

Tija ya mada hiyo ilifikia kuwa Quraani lafdhi ni kiumbe ama Quraani maana Sh. Abu Hamed Al Sawafi akasema ni kwa mujibu wa neno husika ikiwa mkusudiwa ni muumba basi si kiumbe ama ikiwa ni kiumbe basi ni kiumbe, ama Masheikh waliobaki walisema kuwa Quraani maana si kiumbe, lakini Sh Abu Hamed Al Sawafi alisema kuwa Quraani hiyo haipo na alitaka nakala za Wanavyuoni waliothibitisha Quraani maana, hapa aliletewa neno la Al-Imamu Saalimi akiwa amesema: "Vile vile maana (imeumbwa) usiwe na shaka." na yeye bila shaka ni moja katika Maimamu wakubwa katika Ibadhi.

Sasa Jee! Maana za maneno ya Allah pia zimeumbwa?

JAWABU:

Amesema Imamu Nuurudini Assaalimi Allah amrehemu katika Jauhari Nidhaami

والحــق ما قالت بـه الأعــلام * بأنـــــــه لـربـنــــــــا كــــــــلام
ووحيــه وأنــــه تنــزيلــــــــه * سبحـانـــه صــح لنــــا دليـلــــه
لكن أقول الأحرف الملحوظه * في الكتــب من ألسننا ملفـوظــه
بأنهـــا مخلوقـــــة للبـــــاري * قلت كـــذا المعـنى فلا تمـــاري
لأنهـــا مظــروفــة للأحـرف * وكل مظروف حدوث فاعـــرف
وذاك غيـــر علمـــه تعــــالى * وإن يكنــه يعلمــــه كمـــــــــالا
فالعلــم والمعلـوم ليــس واحدا * كالضرب والمضروب قد تباعدا
وأنــه فــي اللوح قطعا رسما * كذاك أيضا في صدور العلمـــا
وذاك مخلـوقــان هل تقـــول * يحــوي القديـم حــادث منـقــول

"Na haki ni yale waliyoyasema Maulamaa, ya kuwa Mola wetu anayo maneno, na wahyi wake, na kuwa huo ni uteremsho wake (Allah) aliyetakasika, na dalili yake imesihi kwetu. Lakini nasema: Herufi zinazotambulika katika vitabu vinazotamkwa na ndimi zetu, ya kuwa hizo ni viumbe vya Muumbaji, ninasema pia Maana (ni kiumbe) usiwe na shaka; kwa sababu ni vichukuzwi vya herufi, na kila kuchukuzwi kimetokeza utambue. Na hiyo sio elimu yake aliyetukuka, hata kama ni mwenye kuijua kiukamilifu, kwani kujua na kijulikanwacho si kitu kimoja, kama kupiga na kipigwacho ni viwili tafauti, na kwa hakika katika Lauhi -bila shaka- imeandikwa, vile vile katika vifua vya Maulamaa, na hivo viwili ni viumbe, jee! utasema kuwa cha tangu (kisichokiumbe) kimechukuliwa na kilichotokeza (kiumbe) chenye kuchukuliwa?."

Haya ndiyo maneno ya Imamu Assaalimi Allah amridhie, nayo hayana doa lolote, wala hayapingani na yaliyofafanuliwa katika mada husika, kwa sababu Imam Assaalimi katika beti zake hizi anatuambia kuwa Maneno ya Allah ni lafdhi na maana, na sio maana peke yake wala lafdhi peke yake, na maana sio kilichomaanishwa ambacho ndio kusudio, na dalili ni kuwa maana ni madhruufun yaani imechukuliwa na herufi zinazofanya neno, na kisichokua kiumbe hakichuliwi na kiumbe, kwa hiyo kilichomaanishwa kupitia hiyo maana aliyoizungumza Imam Saalimi Allah amridhie ndicho tulichokusudia kukieleza katika mada husika; ili kuwepesisha ufahamu kwa watu wa kawaida bila kuwapa uzito ndani yake, ama kiuhakika maana imechukuliwa na neno, nayo ndiyo inayobainisha kusudio; kwa hiyo neno na maana vyote ni viumbe ama kusudio ima litakua ni kiumbe au si kiumbe.

Wabillahi Taufiqi.

Wallahu Aalamu wa Ahkamu. 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment