Ibadhi.com

JANABA NA JOSHO LAKE

Janaba ni hali inayompata Mwanamme au Mwanamke, kwa moja ya njia zifuatazo:

1.     Kufanya tendo la Jimai [1].

2.    Kutokwa au kujitoa Shahwa kwa njia yoyote ile [2].

 YALIYOKATAZWA KATIKA JANABA

Tambua ewe mwanafunzi, Allah akurehemu kuwa kuna mambo yanakatazwa kufanywa na Mwenye janaba, mambo hayo ni haya yafuatayo:

1.     Kushika Msahafu.

2.    Kusoma Qur-an.

3.    Kuingia Msikitini.

4.    Kusali.

Hata hivyo kuna mambo mengine yanaruhusiwa kwa Mwenye-Janaba kuyafanya, kama vile kusoma hadithi, kula, kunywa, n.k. Wallaahu-A'lam.

 NAMNA YA KUOGA JANABA

Tambua Ewe Mwanafunzi, Allah akurehemu kuwa kuna aina mbili za kuoga janaba:

(A)- Kuoga Janaba ki-kawaida tu.

(B)- Kuoga Janaba Ki-sunna.

 KUOGA JANABA KI-KAWAIDA

Tambua ewe mwanafunzi, Allah akurehemu kuwa anaepata Janaba ni wajibu wake kuliondosha janaba hilo kwa kueneza maji mwili mzima, wakati anafanya hivyo inampasa aweke nia moyoni: kuwa josho hilo ni la kuondosha Janaba.

 N.B: Kwa maana hiyo tuliyoiainisha hapo juu,  basi laiti Mtu atapata Janaba kwa bahati akaanguka mtoni au baharini, au akapigwa na mvua, mpaka akaroa mwili mzima, kwa vile hakutia nia ya kuondosha janaba, basi janaba itakuwa bado ipo, Wallaahu-A'alam.

 KUOGA JANABA KI-SUNNA

Tambua Ewe Mwanafunzi, Allah akurehemu kuwa Aliepatwa na Janaba akitaka kufuata Suna ya Mtume wake (s.a.w.w) katika kuondosha Janaba, basi kwanza atatakiwa afanye yafuatayo:

·       Aondoshe najsi katika utupu ('aura) wake, na sehemu nyengine.

·       Atie udhu kama udhu wa Sala.

·       Ajitie maji kichwani, kwa kuanzia kulia na kumalizia kushoto.

·       Ajitie maji kifuani na tumboni, kwa kuanzia Kulia na kumalizia Kushoto.

·       Ajitie maji mgongoni, kwa kuanzia kulia na kumalizia kushoto.

·       Ajitie maji miguuni, kwa kuanzia kulia na kumalizia kushoto.

-------------------------------------------------------------------------------------------------------

N.B: Udhu uliokogea janaba ikiwa haujatenguliwa na kitu, kama vile kutokwa na upepo, au kukamata utupu basi unaweza kusalia udhu huo, Wallaahu-A'alam.

[1]- Janaba inapatikana kwa njia ya Maingiliano ya kijinsia, sawa ikiwa ni ya-halali au ya-haramu, sawa ikiwa ni binaadamu kwa binaadamu, au binaadamu na mnyama, sawa ikiwa ni kwenye utupu wa mbele au wa nyuma, Wallaahu A'alam.

[2]-  Mtu anaweza kutokwa na shahwa (manii) kwa njia ya ndoto, kujifikirisha, kujichezea (ponyeto), Wal-'iyaadh-billaah.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment