Ibadhi.com

84:JINSI YA KUKOSHA MAITI

You have a new Question by:

Hamed Shaffi from

Tanzania

--------------------------------------

Swali:

Jinsi ya kuosha maiti.

JAWABU:

Waalayku Salaam.
Ni wajibu wa kutoshelezana kwa walio hai kumkosha aliyekufa akiwa muislam, na ikiwa maiti wa kiislam hatokoshwa basi dhambi zitawaenea wanajamii husika wote.

Jambo la mwanzo afanyiwalo maiti wa kiislam ni kufunikwa macho yake na mdomo wake, kisha huvuliwa nguo zake za kawaida na kufunikwa shuka, kisha maiti hutayarishwa kwa kukoshwa (( kunyooshwa viungo vyake, na kuondosha vilivozidi katika mwili wake))

Maji ya moto yasiyounguza ((uvuguvugu)) hutumika katika kumkosha maiti, pia sabuni yenye manukato au majani ya mkunazi au vinavyoweza kusimama sehemu yake hutumika.

Maiti huanzwa kwa kutolewa haja kubwa na ndogo zilizobakia katika njia zake, hii inakuwa kwa kulibinya kwa upole tumbo lake, na ili iwe rahisi zaidi, ni vyema kumkalisha kwa mtu kumuegemeza katika magoti yake, kiasi itakuwa njia ya tumbo lake imeelekea kwa chini na kila kisichohitajika kitateremka kwa wepesi kabisa. Wakati huo itakuwa anamiminiwa maji ili kutoka kwa haja yake kuendane na kusafika.

Anayekosha atamstanji mpaka ahakikishe najisi yote imemalizika wala haitoki tena, na hiyo itakuwa kwa kuchukua kitambaa kisafi cheupe au gloves na kumstanjia ili kuhakiki kuwa hakijachafuka hat kidogo, hapo atajua kuwa tayari amesafika.

Baada ya hapo, atapigishwa mswaki kwa kitambaa safi kukipitisha katika meno, kisha atatilishwa udhu kama wa sala.

Kisha ataanzwa kumwagiwa maji sehem za kichwa pamoja na kuzuwiya matundu yote yasipitishe maji kuingia ndani.

Kisha atakoshwa sehem za kulia kwa mbele, kisha Sehem za kushoto kwa mbele.

Kisha atalazwa upande wa kushoto ili akoshwe upande wa kulia wa mgongoni kwake kuteremka chini mpaka miguuni, kisha atalazwa upande wa kulia ili akoshwe upande wa kushoto wa mgongo wake kuteremka chini mpaka miguuni. Si vibaya kutumia sabuni katika josho hili.

Kisha atamwagiwa maji yalotewa mafuta mazuri au majani ya mkunazi mwili mzima kufuata Sunnah ya Mtume -Sallallahu alayhi wasallam-.

Atakaushwa maji yake kwa kubadilisha shuka bila kumfunua mwili wote akaonekana.
Na hapo atakuwa tayari kwa kuvikwa sanda.

Muhimu ni kuwa hatua zote hizo zitatimia hali ya kuwa amefunikwa na kusitiriwa, pia mkoshaji awe amevaa kitambaa na ajiepushe kufanya lolote linalovunja heshima ya maiti huyo, na wala asiuguse utupu wake ispokuwa kwa dharura tu.

Mwisho, uandishi si kama kuona amali yenyewe, hivyo nakushauri uingie katika wakoshaji ili upate mazoezi na uzoefu.
Wallahu aalam.

Ameyaandika Mja dhaifu:
Khamis bin Yahya Alghammawi
Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
8 February 2018m
Jeddah, Saudi Arabia.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment