Ibadhi.com

112:HUKMU YA KUMUOA MWANAMKE ALIYEZINI NAYE.

You have a new Question by:

Bakari Omary from

Tanzania

--------------------------------------

Swali:

Je inajafaa kumuoa mwanamke ulliye zini nae..? Na ipi hukumu yake...?

JAWABU:
Waalykum salaam warahmatullah wabarakatuh.
NDOA HIYO NI HARAMU kwa sababu:

KWANZA: inajulikanwa kuwa ndoa ni fungamano tukufu linalojengwa katika kuaminiana ili kupata upendo na huruma kwa wanandoa. Na bila shaka baina ya waliokwisha kuzini inakosekana kuaminiana baina ya hawa watu wawili kwa kila mmoja kuijua khiyana ya mwingine, kama ambavyo anakosa amani ya kwamba mwenzie hatomkhini huko alipo.

Pili: Zinaa ni kuivunja heshima ya mwanamke na familia yake kwa ujumla, na mvunjifu wa heshima hatakiwi kupewa zawadi Bali kupewa adabu ya uvunjifu wake wa heshima, na kwa ajili hiyo uislam umeweka mijeledi mia moja ikiwa hajaoa au kuolewa, amma ikiwa ameoa au kuolewa kabla basi adabu yake ni kupigwa mawe mpaka afe ili akome yeye na wengine kuchezea heshima za watu, ajabu ya zama hizi ni kuwa mzinifua badala ya kupewa adabu anapewa mke kwa ndoa za mkeka au kwa njia nyingine, yaani kwa ufupi anapongezwa hadharani kwa kuvunja heshima na anapewa zawadi. Subhaanallah... Basi kuna udhalili kuliko huo?

TATU: Mtu akifanya madhambi yatakiwa ajistiri, aombe touba sio kuhalalisha madhambi yake, kama wafanyavyo wazinifu, na uislam umeharamisha mtu kumuuliza mwanamke kwa vipi imeondoka bikira yake? Bali hata akilazimishwa kusema uislam unamtaka mwanamke atafute lolote la kusema lakini asiseme yaliyopita kama aliingia katika uchafu wa zinaa, kwani akikiri tu kuwa alizini ndoa itakuwa imevunjika, na kwa utaratibu huu khofu ya kusema ataolewa na nani haipo aslani, kama ambavyo Allah mtukufu ndio mpangaji wa riziki.

NNE: Ikiwa wanandoa watalaaniana kwa kutuhumiana kuzini basi ndoa itakuwa imekufa hapo hapo kwa makubaliano ya waislam wote, basi ikiwa kutuhumiana zina tu kunaharibu vipi itakuwa hukmu ya waliozini kabisa?? Bila shaka ni wasikutane kabisa milele.

TANO: Kulinda heshima na utukufu wa watoto, kwani kikawaida watoto hujihisi unyonge pale wajuapo kuwa wazee wao walikuwa vimada kabla, kama ambavyo hilo litapelekea kuingia tabia hiyo kwao wao na hivyo kueneza uchafu wa zinaa katika jamii.

SITA: kuhalalisha ndoa hizi kunapelekea kuenea kwa uchafu wa kuwazini wanawake kwa hoja ya kuwadanganya kuwa watawaoa, na hili lipo wazi kuliko jua LA mchana, mabinti wangapi wameharibiwa kwa kuambiwa wataolewa kisha wakaachwa na mizigo ya malezi ya watoto wa nje hata imekuwa kila mtoto ana baba yake... Wallahu l mustaan. Bora mlango huu ufungwe na ajue kila binti kuwa akiziniwa na ndoa hakuna... Ili ajistiri na asidanganywe na mbwa mwitu.

SABA: Kuchanganyika kwa mirathi, nasabu, na haki, kwani wengi katika wazinifu huficha mimba walizozipata katika uzinifu wao, kwa kuoana haraka.. Na hili lina athari mbaya ya dhulma katika haki mbali mbali. Bali linapelekea kutokea kwa ndoa za haram baadaye.

NANE: Kuchanganyika kwa watoto wa wengine kwa baba huyo. Kwani inajulikana kuwa mwanamke mzinifu au mwanamme mzinifu sio wa mtu mmoja, basi nini kijulishacho kuwa watoto wote ni wake, utaona watu wanaishi kwa wasiwasi.

TISA: kuwepo kwa Qauli ya Allah mtukufu yenye kuharamisha ndoa hizo aliposema:
(الزَّانِي لَا يَنْكِحُ إِلَّا زَانِيَةً أَوْ مُشْرِكَةً وَالزَّانِيَةُ لَا يَنْكِحُهَا إِلَّا زَانٍ أَوْ مُشْرِكٌ ۚ وَحُرِّمَ ذَٰلِكَ عَلَى الْمُؤْمِنِينَ)
(Kikawaida) Mzinifu mwanamme hapendi kuoa ispokuwa mzinifu au mshirikina, na mzinifu mwanamke hapendi kuolewa ispokuwa na mzinifu au mshirikina, NA NDOA HIYO IMEHARAMISHWA KWA WAUMINI"
[Surat An-Nur 3]

KUMI: Pia imeharamishwa na Allah mtukufu katika Kauli yake:
(.... ۚ فَانْكِحُوهُنَّ بِإِذْنِ أَهْلِهِنَّ وَآتُوهُنَّ أُجُورَهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ مُحْصَنَاتٍ غَيْرَ مُسَافِحَاتٍ وَلَا مُتَّخِذَاتِ أَخْدَانٍ ۚ... )
"Waoeni kwa idhni ya watu wao, na wapeni mahari yao kwa wema, wanawake waliojihifadhi sio Malaya wala waliofanywa vimada (Uhawara)...
[Surat An-Nisa' 25]
Basi tuambiane tangu lini mtu anayemjua mwenziwe kuwa ni mzinifu amekuwa aliyejihifadhi???

KUMI NA MOJA:
Kuchukua hukmu yenye salama katika masuala, kwani ikiwa wataoana ambao hawajaziniana ummah mzima wanasema ndoa imetimia, amma akimuoa aliyekwisha mzini basi atakauwa ameingia katika Khilaf za wanachuoni, na kutoka katika khilafu ni bora kuliko kuingia.

KUMI NA MBILI:
Wanachuoni wameweka Kanuni mashuhuri ya kuwa MWENYE KUHARAKISHA JAMBO KABLA YA WAKATI WAKE ANAHUKUMIWA KUNYIMWA KWAKE.

Na mwenye kuharakisha kulamba asali kabla hajaruhusiwa kuilamba anaharamishiwa bila shaka. Kwa mujibu wa kanuni hii.

KUMI NA TATU: IJMAA YA MASAHABA
Wamekubaliana Masahaba kuwa ndoa hiyo ni haramu, kupitia hukmu ya Sayyidna Omar pale wakipoletwa waliooana katika EDA ya mwanamke, akawaachanisha kisha akasema: Ikiwa amemuingilia basi itakuwa haram kukutana kwao tena milele na ikiwa hajamuingilia ataruhusiwa kumuoa baada ya eda"
Na bila shaka hapa Sababu ya kutooana tena milele ni Zinaa, kwani kumuoa ndani ya EDA, ndoa haitimii na kwa hivyo inakuwa ni Zina. Ndio akasema: law angemuingilia angemharamikia milele.
kaipokea Imam Malik Amesema Albaaji naye ni mwananchuon wa kimaaliki kuwa hiyo ilikuwa ni Ijmaa ya masahaba kwa sababu haikupokewa kuwa yupo aliyepinga.

KUMI NA NNE:
Kuthibiti kwa riwaya za wazi kutoka kwa baadhi ya masahaba zikipandishwa mpaka kwa Mtume -sallallahu alayhinwasallam- kukataza ndoa hii, kutoka kwa Bii Aisha, na Sahaba Albaraa bin Aazib, na wengineo kuwa wamesema kuhusu wazinifu wawili watakao oana "Wao watakuwa wanaendeleza zinaa muda wote wakiwa pamoja" Amesema Sheikh Alqutb Allah amrehem katika kitabu Sharh Niil : "Hizi ni riwaya zinazonyanyuliwa mpaka kwa mtume -Sallallahu alayhi wasallam- kwani haya ni katika mambo yisyoongelewa kwa rai"
Na riwaya nyingine inasema kuwa wamesema: [- Mwanamke na mwanamme waliozini wakataka kuoana- wekeni baina yao bahari ya kijani - ili wasikutane milele-"

KUMI NA TANO:
MAKUBALIANO YA MADHEHEBU YA IBADHI.

wamekubaliana wanachuoni wote wa madhehebu ya Ibadhi kuwa ndoa hiyo ni batili, na katika lisilo na shaka ni kuwa Maimam wa Kiibadhi wa mwanzo walikuwepo kabla ya wanachuoni wengine wote, kwani Imam wao wa kwanza Imam Jabir bin Zeid kazaliwa mwaka 18 au 21 hijri katika zama za Ukhalifa wa Sayyid Umar bin Alkhattab. Wakati Imam wa mwanzo wa madhehebu za kishia na kisunni wamezaliwa mwaka 80h. Au kabla ya hapo kwa kidogo.
Kwa hivyo Ijmaa ya wanachuoni wa kiibadhi imezitangulia khilaf za wanachuoni wengine. Na hivyo yenyewe ni yenye kutangulizwa.

Haya ni kwa alivotuwezesha Allah mtukufu kunukuu kwa haraka, bila ya kurejea na bila shaka kwa kurejea kuna dalili zaidi ya hizo, tunamuomba Allah mtukufu atulipe katika kupatia na atughufurie tulipokosea. Na kwa ufupi zaidi waweza kurejea risala aloiandika Sheikh wangu Hafidh Alsawwafi -Allah mtukufu amhifadhi- juu ya ndoa kama hii, nayo IPO katika website yetu [ibadhi.com] sehemu ya vitabu, kwa lugha ya kiswahili.
Wallahu aalam.

Ameyaandika
Khamis Yahya Alghammawi

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment