10. NI NANI MAKHAWARIJI?

Written by
SUALI

Aslamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh

Tunasikia sana tuhuma ya ukhawariji dhidi ya Ibadhi, tunataka kujua hasa hivi kweli Ibadhi ni katika makundi ya Kikhawariji? Na Ukhawariji ni nini hasa? Na nani Makhawariji?

JAWABU:

Waalaykum salam wa rahmatullahi wa barakatuhu.

Kwa hakika tuhuma ya ukhawariji dhidi ya Ibadhi imeanza mapema sana, hata kama tuhuma hii ni mbaya katika uhakika wake lakini imehakikisha ushahidi muhimu sana kwa upande wa Ibadhi, nao ni ushahidi wa ukweli na kujiepusha kwao na kila mwenye dhambi kubwa, na ushahidi huu umetoka kwa hao hao wanaoiona Ibadhi kuwa madhehebu ya Kikhawariji, mpaka ikafikia kusema kuwa haijulikani kwao wao mwenye kusema uongo, kutokana na hapo zikasalimika safu za Ibadhi kutokana na hadithi za uongo na kuongozewa, na likidhihiri hili basi Allah mtukufu ametuamrisha tuwe pamoja na walio wakweli.

Ama kuhusu Jee! Ibadhi ni miongoni mwa Makhawariji?

Tunasema kuwa ikiwa makusudio ya ukhawariji ni kutoka dhidi ya udhalimu na kutokubali kushiriki katika madhambi na uadui basi hiyo ni sifa njema asiiondoshe Allah kwa Ibadhi, ama ikiwa ukhawariji ni kutoka nje ya dini na kuiacha haki kama zilivyobashiria hadithi za Mtume (s.a.w) basi Ibadhi sio katika hao wala haiwezeni kuwa katika hao.

Na Ukhawariji mbaya na ulio hatari ni ule aliouleza Mtume (s.a.w) pale aliposema:

يَخْرُجُ فِيكُمْ قَوْمٌ تَحْقِرُونَ صَلاَتَكُمْ مَعَ صَلاَتِهِمْ، وَصِيَامَكُمْ مَعَ صِيَامِهِمْ، وَأَعْمَالَكُمْ مَعَ أَعْمَالِهِمْ، يَقْرَؤُونَ الْقُرْآنَ وَلاَ يُجَاوِزُ حَنَاجِرَهُمْ، يَمْرُقُونَ مِنَ الدِّينِ كَمَا يَمْرُقُ السَّهْمُ مِنَ الرَّمِيَّةِ

“Watatoka katika nyinyi watu mtazidharau Sala zenu mbele ya Sala zao, na funga zenu mbele ya funga zao, na vitendo vyenu (vyema) mbele vitendo vyao, wanasoma Qur`ani lakini haivuuki koo zao (haifiki Qur`ani katika mioyo yao), wanatoka katika dini mfano wa mshale unavyochopoka kwenye kiwindwa...." Rabii 36 Muwataa 694. Bukhari 5058.

Mtume (s.a.w) ametuambia kuwa Makhawariji waovu (Maariqah) sifa zao ni:

  1. Watakuwa wanajinasibisha na Uislamu nao wanatoka katika safu za Waislamu.
  2. Watakuwa ni wingi wa ibada kiasi cha kudharau ibada nyengine mbele ya ibada zao.
  3. Wanasoma Quraani.
  4. Quraani haivuuki koo zao.
  5. Wataihama dini mfano wa mkuki inavyokihama kiwindwa.

Katika ufafanuzi huu wa Mtume (s.a.w) tunapata kuwa Makhawariji watakuwa ni wingi wa ibada na wasomi wazuri wa Quraani, bila shaka hizi ni sifa nzuri na bora, kila muislamu anatakiwa ajipambe nazo, wala hakuna aibu katika sifa hizi, lakini amezitaja Mtume wetu (s.a.w) kwa njia ya kutuzindua, tusije tukahadaika na mazuri yao na dhahiri yao, kwani mazuri hayo hayatawafaa kitu kwa sababu ya sifa zao mbaya, nazo ni:

  1. Kutovuuka Quraani koo zao, na sifa hii inamaanisha kuwa itikadi yao itapingana na Quraani, wataipa Quraani tafsiri za kuvunja mafundisho yake.
  2. Kuihama dini ingawa watajinasibisha nayo, na hili linafasiriwa katika riwaya nyengine kuwa wao wataua waislamu na kuwaacha washirikina wanaoabudu masanamu kama ilivyo katik [Bukhari 3344, 7432 Muslim 1064]

Tukirejea katika matokeo ya kitarehe, tunakutia Makhawariji wa mwanzo walipatikana mwaka wa 64 Hijiria, na makundi yao yakawa maarufu kwa majina ya Azaariqah na Najidiyah na Sufriyah. Wao walitakidi kuwa kila aliyemo katika dhambi kubwa ni kafiri mshirkina ameritadi damu yake ni lazima kuimwaga na mali yake ni ngawira na watoto wake na wake zake ni mateka wa kuingizwa katika utumwa au kuuliwa, waliitakidi kuritadi kila asiyekubaliana na wao, na huu ndio ukhawariji kiuhakika.

Kwa hiyo Ukhawariji ni kuitakidi kuritadi kila asiyekubalina na Itikadi ya wenye kuiitakidi itikadi anayoitakidi Mkhawariji.

Kutokana na hapo tutafahamu kuwa madhehebu yoyote yenye mafundisho ya kuitikadi kuwa kila aliyetafautiana nayo kiitikadi katika waislamu huyo atakuwa ni kafiri mshirkina aliyeritadi hayo ndiyo Madhehebu ya Kikhawariji.

Na Mawahabi bila shaka ni makhawariji; kwani wao wanaona ulazima wa kumuua kila aliyetafautiana na wao katika masuala ya kiitikadi, utakutia Maimamu wao tegemewa wako mbele katika kukufurisha waislamu wengine ukafiri wa kuritadi na kuwatoa nje ya uislamu, hili ni maarufu kwao hususan katika mlango wanaouita asmaau wa sifaati, kila asiyekubaliana na wao katika kumuitakidi Allah mwenye viungo walivoviita sifa, Allah mwenye harakati za kuteremka na kukaa kitako huyo kwao ni muattilah, na muattilah kwa mujibu wa itikadi yao ni jahamia kafiri murtadi, kutokana na hapo shari yao katika umma wa kiislamu ni mbaya sana, na fitina zao ni korofi sana, inalazimika kujihadhari nao.

Baada ya haya tuliyoyaeleza tufahamu kuwa Makhawariji hata kama ni wapotevu wapotezaji bado wanahesabiwa kuwa katika safu za Waislamu wala hawahesabiwi kuwa ni washirkina wala kuwa wameritadi.

Amesema Ibnu Taimiyah Al-Harrani kuhisana na Makhawariji:

((Hakika yao (hao Makhawariji) hakukuana yoyote aliye shari zaidi kwa waislamu kuliko wao, si Mayahudi wala Manasara; kwani wao walikuwa ni wenye kujitahidi katika kuua kila muislamu asiyekubalina na wao, ni wenye kuhalalisha damu za waislamu na mali zao na kuua watoto wao, wakiwaona kuwa ni makafiri, walikuwa ni wenye kuliitakidi hilo kwa ukorofi mkuu wa ujinga wao, na bidaa yao yenye kupoteza. Pamoja na hayo, Masahaba (r.a) na Matabiina waliowafutia kwa wema hawakuwakufurisha (Makhawariji), wala hawakuwafanya wenye kuritadi, wala hawakuwafanyia uadui kwa neno wala kitendo, bali walimcha Allah kwao wao)) [Mihaaj Sunna 5/248].

Na maesema katika sehemu nyengine ya kitabu chake hicho kuhusu Makhawariji ((Na haukuacha mwendo wa Waislamu kuwa juu ya hili, hawakuwaona kuwa wameritadi))

Tumeleta neno la Shekhe huyu wa Kiwahabi ili liwe hoja kwao wao wenyewe, wajiepushe na sifa ya ukhawariji aliyoieleza Sheikh wao; kwani mazingatio ni maradhi sio tafauti ya wagonjwa, pia wakubali shahada ya Imamu wao waondokane na mwendo wa kuwakufurisha wanaowaona kuwa ni Khawariji nao ni Ibadhi kwa mujibu wa mtazamo wao, kwani salafu wema Masahaba na Matabiina (r.a) hawakuwakufurisha Makhawariji wala hawakuwaona kuwa wameritadi.

Wabillahi Taufiqi.

Read 6284 times
Sh. Hafidh Al-Sawafi

ibadhi.com | This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Add comment


FaLang translation system by Faboba