Ibadhi.com

108:NINI HUKMU YA MTU MWENYE DHARAU NA KIBRI ?

Hamed from

Tanzania

--------------------------------------

Swali:

Nini Hukmu ya mwanadamu mwenye kiburi na dharau?

JAWABU:

Hawi na dharau na kibri ispokuwa mtu aliye na mapungufu mengi anayotaka kuyafunika kwa kujipandisha na kuwadharau wengine.

KIBRI ni sifa ya Allah mtukufu basi atakayejipa sifa hiyo atakuwa amestahiki adhabu ya milele katika moto wa Jahannam kama atakufa bila kutubia.

Kwani imepokewa katika hadithi sahihi kuwa Mtume amesema:

(لا يدخُلُ الجنَّةَ عبدٌ في قلْبِهِ مثقالُ ذرَّةٍ مِنَ الكبرِ )

[Haingii peponi Mja ambaye moyoni mwake muna chembe ya kibri]

Na imepokewa katika hadith Qudsi kuwa Allah mtukufu amesema :

الكبرياءُ رِدائي ، والعظمةُ إِزاري ، فمن نازعَني واحدًا منهما ، قذفْتُه في النارِ .

[Kibri na utukufu ni mavazi yangu (sifa zangu), atakayeninyang'anya moja ya viwili hivyo nitamtupa motoni]

Na bila shaka sifa ya kibri si sifa ya waumini bali ni sifa ya waovu, wanafiki, na makafiri na wote hao wameiga kutoka asili ya shari, Ibilisi - Allah mtukufu amlaani-; Amesema Allah mtukufu:

(إِلَّا إِبْلِيسَ اسْتَكْبَرَ وَكَانَ مِنَ الْكَافِرِينَ)

[Ispokuwa Ibilisi -hakusujudu- alifanya kibri na akawa katika Makafiri]

{Surat Sad 74}

Kama ambavyo dharau pia ni katika sifa za Unafiki, ambazo zimeigwa kutoka kwa wapingaji wa Mitume nao wakiiga kutoka kwa Ibilisi aliyelaaniwa, kwani ni yeye aliyeweka misingi ya kudharau wengine pale alipomdharau Adam kwa sababu ya asili yake ya udongo akasema kwa majivuni:

(قَالَ أَنَا خَيْرٌ مِنْهُ ۖ خَلَقْتَنِي مِنْ نَارٍ وَخَلَقْتَهُ مِنْ طِينٍ)

[Akasema: Mimi ni bora kuliko yeye; umeniumba kwa moto na umemuumba yeye kwa udongo]

{Surat Sad 76}

Kwa hivyo mwenye kuchukua tabia hiyo amejufananisha na mlaanifu huyo, basi ajiandae ukaaji wa milele katika Moto wa Jahannam kama hakutubia.

Pamoja na hayo mtu huyo aitapata adhabu ya Allah mtukufu hapa duniani ili akumbushwe kwani maradhi hayo ni maradhi ya moyoni, ambayo yamejificha katika nafsi kama mdudu chungu mweusi katika weusi wa kiza cha usiku akiwa katika jiwe kubwa. Hivyo atakayekuwa katika madhambi haya atapata adhabu za kumkumbusha na kumrejesha akikumbuka basi kheri yake akisahau au akadharau basi khasara iliyoje ya kughafilika huko. Na itoshe hali ya mwenye bustani kuwa ni mazingatio pale apoingia bustanini kwale akijivika kibri na kuwadharau wana bustani wenziwe kwa kusema :

(وَدَخَلَ جَنَّتَهُ وَهُوَ ظَالِمٌ لِنَفْسِهِ قَالَ مَا أَظُنُّ أَنْ تَبِيدَ هَٰذِهِ أَبَدًا * وَمَا أَظُنُّ السَّاعَةَ قَائِمَةً وَلَئِنْ رُدِدْتُ إِلَىٰ رَبِّي لَأَجِدَنَّ خَيْرًا مِنْهَا مُنْقَلَبًا)

Akaingia bustanini kwake akiwa ni mwenye kuidhulum nafsi yake, akasema: Sidhani kama hivi vitu vitakwisha, wala sidhani kwamba Qiyama kitasimama]

[Surat Al-Kahf 35 - 36]

Akaonesha dharau ya wazi kwa mwenziye aliyepewa mtihani wa uchache wa rizki kwa kumwambia kwa fakhari na majivuni:

(وَكَانَ لَهُ ثَمَرٌ فَقَالَ لِصَاحِبِهِ وَهُوَ يُحَاوِرُهُ أَنَا أَكْثَرُ مِنْكَ مَالًا وَأَعَزُّ نَفَرًا)

[Na alikuwa na matunda -bustanini kwake- akasema kumwambia mwenziwe walipokuwa wanajadiliana: Mimi Nina Mali nyingi zaidi na mwenye nguvu ya watu wengi zaidi]

[Surat Al-Kahf 34]

Allah mtukufu akaiharibu ile mali ilokuwa ikimpa kibri na dharau kwa wenziwe akatueleza hayo kwa kusema:

(وَأُحِيطَ بِثَمَرِهِ فَأَصْبَحَ يُقَلِّبُ كَفَّيْهِ عَلَىٰ مَا أَنْفَقَ فِيهَا وَهِيَ خَاوِيَةٌ عَلَىٰ عُرُوشِهَا وَيَقُولُ يَا لَيْتَنِي لَمْ أُشْرِكْ بِرَبِّي أَحَدًا)

[Yakazungukwa matunda yake usiku ule kwa adhabu, ikawa asubuhi yake anajuta kwa Yale aliyotoa kuihudumia bustani, nayo ipo tupu haina chochote, hali akisema: Yaa leit nisingemshirikisha mola wangu na yoyote]

{Surat Al-Kahf 42}

Basi hiyo ndiyo hali ya mwenye kibri na dharau hapa duniani, Allah mtukufu humuadhibu hapa duniani na kesho Akhera hali yake itakuwa mbaya zaidi.

Basi amche Allah mtukufu mwenye sifa hii mbaya, na kwa lipi kubwa alilofanya mwanadamu hata awe na kibri na dharau kwa wengine ?

Allah mtukufu atukinge na sifa hizi mbaya.

Wallahu aalam.

Ameyaandika:

Khamis Yahya Alghammawi

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment