Ibadhi.com

5. SUALI KUHUSU KUJINASIBISHA NA IBADHI

Suali:

Asslamu alaykum.

Niulize Suali nilanolisumbua kidogo kwenye mawazo na ambalo sina hikima nalo hata kidogo.

Hii kujinasibu sisi na jina letu la Uibadhi hatukosei kweli kweli? Naogopa isije ikawa tumesukumika kijifanya kundi (sect) katika makundi ya dini kimakosa.

Jawabu:

Waalaykum salamu warahatullahi wabarakatuh.

Kwa hakika kujinabasibu kwetu na Ibadhi sio kosa, bali kiuhakika hilo limekuwa ni wajibu kwa sababu zifuatazo:

  1. Masheikh wetu waliotangulia tokea mwanzo -ingawa wao hawakutumia jina isipokuwa la Uislamu na Wanadaawa, na Wanaistiqamah, na Jaamatulmuslimina- hawakupinga kuitwa Ibadhi, na baada ya muda kupita walilikubali jina la Ibadhi bila ya kutofautiana ndani yake, nao ni hoja kwetu, basi makubaliano yao ni hoja kwetu.
  2. Kujiita Ibadhi hakubatilishi Uislamu wetu; kwa sababu Muibadhi ni Muislamu, kwa hiyo ni jina mahususi katika mjumuiko mkubwa, na Allah mtukufu aliwaita wema wa mwanzo wa umma huu kwa majina tofauti, aliwaita Maansari na Muhajirina, nazo bila shaka ni aina mbili za Masahaba (r.a) hali ya kuwa wote ni Waislamu wako chini ya kivuli cha Mtume (s.a.w).
  3. Lengo la kuitwa Ibadhi ni kupambanua fikra moja kutokana na fikra nyengine na Itikadi moja kutokana na nyengine katika yale yenye kutofautiana ndani yake, na sio kujitungia jina, kwani jina ni alama tu ya fikra, na hapa utagundua kuwa:
    1. Ibadhi ni anuani ya kuhifadhika mafundisho na kuwajuwa wahusika wake, na kuwa jina hili ni ngome ya kuhifadhika kwa kutojiingiza katika safu zetu asiyukuwa wa upande wetu, kuweza kuainisha yale yenye tofauti ndani yake, na hilo limetuhifadhi na uwezekano wa wengine kuharibu mafundisho na kuzua fitna katika safu setu. Kama hayo yanavyodhihiri hayo kwa wengine; kwani tunaona jinsi walivyoweza kuathiriwa na fikra za kiitikadi zisizokuwa zao na hata kufikia kupigwa vita kwa jina lao wenyewe.
    2. Ibadhi ni utambulisho wa mafundisho na misimamo katika yale yaliyoingiwa na tofauti ndani yake tu; kwa hiyo kujinasibu kwetu na Ibadhi ni kuhifadhika kutokana na majukumu ya wengine katika yenye tofauti ndani yake, na kupelekea hilo kuhusika kila upande na mizigo ya mafundisho yake. Leo tunaona jinsi vichwa vya watu vinavyokatwa na kucherengwa kama kuku, pia tunaona uharibifu unaofanywa katika miji ya waislamu, na yote hayo yanafanywa na wafanyaji wake kwa jina la Uislamu, lakini uhakika wake utabakia pale pale kuwa ni mazao ya mafundisho ya wahusika wake tu kwa mujibu wa madhehebu zao hata kama wao wanaamini kuwa wamo katika kuisimamisha Dini na kuwa ndio Uislamu; kwa hiyo kila chuo cha Madhehebu kihusike na mambo yake katika yenye tofauti ndani yake, pia kihusishwe na majukumu yake. Tunataraji hata ndugu yetu muulizaji anafahamu kuwa yeye anahusika kwa jina lake, na kuwa jina lake ni utambulisho wake, na hakubali kubandikwa yeye makosa ya wengine kwa kutumia jina lake.   

Tunasema, kuwa Ibadhi inakataa kubebeshwa makosa ya wengine, kwa hiyo kama kutakuwa na makosa -kwa wengine- yanayoathiri safu ya waislamu kwa ujumla, ni wajibu waelekewa hao wenye makosa na na sio watujie sisi na kutubebesha matatizo ya wengine.

Ndugu zangu Maibadhi tujuwe kuwa kubaguka Ibadhi na wengine ni kwa njia ya hao wengine kujipangia Madhehebu zao.

Sisi katika Ibadhi hatuna mafundisho ya chinjachinja wengine katika tuliyotofautiana nao, wala hatuna mafundisho ya kuwakana wengine katika Uislamu uliotukusanya sote, basi tunashirikiana na wengine katika yale ambayo Uislamu umetukusanya pamoja, na katika yenye tofauti kila upande uhusike na mambo yake pia uhusishwe na athari zake.

Na Ibadhi hata kama itadhulumiwa na wengine basi katu kaitodhulumu wengine, mifano:-

  1. Imam Twalibu Al-haqi Abdullahi bin Yahya Al-Kindi (r.a) aliishika Yemen katika mwaka 128 Hijiria kwa kufanya mapinduzi ya amani dhidi ya utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiitawala Yemen kidhulma na ujeuri, na miongoni mwa waliongia katika mikono yake ni Magavana wa Bani Ummayah wa miji ya San-aa na Aden, wallahi hakuwaua, wala hakuwadhuru, wala hakuhalalisha chochote katika nafsi zao wala mali zao, kubwa alilolifanya kwao ni kuwaweka kizuizini kwa muda wa siku chache kisha akawambia: "Hakika nimewaweka kizuizini kwa kuogopea maisha yenu kuwa hatarini kwa Raia wa kawaida, basi hivi sasa muna hiyari yenu ya kubakia au kuondoka". Nao wakahiyari kuondoka.
  2. Imam Abu Al-Khatwab Al-Maafiri (r.a) alipigana na waasi Khawariji Sufria Waafurjuumah na akawashinda vita waasi hao na kuuzima uasi wao na kuwanusuru wanye kudhulumiwa, hapo alimjia mmoja wa askari wake na kumwambia: ((Tuwafanyie hawa kama wao wanavotufanyia sisi pidi wakitushinda)) hapo Imam Al-Maafiri (r.a) alimjibu yule askari kwa kumwambia: "Basi itakuwa ni haki kwa Allah mtukufu kutuadhibu sisi kama atakavowaadhibu wao, na hapo tukawa pamoja nao kama alivyosema: ((Kila ukiingia umma huulani ndugu yake, mpaka wakishakutana humo wote, watasema wa mwisho wao kuwaambia wa manzo wao: Ewe Mola wetu, hawa walitupoteza basi wape adhabu ya Moto nyongeza mara mbili. Atasema: Kila mmoja ana maradufu yake lakini hamujui)) [Al-Aaraaf 38].

Na mifano ni mingi na kwa hii miwili tutosheke.

Wabillahi Taufiqi

Wallahu aalamu wa ahkam.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment