Ibadhi.com

11. HUKUMU ZA SIKU YA TAREHE 9 DHUL-HIJA (SIKU YA ARAFA)

 

î Inapendelewa kwa mwenye kuhiji aoge mwili mzima huko Mina kwa nia ya kusimama Arafa.

î Mwenye kuhiji ataondoka Mina siku ya tarehe 9 Dhul-hija baada ya kuchomoza jua kuelekea Arafaat huku anatamka takbira na ‘laa ilaaha ila-LLah’ na talbia.

î Akifika Arafaat na jua likapindukia (wakati wa adhuhuri) atahudhuria khutba ya imamu kisha atasali adhuhuri na alasiri kwa kujumuisha na kufupisha mwanzoni mwa wakati wa adhuhuri.

î Kusimama Arafa ndiyo nguzo kuu ya hija kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Hija ni Arafa.” Imepokewa na a'Nasai, a'Tirmidhi na Abu Daud.

î Kinachokusudiwa kwa kusimama Arafa ni kuhudhuria sehemu yo yote ya Arafa isipokuwa ndani ya Urana (bonde liliopo upande wa magharibi ya Arafaat) tangu baada ya kupindukia jua (adhuhuri) hadi lizame kwa siku hiyo.

 

MAZINGATIO

 ·        Tohara si sharti katika kusimama Arafa.

·        Katika sunna ni kujitahidi kwa dua na kumdhukuru Allah baada ya sala ya adhuhuri na alasiri mpaka kutua kwa jua.

·        Mwenye kuhiji hataondoka Arafaat kuelekea Muzdalafa ila baada ya kuzama kwa jua. Maulama wetu wamekemea sana kuondoka mwenye kuhiji pahala pake kwenda kwingine kwa nia ya ifadha (kuondoka Arafa) kabla ya kuchwa kwa jua na wamekufanya sawa na ifadha japokuwa hajatoka nje ya mipaka ya Arafa ila baada ya jua kuzama.

·        Wengi wa Maulama wa madhehebu yetu na madhehebu ya Malik wanaona kuwa kuondoka Arafa kabla ya kuchwa jua hubatilisha hija; wengineo wanaona hakubatilishi lakini kunawajibisha kuchinja.

·        Inapendelewa kwa mwenye kuhiji kuomba dua zilizopokewa na kutamka talbia katika Arafa, kwani kutamka talbia kuna kheri na kwa hiyo haipasi kusitishwa kabla kulipiga jamra siku ya kuchinja (10 Dhul-hija).

·        Mwenye kudiriki kabla ya kuchwa jua kusimama Arafaat kadiri ya kusoma “Albaaqiyaat Assaalihaat” (SubhaanaLLah walhamduliLLah, walaa ilaaha illa-LLah waLLahu akbar) amewahi hija kwa maafikiano ya wote. Hitilafu ipo kuhusu atakayewahi hayo wakati wa usiku kabla alfajiri ya siku ya kuchinja (10 Dhul-hija); na fatwa inayotolewa kwetu ni kwamba mwenye kuwahi kusimama Arafaat usiku au mchana kisha akasimama Muzdalafa usiku wa kuamkia siku ya kuchinja na akaiwahi sala ya alfajiri hapo Muzdalafa basi huyo ameiwahi hija.

·        Katika sunna ni kuondoka Arafa kwa utulivu kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie - wakati alipoondoka huko: “Enyi watu! Kuwenu watulivu; hakika wema si katika kwenda mbio.”  Imepokewa kwa maafikiano.

Vilevile imekuja kwenye Musnad ya Imam A'Rabi'u - Allah amridhie - kutoka kwa Abu Ubaida kutoka kwa Jabir bin Zaid amesema: Ameulizwa Usama bin Zaid vipi Mtume wa Mwenyezi Mungu - rehma za Allah na amani zimshukie - alikuwa akienda katika ‘hija ya maagano’ alipoondoka Arafa, akasema: Alikuwa akikazana na akipata nafasi huzidisha kasi ya mwendo.[1][1] - Sk. Saalimiy amesema katika sherehe ya Musnad hii uk. 233: “Amesema Ibnu AbdilBarri: hamna katika hadithi hii zaidi ya ujuzi wa hali ya mwendo wa kuondokea Arafa kuelekea Muzdalafa. Akasema: nalo ni katika yanayowalazimu viongozi wa hija na walio chini yao kuyafanya kwa ajili ya kuharakia sala, kwasababu magharibi haisaliwi ila pamoja na isha huko Muzdalafa, yaani zijumuishwe maslahi mbili – utulivu wakati wa msongamano na kuharakiza pasipo msongamano kwa ajili ya sala.”

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment