Ibadhi.com

7. TAWAFU

 

Ni kuizunguka al-Kaaba kuanzia kwenye Jiwe Jeusi na kumalizia hapo hapo ili utimie mzunguko wa mwanzo, na hurudiwa mara saba pamoja na kutamka “SubhaanaLLah walhamduliLLah, walaa ilaaha illa-LLah waLLahu akbar” na kuomba dua.

 

VIPI KUTUFU:

è Tawafu huanza kwa kulibusu Jiwe Jeusi ikiwezekana; isipowezekana atatosheka na kuligusa au kuliashiria kwa mkono wake pamoja na kutamka “Allahu Akbar” wakati wa kulishika.[1]

è Ataanza kutufu na hali ameifanya Nyumba ya Allah iwe kushotoni kwake.

è Ataomba dua atakazo wakati wa kutufu na atasoma “Albaaqiyaatu-ssaalihaatu” yaani:

سُبْحَانَ اللَّهِ وَالْحَمْدُ لِلَّهِ وَلاَ إِلَهَ إِلاَّ اللَّهُ وَاللَّهُ أَكْبَرُ

(Subhaana'Llah walhamduli'Llah, walaa ilaaha illa'Llah wa'Llahu akbar)

è Anapokuwa sawa na Pembe ya Yamani ataigusa ikiwezekana na hataiashiria kama hakuweza kuigusa.

è Akifika kwenye Jiwe Jeusi mzunguko wa kwanza unakuwa umemaliza, na ataanza mzunguko wa pili kama alivyofanya mwanzo mpaka atimize mizunguko saba.

 

SUNNA ZA TAWAFU:

1.     “Ramal”: Nayo ni kutembea kwa haraka na hatua zinazokaribiana bila kwenda mbio na kuchupa; hili linasuniwa katika mizunguko mitatu ya mwanzo.

2.     “Idh-tiba'u”: Nayo ni kupitisha sehemu ya kati ya shuka anayojifunika chini ya bega la kulia kwenye kwapa na kuzitupia ncha zake juu ya bega lake la kushoto, yaani aweke wazi bega lake la kulia. “Idh-tiba'u” huwa katika mizungu-ko yote saba[2].

Tanbihi: “Ramal” na “Idh-tiba'u” haziwi ila katika tawafu ya “al-quduumi” au tawafu ya umra[3].

3.     Rakaa mbili za tawafu: Nazo ni rakaa mbili zinazosaliwa baada ya tawafu nyuma ya Maqamu ya Nabii Ibrahim - amani imshukie - au po pote itapowezekana. Dalili ya hilo ni hadithi ya Ibnu Umar Allah amridhie iliyoko kwa al-Bukhari anasema: Alikuja Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - akaizunguka Nyumba ya Allah mara saba kisha akasali nyuma ya Maqamu rakaa mbili kisha akatoka kwenda kwenye Safa, na Allah Aliyetukuka amesema:

) لَقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ(

{Bila shaka katika Mtume wa Allah mmekuwa na kigezo kizuri} [Al-ahzaab 21].

 

MAZINGATIO

¨     Inajuzu kusali rakaa mbili za tawafu baada ya sala ya alfajiri kabla ya kuchomoza jua na baada ya sala ya alasiri kabla ya kuchwa jua kwa kauli iliyopewa uzito na wenye ilmu, kwasababu hiyo ni sala yenye sababu iwapo atatufu katika nyakati mbili hizi.

¨     Inajuzu kutufu Nyumba Takatifu wakati imamu anahutubu Ijumaa lakini bora kusubiri.

¨     Haijuzu kutufu ndani ya ule ukuta mfupi wa “alhatiim” kwasababu ni sehemu ya Kaaba.

¨     Inajuzu kwa mwenye kuhiji au kufanya umra anapotufu au anaposai kupumzika katika ibada hizo akihitaji hilo.

¨     Haikatazwi kutufu katika nyakati tatu zilizoharamishwa kwani kinachokatazwa ni kusali nyakati hizo.

¨     Mwenye kutufu akawa na shaka katika idadi ya mizunguko aliyozunguka atachukulia idadi iliyo ndogo kati ya idadi mbili anazozifikiria, kisha ataendelea na mizinguko iliyobaki.[1] - Inasuniwa kukabir katika kila mzunguko hata katika mzunguko wa mwisho, na akitamka “BISMILLAHI” kabla yake itakuwa vizuri kwa vile hilo limepokewa kutoka kwa Ibnu Umar – Allah amridhie – kwamba alikuwa anapolishika Jiwe hilo husema: “BISMILLAHI WALLAHU AKBAR”. Ameipokea al-Baihaqi na wameisahihisha jumla ya wenye ilmu.

[2] - Hii ndiyo sahihi kwa Al Allaama Al-Qannuubi, ingawa iliyo mashuhuri kwamba idh-tiba'u ni kama ramal huwa katika mizunguko mitatu ya mwanzo tu. Angalia Sualu Ahli 'Dhikri kipindi cha tarekhe 9 Dhul-qa'da 1423AH / 12-1-2003CE, jawabu ya suali la kwanza.(Mfasiri)

[3] - Tawafu ya umra ina hukumu ya tawaful-quduumi kwa kuwa ni ya mwazo anapofika Makka.(Mfasiri)

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment