Ibadhi.com

8. KUSAI BAINA SAFA NA MARWA

 

1.     Akikaribia kwenye Safa atasoma kauli Yake Aliyetukuka:

) إِنَّ الصَّفَا وَالْمَرْوَةَ مِن شَعَآئِرِ اللّهِ(

{Hakika Safa na Marwa ni katika alama za kuadhimisha dini ya mwenyezi Mungu} [Albaqara, 158].

2.     Atapanda juu yake mpaka aione Nyumba Takatifu, atakabir mara tatu kisha atamhimidi Allah, na anapendelewa aseme mara tatu:

" لاَ إلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ لاَ شَرِيكَ لَهُ ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وَهُوَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيْر، لاَ إلهَ إلاَّ اللهُ وَحْدَهُ ، أَنْجَزَ وَعْدَهُ وَنَصَرَ عَبْدَهُ ، وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ "

“Laa ilaaha il-la-llaahu wahdahu laa shariika lahu, lahul-mulku walahul-hamdu wa huwa 'alaa kulli shay’in Qadiir. Laa ilaaha il-la-llaahu wahdah, anjaza wa'dah, wa nasara 'abdah, wa hazamal-ahzaaba wahdah”

(Hapana anayestahiki kuabudiwa ila Allah peke Yake hana mshirika. Ufalme ni wake na Yeye ndiye wa kushukuriwa na Muweza juu ya kila kitu. Hapana anayestahiki kuabudiwa ila Allah peke Yake. Ametimiza ahadi Yake, akamnusuru mja Wake na akayashinda makundi ya washirikina peke Yake).

Kisha ataomba dua atakazo.

3.     Kisha atashuka kuelekea Marwa huku anamdhukuru Allah Mtukufu, mpaka akifika baina ya alama mbili za rangi ya kijani atatembea kwa haraka zaidi, na anapendelewa aseme:

"رَبِّ اغْفِرْ وَارْحَمْ، وَتَجاوَزْ عَمَّا تَعْلَمُ، إنَّكَ أَنْتَ الأَعَزُّ الأَكْرَمُ"

“Rabbi-ghfir war-ham, watajaawaz 'amma ta'lamu, innaka antal-a'azzul-akram”

(Mola wangu samehe na urehemu, na yaachilie unayoyajua; hakika Wewe ndiye Mwenye uwezo mkuu na ukarimu wa juu).

Wanawake haiwapasi kutembea kwa haraka.

1.     Kisha atatembea taratibu huku anamdhukuru Allah na kumuomba kheri ya duniani na ya akhera mpaka akifika kwenye Marwa atasimama juu yake na kufanya kama alivyofanya juu ya Safa, na kwa hayo atakuwa ameshamaliza duru moja.

2.     Kisha atafanya duru ya pili kutoka Marwa hadi safa na atafanya kama alivyofanya katika duru ya mwanzo mpaka atimize duru saba kwa kumalizia kwenye marwa.

3.     Inajuzu kusai pasina tohara lakini anapendelewa awe katika tohara.

 

MASHARTI YA SA'YI:

1)   Iwe baada ya tawafu.

2)   Iwe duru saba.

3)   Ianzie kwenye Safa, imalizie kwenye Marwa.

 

 

MAZINGATIO

v Wanazuoni wamekhitalifiana kuhusu hukumu ya sa'yi: kuna kauli ni fardhi na kuna kauli ni sunna ya wajibu. Kwa kauli ya kwanza, atakayeiacha basi hija yake hubatilika, na kwa kauli ya pili hija yake haibatiliki lakini atawajibika kuchinja, nayo ndiyo kauli ya wengi wa wanazuoni wa Madhehebu hii.

v Mwenye kusai kuanzia Marwa na kumalizia Safa kisha akatokana na ihramu itamlazimu arejee kwenye ihramu yake na atimize sa'yi yake kwa kutoihisabu duru ya mwanzo ambayo alianzia Marwa hadi Safa, kisha atawajibika kuchinja mara mbili, na kwa kauli nyengine kitachomwajibikia ni fidiya kwa kutahalali kabla kukamilisha Sa'yi.

v Haikatazwi kusai upande mmoja kutoka Safa hadi Marwa kwenda na kurudi, kwani ugawaji wa eneo la sa'yi ni kwa ajili ya kuwepesisha, ambalo hapo kabla halikuwapo, lakini bora kufuata nidhamu ya mwendo iliyowekwa ili kuondoa msongamano; bali hilo ni wajibu iwapo kusai kwake huko kutapelekea kuwadhuru wengine.

v Mwenye kusai chini ya duru saba na hakukumbuka ila baada ya kutokana na ihramu itampasa arejee ihramu yake na atimize sa'yi yake kisha itamwajibikia kuchinja, na kwa kauli nyengine kitachomwajibikia ni fidiya, na kauli nyengine hakimwajibikii kitu.

v Kupanda juu ya vilima viwili vya Safa na Marwa kunasuniwa kwa wanaume kwa kadri ya mmoja wao kuiona al-Kaaba sio kwa wanawake.

v Iwapo mwenye kusai hakuweza kuisoma dhikri iliyopokewa juu ya vilima viwili vya Safa na Marwa haikatazwi kwake kuisoma wakati anapotembea baina yake, hasa pakiwa na zahama.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment