Ibadhi.com

6. VIPI KUHIRIMIA

§  Inapendelewa ajinadhifishe kwa kuondoa msokotano wa nywele, kunyoa nywele za siri, kukata kucha, kunyonyoa kwapa, kupunguza sharubu na kuondoa manukato, kwa ambaye bado hajafanya hayo.

§  Inapendelewa kuoga na kutawadha kabla kuhirimia kwa kila anayekusudia kuhirimia hata mwenye hedhi au nifasi.[1]

§  Mwanamme avue nguo zilizoshonwa na za kujivika[2] na avae kikoi, shuka ya kujifunika mabegani na viatu vya ndara; kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Na ahirimie kila mmoja wenu katika kikoi, shuka na viatu vya ndara.” Ameipokea Ahmed.

§  Ama mwanamke, kuhirimia kwake ni usoni; haimjuzii kufunika uso wake ila akiogopa kushawishi wanaume atauteremshia uso wake nguo kutoka kichwani. Yeye anaruhusiwa kuvaa nguo iliyoshonwa, lakini aepuke kila ambayo ina mapambo, na anakatazwa kuvaa glavu, kama ilivyokuja kwenye hadithi: “Mwanamke mwenye kuhirimia asijifunge nikabu wala asivae glavu.” Imepokewa na al-Bukhari na wengineo.

§  Asali rakaa mbili za ihramu kwa kauli ya baadhi ya wanazuoni baada ya kuoga. Iwapo umefika wakati wa sala ya fardhi basi bora ahirimie baada ya sala hii na atamke talbia baada yake moja kwa moja. Na kuna kauli atamke talbia akishapanda kipando cha safari yake.

§  Anuie ibada anayokusudia (hija au umra) kama ilivyotangulia katika mlango wa namna za kuhiji na afanye talbia kwa kuainisha namna ya kuhiji anayokusudia. Aseme katika talbia:

[لَبَّيْكَ اللَّهُمَّ لَبَّيْكَ، لَبَّيْكَ لاَ شَرِيكَ لَكَ لَبَّيْكَ، إِنَّ الْحَمْدَ وَالنِّعْمَةَ لَكَ وَالْمُلْكَ، لاَ شَرِيكَ لَكَ]

(Labbayka-LLahumma labbayk. Labbayka laa shariika laka labbayk. Innal-hamda, wan-ni'mata laka wal mulk. Laa shariika lak)

(Yaani: Nakuitika tena na tena ewe Allah. Nakuitika tena na tena, huna mshirika, nakuitika tena na tena. Hakika shukrani na neema ni Zako pamoja na ufalme; huna mshirika)

Akishakuwa juu ya kipando chake atanyanyua sauti kwa talbia.

§  Atakithirisha kutamka talbia hususan zinapobadilika hali na nyakati, k.m. akipanda kilima au akiteremka bonde na wakati wa kupanda kipando na wa kushuka, na kila baada ya sala; kwani talbia inaushughulisha wakati kwa kumdhukuru Mwenyezi Mungu. Imepokewa kwa Sahlu bin Saad kuwa Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - amesema: “Hatamki talbia Muislamu ye yote ila vitatamka naye talbia viliopo kuliani na kushotoni kwake vikiwa mawe au miti au udongo mpaka mwisho wa ardhi kwa upande huu na upande huu.” Imepokewa na Ibnu Majah, al-Baihaqi, a'Tirmidhi na al-Haakim akaisahihisha.

§  Akifika Masjidul-Haram ataacha talbia na kuanza ibada ya umra.

 

MAZINGATIO

 §  Bora ahirimie katika nguo nyeupe ingawa hazikatazwi nyenginezo, kutokana na kauli ya Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie: "Zishikeni hizi nguo nyeupe; wavikeni walio hai kati yenu na wakafinieni maiti zenu, kwani hizi ndiyo bora kati ya nguo zenu…". Kaipokea Imam a'Rabii' bin Habib.

§  Mwenye kusafiri kwa ndege atahirimia kabla hajafika kwenye miiqati ili asiivuke miiqati ila amehirimia, na hapana ubaya kwake akitamka talbia baada ya kuondoka na ndege.

§  Inamjuzia muhrimu (yaani aliye katika ihramu) kuoga na kubadili nguo za ihramu alizovaa kwa nguo nyingine za ihramu akiepuka yaliyozuiwa katika ihram.

§  Kuhirimia na kuvaa ihramu hakumlazimu mwenye kuingia Makka kama hajakusudia kufanya umra au hija.

§  Hakuna nia ya matamshi inayomlazimu mwenye kuhiji au mwenye kufanya umra anapohirimia, lakini inamlazimu kufanya talbia kwa kutamka na sio kwa kuileta moyoni.

§  Muhrimu inamharamikia kujitia manukato akiwa katika ihramu.

§  Akishahirimia, muhrimu haruhu-siwi kuondoa vinavyo kamata taka mwilini: kama kunyoa nywele, kukata kucha, kunyonyoa kwapa, kunyoa nywele za siri na nyinginezo, isipokuwa kwa dharura ya ugonjwa n.k.[3]

§  Ni haramu kwa muhrimu maingiliano ya kijinsia baina mume na mke na kushikana kwa matamanio k.m. kulala pamoja katika nguo moja, kubusiana n.k.

§  Muhrimu hafungi ndoa wala hafungishi ndoa kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Muhrimu hafungi ndoa wala hafungishi ndoa wala haposi.” Imepokewa na a'Rabi'u na Muslim.

§  Ni haramu kwa muhrimu kuwinda kiwindo cha nchi-kavu kutokana na kauli Yake Aliyetukuka:

)وَحُرِّمَ عَلَيْكُمْ صَيْدُ الْبَرِّ مَا دُمْتُمْ حُرُماً(

   {Na mumeharamishiwa viwindo vya nchi-kavu maadamu mumo kwenye ihramu} [Al-maida 96]. Ama viwindo vya bahari havikatazwi.

§  Muhrimu mwanamme hafuniki kichwa chake kwa cho chote ila kwa dharura kama matibabu, joto au baridi, ambapo itamwajibikia fidya[4].

§  Muhrimu anakatazwa kubishana kunako sababisha ghadhabu, kutokana na kauli Yake Aliyetukuka:

)الْحَجُّ أَشْهُرٌ مَّعْلُومَاتٌ فَمَن فَرَضَ فِيهِنَّ الْحَجَّ فَلاَ رَفَثَ وَلاَ فُسُوقَ وَلاَ جِدَالَ فِي الْحَجِّ(

{Hija ni miezi maalumu; anayekusudia katika miezi hiyo kufanya hija basi hakuna kusema maneno machafu wala kufanya maasi wala kubishana katika hija} [Albaqarah 197].

§  Hakatazwi muhrimu kupiga msuwaki hata kama utakifanya kinywa chake kitoke damu.

§  Maneno machafu yanapingana na tabia za muislamu, na katika ihramu huwa yanachusha zaidi.

§  Mwenye kuhirimia hija katika miezi isiyo ya hija ihramu yake hugeuka ya umra, na kuna kauli kwamba hubatilika.

§  Inamjuzia Muhrimu kuvaa ukanda akiuhitaji kufungia shuka aliyovaa na kuhifadhia pesa zake.

§  Haikatazwi kuvaa viatu vya ndara vilivoshonwa.

§  Hakatazwi mwanamke aliyehirimia kuvaa mapambo yake ya madini (dhahabu n.k.) katika ihramu ikimwia shida kuyavua, kwa sharti ayafunike kwani kudhihirisha mapambo kwa wasiokuwa mahramu hakujuzu katika hija wala kwengineko.[1]- Kumekuja katika hilo baadhi ya mapokezi yaliyo nasibishwa na Mtume, na kumekuwa na khilafu katika kuyasahihisha au kuyadhoofisha, isipokuwa yaliyopokewa na Muslim kwa njia ya Bibi Aisha - Mwenyezi Mungu amridhie - amesema: “Alijifungua Asma bint Umais Muhammad bin Abi Bakr penye mti (katika eneo la Dhul-hulaifa), Mtume S.A.W. akamuamuru Abu Bakr amuamuru aoge kisha ahirimie.” Kuna riwaya nyingine imemalizikia kwa Ibnu Umar amesema: "Ni katika sunna mtu aoge akitaka kuhirimia na akitaka kuingia Makka.” Ameisimulia al-Bazzaar na a'Daaraqutniy na a'Tabaraaniy kwenye ‘al-Kabiir’ na al-Haakim akaisahihisha.

[2]- Nguo zinazouzunguka mwili au baadhi yake kwa kushonwa au vinginevyo.

[3] - Muhrimu atakayefanya kati ya hayo kwa dharura ya ugonjwa n.k. hana budi kufidia ima kwa kufunga siku tatu po pote atakapo, au kulisha maskini sita walioko Makka (au katika al-Haram, kila mmoja milo miwili [na kuna kauli mlo mmoja] au vibaba viwili [sawa na 1.025 kg] vya chakula, kama mchele, ngano, n.k.) au kuchinja mbuzi mmoja au kondoo kuwasadakia maskini walioko Makka (au katika al-Haram). Haya ni ufafanuzi wa Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- wa kauli ya Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala:

{وَلَا تَحْلِقُوا رُءُوسَكُمْ حَتَّى يَبْلُغَ الْهَدْيُ مَحِلَّهُ فَمَنْ كَانَ مِنْكُمْ مَرِيضًا أَوْ بِهِ أَذًى مِنْ رَأْسِهِ فَفِدْيَةٌ مِنْ صِيَامٍ أَوْ صَدَقَةٍ أَوْ نُسُكٍ}

{Wala msinyoe vichwa vyenu mpaka wanyama wa hadyu wafike machinjoni mwao. Na atakaye kuwa mgonjwa au ana vya kumuudhi kichwani mwake basi afidiye kwa kufunga au kwa kutoa sadaka au kuchinja mnyama} Albaqara: 196

[4] - Nayo ni kama ilivotajwa katika maelezo ya chini yaliyotangulia.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment