Ibadhi.com

30:imi nauliza juu ya maana ya hadithi ya Mtume (S.A.W.) aliposema kwamba Ummat utagawanyika katika mapote/makundi 73

SWALI:
Assalaam alaikum. Mimi nauliza juu ya maana ya hadithi ya Mtume (S.A.W.) aliposema kwamba Ummat utagawanyika katika mapote/makundi 73 na yote hayo yatakwenda motoni isipokuwa kundi moja , je haya makundi yaliyopo leo si katika makundi yale 73 aliyoyasema Mtume ? Mfano wa makundi hayo ni Shiaa, Ibadhi, Sunni na mengineyo. Shukran.


JAWABU.
Waalaykum salaam.
Hadithi hiyo uloitaja ndugu yangu ni hadithi sahihi imepokewa na wengi katika wanachuoni sahihi kwa njia sahihi, katika hao ni Imaam Rabii bin Habib R.A. katika Musnad yake no: 41 amepokea Imaam Abu Ubaidah kutoka kwa Imaam Jabir bin Zaid kutoka kwa Ibn Abbas R.A. kutoka kwa Mtume S.A.W. amesema “Ummah wangu utagawanyika makundi sabini na tatu, yote yatakwenda motoni ispokuwa moja tu, na kila kundi linadai kuwa ndio hilo moja” pia wameipokea Abu daawud, Tirmidhi, Nasaai, n.k.kwa lafdhi zenye tofauti ndogo.
Katika hadithi zingine Mtume s.a.w. ametaja kundi hilo ni lile litakaloshikamana na Sunna zake na mwenendo wa Makhalifa waongofu, walioongoka na kujiweka mbali na yatakayozuka katika dini kwani kila uzushi mbaya ni upotevu. (( kapokea Abu Daawud na Tirmidhi )).
Na makubaliano ya Ummah yapo kuwa makhalifa Abubakri, Umar na nusu ya utawala wa Uthman na Ally ilikuwa ni uadilifu, na nusu nyingine ya ukhalifa wa Uthman na Ally masahaba walitofautiana hata wakapigana vita, na kuuana.
Na wamekubaliana kuwa ufalme wa Banii Umayya na Bani Abbasi ulikuwa uasi wa wazi dhidi ya dola ya uongofu wa Mtume s.a.w.
Kwa maana hiyo, muislam atakayeshikamana na Sunnah ya Mtume s.a.w. na mwenendo wa makhalifa waongofu kabla ya kukhitalafiana baina yao, atakuwe,o katika kundi litakalo okoka, inshalla.
Pia hapana budi kuyapima yale yalopokewa kuwa ni ya Mtume S.A.W. au ni ya makhalifa wake waongofu kabla ya kutofautiana baina yao, kwa kuwa waongo wengi wameyaegemeza mambo yao kwao, kwa kutunga hadithi na riwaya.

Hivyo si kila kitakachosemwa kuwa kimetoka kwa Mtume na makhalfa waongofu kitakubaliwa mpaka kipimwe katika mizani tatu:
1. ISIPINGANE NA QUR AN


Abu Ubaidat kutoka kwa Jabir bin Zaid kutoka kwa Ibn Abbas R,A, kutoka Mtume S.A.W. amesema “ Hakika nyinyi mtatofautiana baada yangu, basi kila kitakachokujieni kutoka kwangu kipimeni katika kitabu cha Allah mtukufu, kitakachokubaliana nacho basi kimetoka kwangu, na kitakachopingana nacho hicho hakijatoka kwangu” ameipokea Rabii bin Habiib katika musnad no 40.
2. ISIPINGANE NA SUNNAH ILIYOKUBALIKA


Amesema Mtume s.a.w. “ Haiwi kwa Allah mtukufu kuukusanya ummah wake katika upotofu” Musnad Imaam Rabii R.A. no 39
3. ISIPINGANE NA MALAZIMISHO YA KIAKILI

Amesema Allah mtukufu: Watasema watu wa motoni “Na watasema: Lau kuwa tungeli sikia, au tungeli kuwa na akili, tusingeli kuwa katika watu wa Motoni!" Mulk : 10
4. ITATAZAMWA MFUATANO WA WAPOKEZI

Amesema Allah mtukufu: “Enyi mlio amini! Akikujieni mpotovu na khabari yoyote, ichunguzeni, msije mkawasibu watu kwa kuto jua, na mkawa tena wenye kujuta kwa mliyo yatenda" Hujuraat:06
5. ISIWE NA MAGONJWA YA MATN kama mgongano n.k.

Amesema Allah mtukufu: “Hebu hawaizingatii hii Qur'ani? Na lau kuwa imetoka kwa asiye kuwa Mwenyezi Mungu bila ya shaka wangeli kuta ndani yake khitilafu nyingi” Nisaa: 82
Habari hii ikitimiza masharti haya, ikiwa ni Mutawaatir (( imepokewa na wengi wasioweza kukubaliana katika uongo )) itachukuliwa katika mambo ya itikadi na mengineyo, amma ikiwa imepokelewa na wachache basi haitotumika katika itikadi, kwa kuwa bado itakuwa na dhana ya kutosihi na itikadi yatakiwa yaqini moja kwa moja. Kwa kuwa itikadi inayohusiana na kumjua Allah mtukufu ambaye yeye ni Yaqinii isiyokubali shaka, Amesema Allah mtukufu: “Basi jua ya kwamba hapana mungu ila Mwenyezi Mungu,” Muhammad:19
Hivyo madhehebu, vikundi, watu, sharia zote, na mienendo yote itapimwa hapo na kupewa hukumu ya upotevu au uongofu sio kwa kutazama majina. Amma idadi iliyotajwa haikukusudiwa umaalumu wake bali wingi wake yaani njia nyingi zitakuwa upotevu na njia ya Mtume S.A.W. na makhalifa wake waongofu itakuwa ni haki.
Mwisho: Allah mtukufu amufupishia njia ya kundi hili kwa kuwaita wachamungu na kusema pepo wameandaliwa wao, si mwingine yoyote, Amesema Allah mtukufu: " Hiyo ndiyo Pepo tutayo warithisha katika waja wetu walio kuwa wachamngu” Maryam:63, kwa hivyo jitahidi uwe katika wao kwa kuifauata HAKI KWA DALILI.
Wassalaam Alaikum warahmatullah wabarakatuhu.


Sh. Abu Muslim Khamis Alghammawi

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment