Ibadhi.com

1. FARIDHA YA HIJA.

HIJA: 

Faridha ya Hijja ni moja katika nguzo tato za Kiislamu, faridha hii ameilazimisha Allah mtukufu katika Kitabu chake Qur-ani tukufu pale aliposema: ((Na Allah amelazimisha kwa watu Kuihiji nyumba (Al-Qaabah) mwenye kuiweza njia yake)) [Aala Imaraan 97] na kutoka kwa Ibn Abbaas (r.a) amesema: Alituhutubia Mtume wa Allah (s.a.w) basi akasema: ((Enyi watu imelazimishwa kwenu kuhiji)) akasimama Al-Aqraa bin Haabis na akasema: Jee! Ni kila mwaka ewe Mtume wa Allah? Basi Mtume (s.a.w) hapo akasema: ((Lau nitalisema basi lingelazimika, na lau lingelazimika musingeliifanya na musingeliweza, Hija ni mara moja, na mwenye kuongeza basi amejitolea))

TAREHE YA KUFARADHISHWA HIJA:

Hija imefaridhishwa katika mwaka wa sita wa Hijiria kwa kuteremka ndani ya mwaka huo neno lake Allah mtukufu: ((Na timizeni Hija na Umra kwa ajili ya Allah tu)) [Al-Baqarah 196]

MAANA YA HIJA

Na neno hija maana yake kilugha ni kukusudia, ama kisheria ni safari ya kwenda Makka kwa nia ya ibada za kisimamo cha Arafah na ibada nyengine ambazo hazifanywi isipokuwa katika msikiti mtukufu wa Makka na sehemu zilizo karibu yake na kwa wakati mahususi.

HUKUMU YA MWENYE KUPUUZA HIJA.

Allah mtukufu ametubainishia kwenye kitabu chake kuwa mwenye kupuuza kwa makusudi ibada hii huyo hukumu yake ni ukafiri, ametuambia: 

((Na Allah amelazimisha kwa watu Kuihiji nyumba (Al-Qaabah) mwenye kuiweza njia yake na mwenye kukufuru basi hakika Allah amejitosheleza hahitaji ya walimwengu)) [Aala Imaraan 97]

Na Aya hii iko wazi kuwa lazimisho la kuhiji ni kwa watu wote (waislamu na wasiokuwa waislamu), na katika hili kuna dalili ya wazi kuwa wasiokuwa waislamu pia wamo katika makosa ya kutomtii Allah mtukufu katika Ibada zake, nalo linapewa uhakika kwa kusamehewa mwenye kusilimu miongoni mwao makosa yake yaliyo chini ya ushirikina; kwa hiyo Uislamu sio sharti ya kulazimika kwa Ibada hii ya hija na nyenginezo, bali Uislamu ni sharti ya kuwa sahihi Ibada hii ya hija na nyenginezo.

Na kwa maana hiyo watu wenye kupuuza ibaada hii ya hija wako aina mbili:

1. Washirkina:

Hawa sio waislamu aslan; kwa hiyo wao wanajihalalishia uasi wao, kwani hawatambui ulazimisho huu katika nafsi zao.

2. Wauislamu:

Hawa ni wenye kutambua ulazimisho wa Ibada hii katika nafsi zao, lakini wao wamo katika uasi wa makusudi.

Makundi yote maiwli haya kama alivyotuambia Allah mtukufu kuwa yamo katika hukumu ya Ukafiri kwa kosa lao hili.

Na hili linatupa uhakika wa wazi kuwa ukafiri ni sifa ya kuasi na ufasiki; kwa hiyo hailazimiki ukafiri kuwa ni ushirikina, basi kwa maana hiyo, sio kila kafiri ni mshirikina ingawa kila mshirikina ni kafiri.

Basi yule mwenye kuhalalisha uasi wake huu kwa kuona hakuna ulazima wa Ibada hii ya hija aslan na kuitakidi hilo katika nafsi yake huyo atakuwa ni Kafiri wa Kishirkina.

Ama yule mwenye kukubali ulazima wa Ibada hii katika nafsi yake na akajuwa kuwa yeye yumo katika kumuasi Allah mtukufu kwa kupuuza kwake Ibada hii huyo atakuwa ni Mnafiki yumo katika Ukafiri wa neema. 

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment