Ibadhi.com

21. VIPI MJA ATAONA UZITO WA CHEMBE WA JEMA NA BAYA?

Asalamu alaykum.

Nauliza suali ambalo ndugu yetu mmoja wa kisunni ametoa Aya za mwisho za Suuratu Zilazalah zenye kusema: ((Basi mwenye kufanya uzito wa tembe ya vyumbi wa kheri atauona * Na mwenye kufanya uzito wa tembe ya vumbi wa shari auaona)).

Hoja yake ni kuwa hii ni dalili ya wazi kuwa siku ya Kiama kutakuwa na Mizani na kutaadhibiwa watu kwa uzito wa yake makosa yao kidogo waliofanya baadae watatolewa watiwe Peponi kwa yale mengi mazuri yaliyopimwa na Mezani.

Jee!! Hii hoja inakubalika kwa dalili za Aya tukufu zilizotolewa?

JAWABU:

KWANZA: Kwa hakika Aya tukufu haijataja Mizani, wala haijaashiria kabisa kuwepo kwa mizani hiyo wanayodai Masunni kuwepo kwake siku ya Kiama, wala hakuna katika Quraani sehemu yoyote iliyotajwa Mizani ya kushindanisha mazuri na mabaya siku ya Kiama, pia hakuna katika Quraani sehemu inayobashiria mja wa motoni kutoka motoni, wala mja wa Peponi kuingia motoni.

PILI: Aya hizi za Suuratu Zilazalah zinatueleza kuwa kila mja ataona yote atakayoyatenda ikiwa ni mabaya au mema, hata jema au baya likiwa ni dogo namna gani basi ataliona, na haya ameyaeleza Allah mtukufu katika Aya nyengine pale alipotuambia:

وَوُضِعَ الْكِتَابُ فَتَرَى الْمُجْرِمِينَ مُشْفِقِينَ مِمَّا فِيهِ وَيَقُولُونَ يَا وَيْلَتَنَا مَالِ هَذَا الْكِتَابِ لَا يُغَادِرُ صَغِيرَةً وَلَا كَبِيرَةً إِلَّا أَحْصَاهَا وَوَجَدُوا مَا عَمِلُوا حَاضِرًا وَلَا يَظْلِمُ رَبُّكَ أَحَدًا (49)

((Na kitawekwa Kitabu, basi utawaona waovu wanahaha kwa yaliyomo ndani yake, na watasema: Ee ole wetu, kina nini Kitabu hichi?!! hakikuacha dogo wala kubwa ila kimelidhibiti!!, Na watakutia waliyoyafanya yamehudhuria na hadhalumu Mola wako yoyote))

[Kahaf 49]

Kwa hiyo Mchamungu ataona mema yake na mabaya yake, basi atafurahi furaha isiyokua na kifani kwa kukubaliwa mema yake na kusitiriwa kwa makosa yake aliyotubia kwayo; kwani atakua ameingia katika rehma za Allah mtukufu, anatuambia Allah mtukufu kupitia ndimi za Malaika wake wa karibu zaidi:

وَقِهِمُ السَّيِّئَاتِ وَمَنْ تَقِ السَّيِّئَاتِ يَوْمَئِذٍ فَقَدْ رَحِمْتَهُ وَذَلِكَ هُوَ الْفَوْزُ الْعَظِيمُ 

((Na uwakinge na makosa, na ambaye utamkinga na makosa siku hiyo (ya akhera) kwa hakika huyo umemrehemu, na huko ndiko kufaulu kukubwa))

[Ghaafir 9].

Ama muovu aliye fasiki ambaye yumo katika mwendo wa Ibilisi mlaaniwa wa kutotubia kwa dhambi anaijua mpaka mauti yakamfika, kwa hakika huyo ataona mema yake na maovu yake, lakini yeye atajawa na huzuni na majuto yasiyokuwa na mfano; kwani mema yake hayakukubaliwa kwa sababu ya ukaidi wa kutubia kwake katika dhambi kubwa iliyomzonga na hapo hali yake itakua kama alivyotueleza Allah mtukufu:

وَيَوْمَ يَعَضُّ الظَّالِمُ عَلَى يَدَيْهِ يَقُولُ يَا لَيْتَنِي اتَّخَذْتُ مَعَ الرَّسُولِ سَبِيلًا (27)يَا وَيْلَتَى لَيْتَنِي لَمْ أَتَّخِذْ فُلَانًا خَلِيلًا (28)لَقَدْ أَضَلَّنِي عَنِ الذِّكْرِ بَعْدَ إِذْ جَاءَنِي وَكَانَ الشَّيْطَانُ لِلْإِنْسَانِ خَذُولًا (29)

((Na siku atakapon`gata dhalimu mikono yake, atasema: Ee!! Laiti ningalifanya kuwa pamoja na Mtume ndio njia yangu * Ee!! Ole wangu, laiti nisingalimfanya fulani kuwa kipenzi changu * Kwa hakika amenipoteza nje ya ukumbusho baada ya kunifikia. Na akawa Shetani ni mwenye kumuacha mtu))

[Furqaan 27-29].

TATU: As-habu wetu (Ibadhi) wamechukua Itikadi yao moja kwa moja katika Quraani tukufu, basi amesema Imamu Qutubu Al-Aimah R.A kuhusu Aya hizo:

والمراد الجزاء القليل والكثير فرؤيته رؤية جزائه على حذف مضاف وذلك بحسب ما ختم عمله فالسعيد يرى ثواب علمه الصالح كله إذ لم يمت مصراً وسيئاته كلها محبطة ، والشقى يرى عقاب سيئاته كلها مبطلة بإصراره كأنه قيل خيراً يره إن لم يحبط وشراً يره إن لم يكفر

((Na Makusudio ni malipo kidogo na mingi, basi kuona kwake ni kuona malipo yake kwa njia ya kuondolewa mudhaafu, na hayo ni kwa mujibu wa aliyomalizia matendo yake, basi mwenye kufaulu ataona malipo ya matendo yake mema yote ikiwa hakufa akiwa ni mkaidi wa kutubia, basi ataona makosa yake yote yameporomoka hayakuzingatiwa. Na muovu ataona adabu ya maovu yake ya batili. Kama hapo imesemwa KHERI ATAIONA IKIWA HAIKUPOROMOKA, NA SHARI ATAIONA IKIWA HAIKUSITIRIWA)).

NNE: Kama tulivyosema kuwa katika Quraani hakuna sehemu iliyotaja kuwepo kwa Mizani ya kushindanisha mabaya na mazuri siku ya kiama, na Aya zote lizozokuja kuhusiana na suala la kipimo cha matendo ya waja zimekuja kwa mfumo wa ((Yule zitakaekua nzito mizani zake)) kwa wingi, na ((Yule zitakaekua nyepesi mizani zake)) kwa wingi vile vile, kwa maana hiyo mizani ni hizo hizo, ima zitakua nzito au zitakua nyepesi.

Bila shaka hizo ni mizani za matendo mema ya mja, kila tendo ima litakubaliwa au litakataliwa, lililokubaliwa ndilo limekua zito na lililokataliwa ndilo limekua jepesi, basi yule ambaye yatakubaliwa mema yake hata kama ni jema moja tu huyo imekua nzito mizani ya jema hilo, na huyo haguswi na moto asilani achilia mbali kutoka humo, na Allah ameshahukumu katika Kitabu chake kuwa yeye anawakubalia Wachamungu, na Pepo ameiandaa kwa ajili ya Wachamungu tu, amesema:

قَالَ إِنَّمَا يَتَقَبَّلُ اللَّهُ مِنَ الْمُتَّقِينَ (27)

((Hakika halivyo ni kuwa Allah anawakubalia wachamungu))

[Al Maaidah 27]

Ama aliye fasiki amejitosa katika asi analijua akawa ni mkaidi wa kutubia mpaka kifo kikamkutia huyo mema yake yamekosa sharti ya kukubaliwa nayo ni sharti hiyo ya uchamungu; kwa hiyo mizani za mema yake zimekua nyepesi, naye atazongwa na maovu yake hata kama ni ovu moja, na atasalia katika adhabu ya Jahannamu humo atabakia milele, na ukali wa adhabu yake humo ni kwa mujibu wa maovu yake.

Amesema Allah mtukufu:

فَمَنْ ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ (102) وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنْفُسَهُمْ فِي جَهَنَّمَ خَالِدُونَ (103)

((Basi yule ambaye mizani zake zitakua nzito hao ndio waliofaulu * Na yule ambaye mizani zake zitafifia hao ndo waliozihasiri nafsi zao katika jahannamu watabakia))

[Al Muuminuna 102-103]

TANO: Itikadi ya kusamehewa waovu wakaidi wa kutubia siku ya kiama au kuadhibiwa kwa muda au kuombewa na wakuu (Shafaa) bila shaka ni itikadi batili na maradhi mabaya ya kiitikadi yaliyowapata wana wa Israili ambao ni watoto wa Mitume kwani Israili ni Mtume ya Yaaquub A.S naye ni mwana wa Isihaqa A.S naye ni mwana wa Ibarahim A.S, lakini Wana wa Israili walioasi walilaaniwa kwa sababu ya uasi wao na uadui wao na udhalimu wao, na kwa hakika maradhi ni hayo hayo hata kama wangonjwa ni tafauti ugonjwa unabakia pale pale, basi tujihadhari nayo maradhi hayo na mengineo, kwani wao hali zao ni kama alivyozieleza Allah mtukufu:

فَخَلَفَ مِنْ بَعْدِهِمْ خَلْفٌ وَرِثُوا الْكِتَابَ يَأْخُذُونَ عَرَضَ هَذَا الْأَدْنَى وَيَقُولُونَ سَيُغْفَرُ لَنَا وَإِنْ يَأْتِهِمْ عَرَضٌ مِثْلُهُ يَأْخُذُوهُ

((Basi walifuatia baada yao waliofuatia, walirithi Kitabu wakachukua pato hili la chini na huku wanasema: TUTASAMEHEWA TU na ilikiwajia pato mfano wake wanalichukua...))

[Al Aaarafi 169]

Twabaan, Allah mtukufu amewatia aibu kwa Itikadi yao hiyo ya kuwa wao watasamehewa tu kwa kuasi kwao, nao ndio aliowasifu kuwa walirithi Kitabu chake... Jee!! Kama hawakusamehewa? Hapo wakazua Itikadi ya Adhabu ya Muda wakasema:

ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَنْ تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَعْدُودَاتٍ وَغَرَّهُمْ فِي دِينِهِمْ مَا كَانُوا يَفْتَرُونَ (24)

((Hayo ni kwa sababu wao wamesema: Hautatugusa moto isipokua siku chache. Na yakawadanganya katika dini yao waliyokua wakiyazua))

[Aala Imraana 24]

Pia walijipa matarajio hewa ya kuombewa siku ya kiama ikiwa hawakutubia, na kwa hakika uombezi ni kwa ajili ya waliotubia ambao amefuata mwendo wa wazazi wetu Adamu na Hawa A.S, na sio kwa waliojizonga na mwendo wa Ibilisi mlaaniwa wa kukaidika katika toba kwa makosa waliyoyaingia.

Wabillahi Taufiqi.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment