117. HAMUONI KUWA MUNATUDHALILISHA?

Written by

Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

SUALI:

Tunaomba muusikilize Ujumbe huu wa sauti kisha mutujibu suali hili, jee! hamuoni kushirikiana na Mawahabi ni kudhalilisha Maibadhi?

JAWABU:

Ujumbe wa sauti tumeusikiliza nao umedhamini tuhuma kwa viongozi wa Istiqamah na baadhi ya Masheikh wetu waliopo Oman ambao walihudhuria katika hafla ya Mashindani ya Quraani yaliyofanyika jijini Dar-Ess-Salaam chini ya Uongozi wa Al-Hikma Foundation katika Ramadhani ya mwaka jana (1439), na uwepo wa mchango wa Maibadhi wa kifedha katika harakati za Mawahabi Tanzania.

Kwanza: Sisi hatumjui ni nani muhusika wa ujumbe huo, alikua ajitaje jina lake; kwa sababu ujumbe umedhamini lawama ambazo kikawaida hata Mawahabi wa Tanzania wanaweza kuziunda na kuzieneza katika Jamii kwa lego kuwapiga vita vya kinafsi Maibadhi, vita ambavyo lengo lake ni kudhoofisha mahusiano mazuri kati ya Maibadhi na Maduati wao, hususan wale ambao wameonekana katika shughuli za mashindani ya Quraani.

Inafaa ifahamike kuwa Mawahabi wanajulikana kuwa wanatukufirisha na kututoa nje ya Uislamu, nao ni watu wenye misimamo mikali inayofikia hata kushutumiana wao kwa wao, na Mawahabi hao kamwe hawawezi kukubali ushiriki wa Maibadhi katika shughuli zao husasan za Kidini, kwa hiyo sio kila msunni ni muwahabi.

Ama upande wetu Ibadhi kwanza hatuwatoi Mawahabi nje ya duara la Uislamu hata kama tunawaona kuwa wamo katika upofu na upotevu wa kiitikadi, inajulikana kuwa Imamu mkubwa wa kiwahabi -katika zama hizi- Ibnu Baaz alitoa fatwa ya kukufurisha Maibadhi na kuharamisha kusali yuma ya Ibadhi na kuoana na Maibadhi, basi Sheikh wetu Imam Al-Allaamah Ahmaed bin Hamed Al-Khalili -Allah amuhifadhi- alipomjibu aliulizwa. Jee! Inafaa kwetu sisi kusali nyuma yao? Akajibu: "Sisi hatufanyi kama alivofanya yeye akitangulia katika kusalisha tunasali nyuma yake......"

Ndugu yangu hiyo ndiyo Ibadhi, sisi tunakwenda kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu na si kwa mujibu wa kulipizana kisasi, Madhehebu yetu yanajenga jamii, kamwe hayavunji wala hayasambaratishi jamii, Madhehebu yetu inatutaka tuwe waadilifu, tujiepushe na aina zote za kudhulumu, Madhehebu yetu imetutaka tujifunge vizuri na Quraani na tujiepushe na mapendwa moyo na hasadi na dhana mbaya na uadui.

Pili: Maibadhi walifika Afrika Mashariki mapema sana, pia walifika tena kwa kuwatokomeza walowezi wa Kinasara wa Kireno na kuondosha madhila ya walowezi hao kwa ndugu zetu wa Kiislamu walioishi katika mwambao wa Afrika, hayo yalikua  katika kipindi cha Imam Seif bin Sultan Al-Yaarubi -Allah amridhie- katika Karne ya 12 Hijiria 17 Miladi, na Maibadhi waliweza kuishi pamoja na Waislamu wenzao kwa mashirikiano, na heshima kubwa sana, na mapenzi, bila kujali tafauti zao za Kimadhehebu, wala za urangi, wala za ukabila, hawakukubali kabisa kuzifanya tafauti hizo ziwe kichochezi na kuni za uhasama wa kuibomoa jamii, kwa hiyo mahusiano kati ya Waislamu wa Madhehebu ya Ibadhi na Waislamu wa Madhehebu nyengine katika Afrika Mashariki ni ya zamani sana, wala si aibu, bali ni neema ya kujivunia, Allah aidumishe.

Kwa itkadi yetu Maibadhi tunasema sisi sote -Ibadhi na Sunni- Uislamu umetukusanya hata kama zipo fatauti kati yetu, basi wajibu wetu ni kushirikiana katika tuliyokubaliana na kuheshimiana katika tuliyotafautiana.

Sisi tunatoa Shukurani kwa Al-Hikma Foundation chini ya Uongozi wa Sheikh Kishk kwa kutuletea mwaliko wa kuhudhuria hafala ya Khitimisho la Mashindani ya kuhifaadhi Quraani tukufu ya mwaka 1439/2018, na kwa mapokezi yao mazuri sana ya kupigiwa mfano Allah awajaze kila la kheri.

Na Allah ni shahidi kuwa kipindi chote cha kuwepo kwetu katika Jiji la Dar-Ess-Salaam tulikua bega kwa bega na ndugu zetu wa Kiibadhi ambao nao -kwa taufiqi ya Allah- waliweza kushirikiana na sisi katika kuendeleza daawa, kwa kweli tunatoa shukurani kubwa kwao pia, na sisi tulihudhuria katika mashindani ya Quraani tukufu ya Kitaifa ambayo Istiqamah waliyafanya hapo hapo Dar-Ess-Salaam.

Ama masuala ya kusaidia katika milango ya kheri hayo yanaihusu jumuia husika ile inayotoa misaada na misingi yake katika hilo, na sisi si wasemaji wa Jumuia yoyote.

Allah azikubali amali njema na asamehe katika mapungufu na kuteleza.

Tunawambia tu: "Wa karibu wana haki zaidi katika kutendewa wema."

Wallaahu aalamu. 

Read 4107 times
Sh. Hafidh Al-Sawafi

ibadhi.com | This email address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it.
Add comment


FaLang translation system by Faboba