Ibadhi.com

45. IMANI ZA MAJINA NA SIFA NA TAUHIDI RUBUBIYAH NA ULUHIYAH.

SUALI:

Asalamu Alaykum.

Jee! Kuna ufafanuzi wowote kuhusu hizi Imani za Asmaa wa Sifaati, Tauhidi Rububiyah na Uluuhiyah, tunataka kujua Imani hizi zina nafasi gani kwetu sisi Ibadhi?

Jazaakumu Allahu khairan.

JAWABU:

Masuala haya siku zote huwa ni tija ya ufafanuzi wa Wanavyuoni katika maandiko yao ili kuwepesisha ufahamu wake kwa wanafunzi na waumini wa kawaida, wameieleza Tauhidi kwa kuzingatia mambo mawili:-

La kwanza ni kuhitajia kila kiumbe kwa Muumba wake ambaye ni Allah mtukufu bila ya yeye kuhitajia chochote katika viumbe vyake, basi Allah mtukufu ndiye aliyepatisha kila kisichokua yeye, yaani kila kiumbe, na yeye Allah mtukufu ndiye mwenye kusimamia mamlaka yake, uumbaji ni wake na amri ya kuvitawala na kuvisimamia ni yake peke yake, na kwa kuzingatia upande huu anakua ndiye Rabbu na hapa inapatikana Tauhidi rububiyah.

Jambo la pili ni kuzingatia kustahiki kwake ibada za waja wake bila ya kushirikishwa na chengine chochote, na hapa ndipo inapopatikana Tauhidi uluuhiyah, yaani Tauhidi ya Uungu, na uhakika wa Uungu ni kuabudiwa, kwa hiyo, kama alivokua Allah mtukufu ni mpweke katika kupatisha viumbe na kuvisimamia vile vile ni mpweke katika kustahiki ibada za waja wake, hana mshirika katika yote mawili.

Ama Tauhidi na Asmaa wa Sifaati, hili wameliweka Masalafi ambao maarufu wanajulikana kwa jina la Mawahabi, nalo wameliweka ili kupitisha itikadi zao pofu za kumuitakidi Allah kuwa na sifa za viungo na harakati, na kuwakufurisha kwa kuwatoa nje ya Uislamu wale wote waliopingana na wao katika kumsifu Allah kwa sifa hizo za viungo na harakati nao wamewatungia jina ambalo Allah hakuliteremshia hoja wala dalili wamewaita Muattilah, uitaji wa bidaa hakuwahipo Mtume S.A.W. kufundisha uitaji huo.

Sisi hatuna shaka katika uhaki wa majina ya Allah mtukufu na kusifika Allah mtukufu lakini yote hayo elimu yake inapatikana katika Tauhidi Rububiyah na Tauhidi Uluuhiyah, bila ya hii ya Asmaau wa Sifaatu.

Wallahu Aaalamu wa ahakamu.

Wabillahi Taufiq. 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment