Ibadhi.com

5. NAMNA ZA KUHIJI

 

Kuhiji kuna namna tatu, nazo:

 

1-    Tamat-tu': Nayo ni kuhirimia umra peke yake katika miezi ya hija, akimaliza atatokana na ihramu ya ibada hiyo, kisha atahirimia hija siku ya Tarwiya (8 Dhul-hija) au kabla yake. Tamat-tu' ndio namna bora ya kuhiji, na inashurutiziwa iwe umra na hija katika mwaka mmoja, safari moja na asirejee nchini kwake au mfano wake kwa umbali baina ya ibada mbili hizo.

 

 

Mfanya-tamat-tu' humwajibikia kichinjo cha Tamat-tu'.

 

 

 

2-    Qiraanu: Nayo ni kuhirimia hija pamoja na umra katika miezi ya hija kisha kubaki na ihramu mpaka atakapotokana na ihramu ya ibada mbili hizo kwa pamoja siku ya kuchinja (10 Dhul-hija).

 

 

 

Mfanya-Qiraanu huwajibika pia kuchinja. Yeye inamtosheleza Tawafu moja na Sa'yi moja kwa hija na umra yake, kutokana na kauli yake - rehma za Allah na amani zimshukie: “Mwenye kuhirimia hija pamoja na umra itamtosha Tawafu moja na Sa'yi moja kwa zote mbili mpaka ajihalalishe nazo pamoja.” Ameipokea a'Tirmidhi na Ibnu Maajah. Na kuna kauli kuwa lazima kuwe na Tawafu mbili na Sa'yi mbili.

 

 

Mwenye kufanya hija ya Qiraanu akiingia Maka atatufu Tawaful-Quduumi[1], na anaweza kufanya Sa'yi kabisa akitaka, halafu atakaporejea siku ya  kufanya Tawafu ya Ifadha akatoshelezeka kwa Tawafu tu; kwasababu ameshafanya Sa'yi hapo kabla kwa uoni wa baadhi ya wanazuoni.[2] Na kuna kauli aakhirishe Sa'yi apate kuifanya pamoja na Tawafu ya Ifadha.

 

 

 

3-    Ifraadu: Nayo ni kuhirimia hija peke yake na kubaki na ihramu mpaka utakapolirushia vijiwe Jamratul-Aqaba siku ya kuchinja (10 Dhul-hija), kisha baada ya hapo unatahalal (yaani unatokana na ihramu).

 

 

 

MAZINGATIO

 

† Mfanya-Ifraadu haimlazimu umra anapofanya hija pekee. Akitaka kufanya umra ni baada ya siku za Tashriiq (ambazo ni 11 – 13 Dhul-hija).

 

† Inajuzu kuhirimia hija pekee hata kwa ambaye hakufanya umra hapo kabla.

 

† Mfanya-Ifraadu inamjuzia kutufu Tawaful-Quduumi bila kufanya Sa'yi, na kwa kauli nyengine anaweza kufanya na Sa'yi ya hija kabisa.[3]

 

† Mfanya-Ifraadu na Mfanya-Qiraanu wakiwa hawajasai baina ya Safa na Marwa walipotufu Tawaful-Quduumi itawalazimu wafanye Sa'yi watakapotufu Tawaful-Ifadha kwa mawafikiano ya wote.

 [1]- Tawaful-Quduumi ni tawafu iliyosuniwa kwa mwenye kuingia Makka akiwa amehirimia hija ya Qiraanu au ya Ifraadu; ama anayekwenda Mina au Arafa moja kwa moja bila kuingia Makka hakusuniwa kufanya Tawaful-Quduumi. Kuna kauli kuwa tawafu anayotufu kabla ya kwenda Mina mwenye kuchanganya hija na umra (Qiraanu) ni tawafu ya umra na humtosheleza badala ya Tawaful-Quduumi. Pia mwenye kufanya umra kabla ya hija (yaani Tamattu'), inamtosheleza tawafu ya umra badala ya Tawaful-Quduumi - yaani hakusuniwa kufanya Tawaful-Quduumi mbali na tawafu ya umra.(Mfasiri)

 

[2]- Kuruhusiwa mwenye hija ya Qiraanu au ya Ifraadu aliyetufu Tawaful-Quduumi kufanya Sa'yi kabisa ndiyo sahihi kwa Sheikh wetu Al-Allaama Said Al-Qannuubi; bali kasema ndiyo bora kwa kuwa ndivo alivofanya Mtume wa Allah –rehma za Allah na amani zimshukie. Kwani yeye –rehma za Allah na amani zimshukie- alifanya hija ya Qiraanu (hakuweza kufanya Tamattu' kwasababu alikuwa amekwenda na wanyama wa kuchinja), na hakufanya Sa'yi baada ya Tawafu ya Ifadha kwa kuwa aliitanguliza Sa'yi baada ya Tawaful-Quduumi, na ndivo pia walivofanya masahaba kwa idhini yake kati ya waliohirimia hija ya Qiraanu na waliohirimia hija ya Ifraadu.(Rejea Sualu Ahli 'Dhikri, kipindi cha tarekhe 6 Dhul-qa'da 1425AH / 19-12-2004CE, jawabu ya suali la tano). Hivyo, Sa'yi anayoifanya mwenye hija ya Qiraanu baada ya Tawaful-Quduumi inamtosheleza kwa umra na hija yake, pia Tawafu ya Ifadha inamtosheleza kwa hija na umra yake na kwa hiyo hatafanya Sa'yi baada ya Tawafu ya Ifadha. Halikadhalika mwenye hija ya Ifraadu iwapo atatanguliza Sa'yi ya hija yake baada ya Tawaful-Quduumi hatafanya Sa'yi baada ya Tawafu ya Ifadha. Hili bila shaka linawapa watu wepesi mkubwa hususan katika zama hizi kutokana na zahma iliyozidi ya mahujaji wakati wa Tawafu ya Ifadha.(Mfasiri)

[3]- Angalia maelezo ya chini nam. 2 yaliyotangulia.(Mfasiri)

 

 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment