Ibadhi.com

3. ELIMU NA UJINGA

Elewa kuwa Allah mtukufu hailazimishi nafsi kwa kilicho nje ya uwezo wake, na kwa hiyo ubainisho wa haki ni njia la kulazimika mja kuitikia wito wa Muumba ambaye ni Allah mtukufu, na Allah mtukufu ametuambia katika Kitabu chake Kitukufu ((Na hatukua sisi ni wenye kuadhibu mpaka tupeleke Mtume)), basi tufahamu kuwa yaliyokamatana na Dini yetu tukufu yamegawika kwa upande wa Mja katika vigao viwili vikuu:

Cha mwanzo: Ni yale ambayo ujinga wake unapata nafasi ya kuzingatiwa, na hayo ni yale ambayo hoja ya kulazimika kwake haijasimama juu ya mja.

Cha pili: Ni yale ambayo ujinga wake hauna nafasi tena, na hayo ni yale ambayo hoja ya kulazimika kwake imeshasimama juu ya mja.

Na kwa maana hiyo tutajua umuhimu wa Dalili ambayo ndiyo Hoja ya Allah kwa waja wake, na kwa maana hiyo tufahamu kuwa haya ya kigao cha pili cha yasiyokubalika ujinga wake yamegawika sehehmu mbili:

 

1.  Yale ya Kiakili, na hayo ni yale ambayo yanapatikana maarifa yake kwa kutumia akili.

2.  Yale ya Kisheria, na hayo ni yale ambayo yanapatikana maarifa yale kwa kuisikia sheria ya Allah mtukufu.

 

Na kwa maana hiyo Dalili zimegawika vigao viwili:

1. Dalili za Kiakili

2. Dalili za Kunaliki (Andiko ya kusikiwa). 

Tukija katika kuyaangalia mambo kwa kuzingatia hukumu za dalili za Kiakili, kwa hakika tutagundua kuwa yamegawika vigao vitatu vikuu navyo ni:

1.Yaliyo ya lazima kiakili: Nayo ni yale ambayo haiwezekani kukosekana kwake kwa mujibu wa hukumu ya akili.

2.Yasiyowezekana kiakili: Nayo ni yale ambayo haiwezekani kupatikana kwake kwa mujibu wa hukumu ya akili.

3.Yanayofaa kupatikana au kukosekana kiakili: Nayo ni yale ambayo inawezekana kuwepo kwake na kukosekana kwake kwa mujibu wa hukumu ya akili.

Basi inamlazimikia Mja kuyathibitisha Kiitikadi yale yaliyo ya lazima Kiakili, kama ilivyokua inamlazimikia Mja kuyakanusha Kiitikadi yale yalisiyowezekana Kiakili.

ZINGATIO:

  Kuna tofauti baina ya yale yaliyokua ya lazima kiakili na yaliyokua ya lazima kimazoea, kama ilivyokua kuna tofauti baina ya yale yasiyowezekana kiakili na yale yasiyowezekana kimazoea.

Kwa mfano:

Mwili mmoja kuwa katika sehemu mbili totauti kwa wakati mmoja, hili haliwezekani Kiakili, ama kama kuungua mtu katika moto, au kupasuka bahari kwa mchapo wa bakora, au kurejea katika uhai aliyekufa, haya ni katika yasiyowezekana kimazoea ama kiakili yanawezekana, na hapo ndipo uwanja wa Miujiza ya Mitume (a.s.w) katika kusadikisha uhaki wa risala zao.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment