Ibadhi.com

4. KUSAFIRI KWA MDAIWA DENI LA RIBA

 

Huyu hali yake ni ngumu mno kuliko aliyetangulia. Ni juu yake kwanza ajitakase na kila muamala wa riba; kwani Allah Mtukufu hawapokelei ila watu wacha-Mungu; na mwenye kuingia katika riba hayumo kabisa katika ucha-Mungu. Inatosha kuwa yeye yumo vitani dhidi ya Allah na Mtume Wake - rehma za Allah na amani zimshukie.

 

MAZINGATIO

—  Kukopa kwa ajili ya kuhiji hakuna haja, kwasababu mwenye kuhiji hutakiwa atokane na majukumu yote kabla hajasafiri, na miongoni mwa hayo ni madeni. Hata hivo, akikopa akahiji, hija yake ni sahihi.

—  Wengi kati ya watu huchelewesha hija mpaka wakifikia umri mkubwa huusia wafanyiwe hija iliyo walazimu. Hili ni kinyume na amri ya Allah Mtukufu aliyetakasika, kwani wasia hauwi badala ya hija. Mwenye uwezo anawajibika kuharakiza kuhiji mwenyewe; kuusia ni kuchukua tahadhari tu yasije mauti yakamfika ghafla kabla ya kuhiji.

—  Haimlazimu mtoto kuwahijia wazazi wake waliokufa maadamu hawakuusia. Akiwahijia itakuwa ni wema aliowafanyia anaolipwa thawabu na ni utiifu kwa Allah; na wao wanatarajiwa kupata thawabu wakiwa katika watu wa kheri.

—  Anayesafiri kwenda Maka au Madina au kwengineko ina-mwajibikia kupunguza sala za rakaa nne ziwe rakaa mbili asiposali nyuma ya imamu mkaazi. Kuisali kila sala kwa wakati wake ni bora, na kuchanganya sala mbili kunajuzu hususan kwa ambaye yumo njiani katika safari.

—  Hija ni nguzo na fardhi mojawapo ya Uislamu. Uwajibikaji wake na utekelezwaji hautegemei kuoa na kuolewa au ukubwa wa umri, kama wanavyodhani wengi kati ya watu. Bali kuhiji ujanani ni bora zaidi ili mtu aweze kuitekeleza kama ipasavyo kisheria.

—  Mwenye kuhiji anatakiwa afanye bidii kubwa ili atekeleze hukumu zote za hija na asidharau cho chote kati ya suna za hija na adabu zake ili kufikia faida ambayo kwa ajili yake imewekwa katika Sharia ibada ya hija, nayo ni uchamungu.

—  Achunge adabu za safari kwenda na kurudi. Kama anavowajulisha watu wake anaposafari awajulishe anaporudi. Mtume –rehma za Allah na amani zimshukie- amekataza mmoja wetu kuwafikia watu wa nyumba yake usiku pasina kumtarajia.

—  Ashikilie subra na tabia njema kwani safari ni jambo linalotarajiwa kuwa na usumbufu, na hija ni zaidi katika hilo kutokana na zahama na kusongamana na watu.

 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment