Ibadhi.com

14. KUCHINJA

 

Baada kulipiga Jamra la Aqaba mwenye kuhiji atachinja mnyama wake wa hadyi ili kumfuata Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie.

Kinachochinjwa huwa ngamia au n`gombe au kondoo au mbuzi. Kondoo au mbuzi mmoja hutosheleza kwa mtu mmoja ikiwa ametimiza mwaka, na kuna kauli miaka miwili. N`gombe akiingia mwaka wa nne na ngamia akiingia mwaka wa sita hutosheleza kwa watu saba.

Kuchinja kuliko wajibu huwa kwa mfanya-tamat-tuu na mfanya-qiraanu.

Mnyama huyo huchinjwa ndani ya eneo la Haram.

Inapendelewa amchinje mwenye kuhiji mwenyewe akiweza.

Anapendelewa ale sehemu ya nyama yake na atoe sadaka iliyobaki.

Mfanya-ifraadu hawajibiki kuchinja.

 

MAZINGATIO

Iwapo amenunua mnyama wa kuchinja na kwa ajili ya msongamano hakutowa thamani basi haitamwajibikia kumrudisha, lakini atapaswa  ikiwa hamjui mwenyewe aigawe thamani yake kwa mafakiri.

Haijuzu kumchinja mnyama wa hadyi kabla wakati wake na vilevile haijuzu pasipo mahali pake. Wakati wake ni siku ya kuchinja (10 Dhul-hija) na kwa hiyo atakaechinja kabla yake basi na achinje tena.

Asipoweza mwenye kuhiji kuchinja siku ya kuchinja atabaki na ihramu yake mpaka achinje kwasababu haisihi kutokana na ihramu kabla kuchinja.

Asiyeweza kumpata mnyama wa hadyi itampasa afunge siku ya tarehe: sita, saba, na nane Dhul-hija kisha afunge siku saba baada kumaliza amali za hija.

Inajuzu kuchinja mnyama wa hadyi katika sehemu zote za Haram na sio eneo la Mina pekee kwani hii ni kauli ya baadhi ya wanazuoni tu.

Haijuzu kupewa nyama mchinjaji kwa ajili ya uchinjaji bali ampe ujira wake mbali.

Mwenye kufanya umra katika miezi ya hija kisha akarudi nchini kwake na akaazimia kuhiji kwa ifraadu (kufanya hija pekee) haitamlazimu kuchinja kwasababu ya kutokuwa katika hukumu ya mfanya-tamat-tuu.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment