Ibadhi.com

2. KUJIANDAA KWA HIJA

 

بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

UTANGULIZI

Shukrani zote zinamstahikia Allah aliyefaradhisha kuihiji Nyumba Yake Takatifu Muadhamu, akaifanya hija mkutano mkuu wa dunia wa Uislamu. Kisha rehma na amani zimshukie Nuru ya uongofu na Taa ya gizani, aliyesema, “Pokeeni kwangu ibada zenu za hija.”

Baada ya hayo:

Idara ya Utafiti wa Kitaalamu imeonelea – katika wakati ambao watu hukumbilia kwenye vifupisho – itoe toleo hili HUKU NDIKO KUHIJI ili kuwahudumia mahujaji wa Nyumba ya Allah Takatifu katika upande wa muongozo na maelekezo. Allah Ndiye tunayemuomba anufaishe kwa toleo hili viumbe.                                                                     

Ofisi ya Fatwa                                                        Idara ya Utafiti wa Kitaalamu

 

 KUJIANDAA KWA HIJA

 Mwenye kutaka kuhiji anatakiwa afanye mambo kadha kabla kuingia safarini, nayo ni:

1.     Kumtakasia nia Allah Mtukufu aliyetakasika; kwani Allah hapokei ila kilichokuwa kwa ajili yake pekee. Mwenyezi Mungu kasema:

                  ﭿ  ﮀﮁ          

{Sema: Nimeamrishwa nimuabudu Mwenyezi Mungu, na nisimshirikishe. Kwake Yeye naita (watu), na kwake Yeye ndiyo marejeo yangu} [A'Ra'du: 36]

Vile vile kasema:

      

{Mwenyezi Mungu ndiye wa kutakasiwa dini bila kushirikishwa} [Az-zumar, 3]

Pia kasema:

            

{Sema: Mwenyezi Mungu tu namuabudu kwa kumtakasia dini yangu} [A'Zumar: 14]

Aidha kasema:

                          ﮤﮥ        

{Wala hawakuamrishwa ila kumuabudu Mwenyezi Mungu kwa kumtakasia dini, waache dini za upotofu, na wasimamishe sala na kutoa zaka, na hiyo ndiyo dini iliyo sawa} [Albayyinah: 5]

2.     Toba ya kweli kutokana na kila kosa alilofanya ili aje kwa Mola wake akiwa msafi wa moyo.

3.     Awaachie wanaomlazimu matumizi ya lazima hadi kurudi kwake. Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie - anasema: “Ni kosa la kumtosha mtu kuwatupa waliomlazimu.” Ameipokea al-Bukhari.

4.     Ajichukulie mahitaji ya safari ya kutosheleza ili abaki katika tabia ya kupendeza. Kutoka kwa Ibnu Abbas – Allah awaridhie – amesema: Watu wa Yemen walikuwa wakihiji na hawachukui mahitaji ya safari, na wakisema: Sisi ndio tunaomtegemea Allah. Wakifika Maka huwaomba watu. Allah Mtukufu akateremsha kauli Yake: “Na jichukulieni mahitaji ya safari, kwani mahitaji bora ya safari ni ucha-Mungu.” Ameipokea al-Bukhari na Abu Daud.

5.     Alipe madeni yake, arudishe alivyoazima na amana za watu, na atokane na kila jukumu lililo juu yake; kutokana na kauli ya Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie: “Nafsi ya Muumini (aliyekufa) imewekwa rahani” – na katika riwaya nyengine “imetundikwa - kwa deni lake mpaka alipiwe.” Ameipokea a'Tirmidhi akaihasanisha na Ibnu Majah.

6.     Aandike wasia wake na haki zilizomlazimu. Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie anasema: “Si halali kwa mtu Muislamu aliye na kitu cha kuusia kulala siku mbili ila na wasia wake umeandikwa, uko kichwani kwake.” Ameipokea a'A'Rabi'u, al-Bukhari na Muslim.

7.     Awatake radhi watu wa nyumbani kwake, jamaa zake, jirani zake na wenzake, na awaage anapoondoka; na aimarishe udugu na wale aliokuwa amekata uhusiano nao, na awafanyie wema aliokuwa amewafanyia ubaya kwa moyo safi na toba ya kweli.

8.     Ajifunze vipi kuhiji; kwani ibada haisihi kwa asiyeijua. Akichukua kitabu kilichokusanya yanayohusu hija ni bora.

9.     Afuatane na watu wema watakaomsaidia kutekeleza ibada za hija.

10.     Ajitahidi matumizi yake yawe ya halali yasiyo na shaka.

11.     Inapendelewa safari yake iwe siku ya Alkhamisi; kwani imekuja kwenye Sahihi Mbili kutoka kwa Kaab bin Malik - Allah amridhie – amesema: “Mara chache Mtume - rehma za Allah na amani zimshukie – aliingia safarini siku isiyokuwa Alkhamisi; ikiwa imempita basi ni siku ya Jumatatu; maana ndiyo siku aliyohama Mtume wa Allah - rehma za Allah na amani zimshukie – kutoka Maka.”

12.     Wamempendelea baadhi ya wanazuoni anaposafiri aiage nyumba yake kwa rakaa mbili, ila ikiwa wakati wa safari yake ni wakati unaoharamishwa au kuchukiwa kusali, ambapo hatasali; kisha asome dua ya safari.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment