Ibadhi.com

81:WAZAZI WANALAZIMISHA NIMUOE MWANAMKE NISIYEMTAKA.

WAZAZI WANALAZIMISHA NIMUOE MWANAMKE NISIYEMTAKA.

Assalaykum sheikh ! Shekhe mm ni kijana mwenye umri wa miaka 24, nimempenda binti fulani ambaye nataka kumuoa ila upande wa kwetu mm mwanaume wazee wanaleta pingamizi zao kwa kuleta dosari kuwa hawataki nioe mke kutoka upande fulani wa nchi, je nawezafunga ndoa bila ya kuwashirikisha wazee wangu? Kwasababu wao wamekataa na wanataka wanichagulie ambae mm simtaki! Naomba msaada / majibu sheikh!

JAWABU;
Waalaykum salaam warahmatullah wabarakatuh.

Ndugu yangu Kijana, jua kuwa ndoa ni muunganiko wa familia moja na nyingine, kwani mwanamme atapata mama na baba wengine, na mashemeji na watoto wake watakuwa na ma anko na makhaloo. Kama ambavyo mwanamke pia.
Na kwa ajili hii inatakiwa kuwe kuna muwafaqa wa familia mbili pale inapotokea kutaka kuoana baina ya familia moja na nyingine. Lakini kukubaliana huku si lazima kisheria ispokuwa ni kwa ajili ya kuhakikisha utulivu wa hao wanandoa wawili.
وَمِنْ آيَاتِهِ أَنْ خَلَقَ لَكُمْ مِنْ أَنْفُسِكُمْ أَزْوَاجًا لِتَسْكُنُوا إِلَيْهَا وَجَعَلَ بَيْنَكُمْ مَوَدَّةً وَرَحْمَةً ۚ إِنَّ فِي ذَٰلِكَ لَآيَاتٍ لِقَوْمٍ يَتَفَكَّرُونَ

Na katika Ishara zake ni kuwa amekuumbieni wake zenu kutokana na nafsi zenu ili mpate utulivu kwao. Naye amejaalia mapenzi na huruma baina yenu. Hakika katika haya bila ya shaka zipo Ishara kwa watu wanao fikiri.
((Sura Ar-Rum, Ayah 21))

Basi hebu niambie ndugu yangu, ataishi vipi mwanamke hali hakubaliki na wazazi wako wawili na inawezekana na ndugu zako wengine ? Atautoa wapi utulivu na furaha ya nafsi? Bali hata wewe utakuwaje uhusiano wako na wazazi wako baada ya kuasi amri yao ?

Kwa hivyo usilitazame jambo hili kwa mtazamo wa kushibisha matamanio ya nafsi yako tu..!!

Pamoja na haya wazazi sehem yao ni kubwa maadam hawakukhalifu sheria katika waliloamrisha, Amesema Allah mtukufu:
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِنْدَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُلْ لَهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُلْ لَهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا

Na Mola wako Mlezi ameamrisha kuwa msimuabudu yeyote ila Yeye tu, na wazazi wawili muwatendee wema. Mmoja wao akifikia uzee, naye yuko kwako, au wote wawili, basi usimwambie hata: Ah! Wala usiwakemee. Na sema nao kwa msemo wa hishima.
((Sura Al-Isra', Ayah 23))

Haya tuliyosema hayana maana kuwa wazazi wana haki ya kuwalazimisha watoto wao katika kuchagua mwenzi wa maisha yao, haasha..!!

Pia wao inatakiwa wawasikilize watoto matakwa yao, wawaelekeze kwa mashauriano na majadiliano matulivu yenye lengo ya kujenga sio kubomoa. Pia wafahamishwe kwa uzuri rai ya dini yetu tukufu kuwa mazingatio sio utaifa ambao ni harufu mbaya ilopandikizwa na wakoloni katika kugawa taifa kubwa la waislam linalotakiwa kuwa chini ya Khalifa wa kiislam. Mazingatio ni Dini na Akhlaaq. Na haiwi kwao wao wazazi kupingana na amri ya Allah mtukufu na Mtume wake kwa matamanio ya nafsi zao.

وَمَا كَانَ لِمُؤْمِنٍ وَلَا مُؤْمِنَةٍ إِذَا قَضَى اللَّهُ وَرَسُولُهُ أَمْرًا أَنْ يَكُونَ لَهُمُ الْخِيَرَةُ مِنْ أَمْرِهِمْ ۗ وَمَنْ يَعْصِ اللَّهَ وَرَسُولَهُ فَقَدْ ضَلَّ ضَلَالًا مُبِينًا

Haiwi kwa Muumini mwanamume wala Muumini mwanamke kuwa na khiari katika jambo, Allah mtukufu na Mtume wake wanapo kata shauri katika jambo lao. Na mwenye kumuasi Allah mtukufu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi.

((Sura Al-Ahzab, Ayah 36))

Pia tunaona kuwa wewe uwakinaishe wazazi wafaham kwa nini umemchagua huyo binti, na kwa nini humtaki huyo alochaguliwa na wao kwa hishma na adabu, au kwa kuwatuma wanaoweza kuwaambia vizuri wakafahamu. Na ikiwa hapana budi kuyakhalifu matamanio ya nafsi yako kwa kuwaridhisha wao basi ni ujira mkubwa ulioje huo...!!

Katika athari imesemwa:

Radhi za Allah mtukufu zipo katika Radhi za wazee wawili, na Machukizo ya Allah mtukifu yapo katika Machukizo ya wazee wawili.
Wallahu aalam.

Ameyaandika mja dhaifu
Khamis bin Yahya Alghammawi
Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
8 Febr 2018
Makkatul Mukarrama.

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment