Ibadhi.com

15. KUTOKANA NA IHRAMU YA HIJA

 

—  Akimaliza mwenye kuhiji siku ya kuchinja (10 Dhulhija) kupiga jamra na kuchinja atatokana na ihramu yake kwa kunyoa au kupunguza nywele. Dalili ya hayo ni hadithi ya Anas “kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehma za Allah na amani zimshukie - alifika Mina akaja kwenye Jamra akalipiga kisha akenda alikofikia katika Mina akachinja, kisha akamwambia kinyozi: ‘Ondoa’, akaonyesha upande wake wa kulia wa kichwa kisha wa kushoto.” Imepokewa na Muslim na Ahmad.

—  Mwanamke haruhusiwi kunyoa kwa ajili ya umra wala hija, bali anapunguza kadiri ya inchi moja. Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - amesema: “Na linalowapasa wanawake ni kupunguza tu nywele zao.” Imepokewa na Abu Daud.

—  Kunyoa ni bora kuliko kupunguza, kwasababu Mwenyezi Mungu amekutaja mwanzo katika kauli Yake Aliyetukuka:

) مُحَلِّقِينَ رُؤُوسَكُمْ وَمُقَصِّرِينَ(

   {mkinyoa vichwa vyenu na mkipunguza nywele} [Al-fat`h, 27], na kwasababu Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - amesema: “Allah awarehemu wenye kunyoa” mara tatu, pakasemwa: ‘na wenye kupunguza?’, akasema: “Na wenye kupunguza.” Imepokewa na A'Rabi'u, Bukhari na Muslim.

—  Yanamhalalikia mwenye kuhiji baada kunyoa (au kupunguza) yale yote aliyozuiliwa kwasababu ya ihramu isipokuwa mke na kuwinda. Hali hii huitwa “tahal-lul as-ghar” yaani kutokana na ihramu kudogo. Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - amesema: “Mkishapiga jamra na kunyoa itakuwa halali kweni kila kitu ila wake zenu.” Imepokewa na Nasaaiy, Ahmed na Baihaqiy.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment