Ibadhi.com

33: Je hili jina la Hawa lilitoka wapi ? nani alikuwa akiitwa mke wa Adam [AS}

SWALI:

Asalaam alee'kum Sheikh. Baada ya kuumbwa mbingu,dunia na vingemevyo, Allah alimuumba Adam na pia akampatia mfariji wake ambaye sote tunajua kwa jina BIi Hawa, lakini ukiuangalia msahafu kwa makini. hakuna sura ye yote katika Qur'aani, ambapo Allah kamtaja Bi Hawa kwa jina hili.ila Allah kataja majina ya manaabii kwa majina yao, pia katajwa Bi Maryam basi kwa jina lake,ikiwa ni mwamke pekeyake kutajwa jina katika Qur'aan Kareem. Je? hili jina la Hawa lilitoka wapi?? nani alikuwa akiitwa mke wa Adam [AS}

JAWABU:
Waaleykum salaam warahatullah wabarakatuh.

Qur an tukufu imetutajia kila lilokuwa linahitajika katika maisha yetu, na lenye tija kwa dini na dunia yetu, Amesema Allah mtukufu:
Na hapana mnyama katika ardhi, wala ndege anaye ruka kwa mbawa zake mbili, ila ni umma kama nyinyi. Hatukupuuza Kitabuni kitu chochote. Kisha kwa Mola wao Mlezi watakusanywa. An'am :38

Na wale alowataka Allah mtukufu tuwajue kwa majina yao aliwataja katika kitabu chake, na wengine alitaka tujue matendo yao na misimamo yao tu, mfano wa hao ni: Mke wa Nabii Lut, Mke wa Nabii Nuh, na wengineo.
Hivyo mke wa Adam si yeye tu ambaye hakutajwa.

Amma katika Sunnah, Amesema Sheikh Ismail bin Nassor Al oufi - Allah amuhifadhi - "Hakuna lilothibiti katika kulitaja jina la Hawa kama mke wa Adam," na yale yalotajwa imma yanaingia katika udhaifu au kuwa hayatoi hukmu ya Yaqini, na makadirio ya juu yamechukuliwa kutoka katika riwaya za Ahlil kitaab.

Miongoni mwa riwaya hizo :
Amepokea Bukhari 3399, Muslim 1470, Tirmidhi 3077
Kutoka kwa Abi Huraira kuwa Mtume s.a.w. amesema

لولا بني إسرائيل لم يخنز اللحم ، ولولا حواء لم تخن أنثى زوجها الدهر

"Kama si bani Israil isingeharibika nyama, na kama si Hawa basi hakuna mwanamke ambaye angemfanyia khiyana mme wake"

Na Riwaya nyingine aloipokea Al uqeily jz 3 uk 327 mesema :
لولا بنو إسرائيل خبئوا اللحم ما خنز اللحم ولولا حواء خانت آدم في قولها لإبليس ما خانت امرأة زوجها
Kama si Bani Israil kuficha nyama, nyama zisingeharibika na kutoa harufu, na kama si Hawa kumfanyia khiyana Adam kwa kumwambia Ibilisi, basi kusingekuwa na khiyana ya mke kwa mmewe"

Na haijifichi kwako baadhi ya ishkaalat zilizopo katika hadithi hizi, ikiwemo kugongana kwake na Qur an, kwani Qur an inatuhadithia kuwa uasi uliwapata wote sawia, bali majukumu yote na lawama tunaona alibebeshwa Adam, na katika biblia toleo la kale tunakuta mithali ya ibara hizi zenye kuashiria kuwa mwanamke ndiye asili ya upotevu, na hivyo alistahiki kuzaa kwa uchungu, na mwanamme kwa kupotezwa kwake akastahiki kutafuta rizki kwa jasho. Hayo nimeyasoma zamani katika biblia ya agano la kale.

Pia katika riwaya hizo kuna kuwabebesha mzigo wa dhambi ya kufuatia wanawake wote wa dunia, kwa khiyana moja ilozushwa kutokea, wakati Allah mtukufu anasema :
Anaye ongoka basi anaongoka kwa ajili ya nafsi yake. Na anaye potea basi anapotea kwa khasara yake mwenyewe. Wala habebi mbebaji mzigo wa mwengine. Wala Sisi hatuadhibu mpaka tumpeleke Mtume. 17:15

Kutokana na hayo inapata nguvu kauli ya kuwa inawezekana kuwa hilo limesikiwa kutoka kwa banii Israil, na wapokezi wakalichanganya wakalielekeza kuwa Mtume s.a.w. ndio kalisema, kwani ni maarufu kuwa Sahaba Abi Huraira R.A. alikuwa akihadithia kutoka katika baadhi ya vitabu vya bani Israil, na wapokezi wakichanganya hayo na kuyaegemeza kwa Mtume kama alivyosema Saeed bin Wahb " jichungeni sana na hadithi, kwani tumewaona watu wakichanganya mapokezi ya Abu huraira kutika kwa Kaab na kutoka kwa Mtume s.a.w., wakiyafanya ya Mtume s.a.w. kuwa ya Kaab na wakiyafanya ya Kaab kuwa ya Mtume s.a.w."

Hivyo, hilo si jambo la kiitikadi, na si muhimu kwetu sisi kujua jina lake, kwani angelitaka Allah mtukufu tulijue angetutajia katika kitabu chake kitukufu.

Wallahu Aalam.
Abu Muslim Alghammawi
21.03.2017m

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment